LATEST POSTS

Saturday, May 3, 2014

MAALIM SEIF NA KARUME.....WAKUTANA FARAGHA ZANZIBAR.....KUJADILI HATMA YA ZANZIBAR NA KATIBA MPYA








zanzibar. Rais Mstaafu wa Zanzibar awamuya sita, Dk Amani Abeid Karume amekutana na viongozi wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar na kujadiliana hali ya kisiasa iliyojitokeza katika mjadala wa Katiba Mpya, pamoja na kujitoa kwa wabunge wa Ukawa kwenye vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa viongozi hao wamekutana faragha  Aprili 30, nyumbani kwa Rais huyo mstaafu eneo la Mbweni mjini Unguja.
Viongozi wengine walioshiriki mazungumzo hayo ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mkurugenzi wa Uenezi,  Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani, Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo na Katibu Mtendaji wa Kamati hiyo, Mansoor Yussuf Himid. 
Wajumbe wengine katika msafara huo walikuwa ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu na Eddy Riyami huku mjumbe mmoja wa kamati hiyo, Aboubakary Khamis Bakary ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria wa (SMZ) akikosekana.
Imeelezwa kuwa kamati hiyo ilitoa muhtasari wa mwelekeo wa mjadala wa Katiba Mpya  na sababu za wajumbe wa Ukawa kutoshiriki vikao vya Bunge la Katiba.
Kamati hiyo ilitaja ni Bunge hilo kutawaliwa na ushabiki, vijembe, matusi na kebehi, huku  ikielezwa pia kuwapo na dhamira ya kupuuzwa maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji JosephWarioba kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Mzee Moyo aliithibitishia jana kamati yake kukutana na Rais mstaafu Karume, ingawa alikataa kuelezea lolote lililojadiliwa wala kutaja azimio lililofikiwa baada ya kikao hicho kumalizika.
“Ni kweli kamati yangu ilikutana Rais Mstaafu Karume nyumbani kwake, wala si kificho, tumekubaliana  Jussa atakuwa ndiye mzungumzaji wa yale tuliyoyazungumza na kuafikiwa, yeye na  Mansoor ndiyo makatibu watendaji wa kamati yetu,”alisema Mzee Moyo.
Gazeti hili lilipompigia simu Rais Mstaafu Karume ili aeleze ajenda na madhumuni ya kikao hicho, hakuwa tayari kueleza lolote.
Hata hivyo, baada ya kumalizika mkutano huo, baadhi ya viongozi hao akiwamo Maalim Seif , Jussa na Mzee Moyo walikwenda moja kwa moja kushiriki mkutano wa hadhara wa Ukawa uliohutubiwa na 
viongozi wa juu wa CUF, NRA, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi na NLD.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa akizungumza na Mwananchi Jumapili amesema kwamba walikutana na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume kama waanzilishi wa maridhiano ya kupatikana kwa mwafaka wa kisiasa Zanzibar na hatimaye kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema katika mkutano wao na Rais Mstaafu Karume, walizungumza kuhusu jinsi ya kulinda maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa hasa kutokana na kuwapo baadhi ya watu wenye mwelekeo wa kutaka kuvuruga maridhiano hayo.
“Kumeonekana kuwapo watu wenye dhamira ya kuvuruga maridhiano yetu kwa maslahi yao ya kisiasa, hivyo tumetafakari nini tufanye ili kulinda maridhiano,” alisema Jussa.
Kadhalika alisema walizungumzia Mchakato wa Kupata Katiba Mpya jinsi ulivyokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar yanalindwa.
“Yaliyokuwa maoni ya Wazanzibari na yanayoendelea hivi sasa katika Bunge Maalumu la Katiba, ni vitu viwili tofauti, hivyo tunataka kuhakikisha kuwa maoni ya Wazanzibari yanaheshimiwa na haki zao zinalindwa,” alieleza Jussa. 
baadhi ya watu waliokuwa hawakuunga mkono maridhiano hayo, kutaka kuvuruga, wafanye nini kulinda maridhiuano na serikali ya umoja wa kitaifa hasa kutokana na majaribio yanayofanywa na baadhi ya watu ambao wanaonekana kusaka madaraka hata kuvcuruga maridhiano ili wafikie malengo yao ya kisiasa. Wametafakari nini wafanye ili kulinda maridhiano
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara Maalim Seif alisema ikiwa CCM wanaendelea kung’ang’ania na kutetea mfumo wa Muungano wa Serikali mbili ni jambo jema, lakini akasema  ni vyema kila upande wa Jamhuri ya Muungano ukapewa  mamlaka yake kamili ya dola.
Alisema ikiwa CCM na Serikali zake wanashabikia mfumo huo korofi wa Muungno wa Serikali mbili na kubeza Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, wajumbe wa Ukawa hawatarudi kushiriki Bunge hilo na kwamba yeye binafsi msimamo wake ni ule wa Ukawa na kamwe hatabadilika.
Mara kadhaa Mansoor na Jussa walipopigiwa simu zao za mikononi zilikuwa zikiita bila ya kupokewa, hivyo viongozi hao kushindwa kutoa ushirikiano ili kuelezea kwa undani mazungumzo kati ya  Rais na Makamu Mwenyekjiti mstaafu huyo wa CCM Zanzibar (Dk Karume).
Kumekuwa na mfululizo wa vikao vya siri tangu wajumbe wa Ukawa walipojiondoa bungeni ikiwa ni pamoja na ujio wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, kutembelea  Zanzibar, Aprili 21 mwaka huu  ambapo alikutana na Rais wa visiwa hivyo, Dk Ali Mohamed Shein, Mzee Moyo, Rais Mstaafu Dk Karume na Maalim Seif.

Wakati kukiwa na juhudi za kidiplomasia za upatanishi ili wajumbe wa Ukawa warejee bungeni, tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete amewataka wajumbe hao warudi na kushiriki katika chombo hicho halali cha kikatiba na ikiwa itashindikana baada ya siku 60 kumalizika, Katiba ya sasa ya mwaka 1977, itaendelea kuliongoza Taifa.

source; mwanachi

0 comments: