Jeshi la Polisi Kikosi cha Uokoaji jana kililazimika kutumia nguvu
kuwaokoa wakazi wawili wa Jangwani waliokuwa wamezingirwa na maji,
lakini wakigoma kuokolewa
Vifo, uharibifu wa mali, miundombinu na mafuriko, msongamano wa
magari, baadhi ya wakazi wa jiji hilo kukimbia makazi yao, wengine
kulala kwenye magari na nyumba za wageni vimewakumba wakazi wa Jiji la
Dar es Salaam na vitongoji vyake, kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha kwa siku ya nne mfululizo.
Timu ya waandishi wa gazeti hili walifanya
uchunguzi maeneo mbalimbali na kushuhudia hali halisi ilivyo, huku
wanawake na watoto wakionekana kupata shida zaidi kwa kukaa nje ya
nyumba zao, wengine kuhamia kwenye majengo ya shule.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
alisema jana kuwa walikuwa wakiendelea kukusanya taarifa za maafa
ikiwamo vifo alivyosema ni vingi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik alisema kuwa yupo kwenye kikao na watatoa taarifa zaidi za maafa baadaye.
Tegeta, Boko na Bunju
Mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne,
amefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kujaa maji na
kushindwa kujiokoa kutokana na ulemavu, wakati mama yake akiwa kwenye
shughuli za biashara.
Majirani wa mtoto huyo walisema tofauti na kawaida
yao kumtoa mtoto huyo mvua inaponyesha, jana walimsahau na mama yake
aliporejea alikuta maiti ya mtoto wake ikielea chumbani.
Katika mvua hizo takribani kaya 180 zimekumbwa na mafuriko huku wakazi wake wakijikuta hawana pa kwenda.
“Mimi nimekuwa hapa tangu Tanu imezaliwa, nyumba
yangu imejaa maji nimeshazeeka sina mtu wa kunisaidia, wala sijui wapi
nitakwenda. Nomba Serikali inisaidie,”alisema Hussein Ngaoma ambaye ni
mjumbe wa nyumba kumi katika eneo hilo.
Naye Husna Ally ambaye pia nyumba yake imekumbwa
na mafuriko alisema: “Nasikitika, maana nimepata hasara kubwa. Mimi ni
mfanyabiashara katika eneo hili la Boko, nina duka la kuuzia samani
limejaa maji na sijaweza kuokoa chochote. Mzigo wa Sh30 milioni
umeharibika wote.”
Jeti Lumo
Katika eneo hilo licha ya kujaa maji,
mfanyabiashara ndogondogo amefariki dunia kwa kusombwa na maji alipokuwa
akijaribu kuokoa jiko lake la kuchomea mishikaki lililotumbukia kwenye
mtaro.
Wakizungumza na gazeti hili wakazi wakazi wa eneo hilo walisema
kuwa wakati mvua zilipoanza kunyesha, marehemu huyo waliyemtaja kwa jina
moja la Ismail alikuwa akiendelea na kazi yake ya kuchoma nyama kando
ya barabara, lakini baadaye maji yakafurika na kulisomba jiko lake,
ndipo mtu huyo alipoingia kwenye mtaro huo ili alitoe, ndipo akasombwa
na maji yaliyokuwa yakienda kwa kasi.
“Tulikuwa hapa na Ismail tunachoma nyama mvua
ilikuwa inanyesha ghafla maji yakafurika na kubeba jiko, alipoingia
mtaroni kulitoa maji yakamsomba. Nasikitika kuwa hatukuweza kumwokoa
akapoteza maisha,” alisema Mwajuma Said.
Msasani na Mikocheni
Waandishi wetu walishuhudia eneo maarufu la ‘My
fair plaza’ likiwa limezingirwa na maji huku wafanyakazi wakijitahidi
kuyatoa maji, huku wakazi wa Msasani Bonde la Mpunga wakionenekana
kuhangaika kuokoa vitu ndani ya nyumba zao, zilizoingiliwa na maji.
“Mvua ilianza kunyesha jana asubuhi, maji yakazidi
kujaa kama unavyoona tunajitahidi kuokoa vinavyookoleka na tunahofia
kupata magonjwa ya milipuko,” alisema mkazi wa eneo hilo Judith Peter.
Mkwajuni, Jangwani na Kigogo
Katika eneo la Jangwani watu walionekana wakiwa
wamekimbia makazi yao huku wengine wakiokoa baadhi ya vyombo vyao huku
magari ya Kampuni Barabara ya Strabag inayojenga barabara ya magari
yaendayo kasi yakiwa yamefunikwa na maji na umati wa watu ulikiendelea
kushangaa mafuriko.
Baadhi ya wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi eneo la
Vingunguti wamelazimika kugeuza shule kama makazi yao ya muda kwa hofu
ya kukumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Gazeti hili lilifika kwenye Shule ya Msingi
Mtakuja na kushuhudia wanawake, watoto na wanaume wachache wakiwa
wamejikunyata kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa ya shule hiyo
waliyoyafanya makazi ya muda.
Mmoja wa wanawake hao, Amina Said alisema baada ya
mvua kuanza kunyesha juzi jioni maji yalianza kutiririka na kujaa
bondeni karibu na nyumba anayoishi hivyo akalazimika kumchukua mwanawe
na kukimbilia shuleni hapo.
“Nilikuwa sina sehemu nyingine ya kukimbilia na
mtoto hivyo shule na ndiyo ikawa mkombozi. Mafuriko yangetukuta
tusingepona…tulilala kwenye haya madawati na mvua ikiendelea kunyesha
tutaendelea kukaa hapa,” alisema Said.
Mama huyo alisema juzi usiku vyumba vyote saba vya
madarasa ya shule hiyo vilikuwa vimejaa watu waliolazimika kuziacha
nyumba zao na kwenda kulala shuleni hapo.
Huku wengine walilimbilia shuleni walioshindwa kufika nyumbani
kutokana na barabara kufurika maji na kusababisha magari na hata bajaji
kushindwa kutembea hao walilazimika kulala kwenye nyumba za wageni.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wahudumu
katika nyumba ya kulala wageni ya New Kampala iliyopo eneo la Gongo
mboto, Khalid Fikiri alisema walianza kupokea wageni kwa wingi majira ya
saa nne na nusu usiku tofauti na ilivyo siku za kawaida.
“Kwa kawaida tunapokea wageni sita lakini juzi
tulipokea wageni kumi na sita kutokana na kukwama njiani kwa sababu ya
mvua”alibainisha Fikiri.
Alisema kutokana na kutambua uhitaji wa baadhi ya
wageni waliokuwa wanaenda kuomba vyumba vya kulala kwa walikokuwa na
fedha nusu pia waliwapa malazi.
“Tunatozaga 10,000 kwa chumba ila kwa waliokuwa na fedha pungufu hatukusita kuwasaidia,” alikiri Fikiri.
Naye Meneja wa nyumba kulala wageni ya Gladys
Maxmillian Machango alisema alipokea wageni waliokuwa wamekwama na
kushindwa kufika nyumbani kutokana na mvua.
Wawili wagoma kuokolewa
Jeshi la Polisi Kikosi cha Uokoaji jana
kililazimika kutumia nguvu kuwaokoa wakazi wawili wa Jangwani waliokuwa
wamezingirwa na maji, lakini wakigoma kuokolewa.
Katika tukio hilo lililovutia watu wengi, waokoaji
walichukua takriban saa mbili kushawishi wazee hao mwanamke na mwanaume
ili waokolewe, huku wakiendelea na shughuli zao wakati vikosi hivyo
vikijaribu kuwatoa kwa kutumia mtumbwi.
Maofisa wa polisi waliokuwa katika eneo hilo
walionyesha kukerwa na hali hiyo, huku wakiwa wamechanganyikiwa kwa kile
kilechoelezwa kwamba wakitumia nguvu wazee hao wangeweza kujirusha
katika maji yaliyokuwa yamejaa, yakienda kwa kasi hivyo kuhatarisha
maisha.
0 comments:
Post a Comment