Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imefanya uamuzi mgumu wa
kuwatimua baadhi ya wapangaji wa nyumba zake zilizopo mjini Dodoma ambao
ni wadaiwa sugu, wakiwamo mawaziri saba na wabunge 15.
TBA katika kutekeleza uamuzi huo imekabidhi
Kampuni ya Yono Action Mart orodha ya majina ya watu hao wanaodaiwa
kiasi cha Sh800 milioni, ili waondolewe kwa nguvu kwenye nyumba hizo
wanazoishi.
Akizungumza na Mwananchi juzi Mkurugenzi Mtendaji
wa TBA, Elius Mwakalinga, alithibitisha kuwa ofisi yake inachukua hatua
hiyo kwa mujibu wa sheria kwa sababu wapangaji hao wamekwenda kinyume na
mikataba yao.
“ Hatukupenda kuchukua hatua hii, lakini ukweli ni
kwamba madeni hayo ni ya muda mrefu, kazi tunayofanya ni kwa manufaa ya
maendeleo ya nchi na siyo yetu binafsi, hivyo tulitegemea wangetimiza
wajibu wao wa kulipa lakini imekuwa kinyume,” alisema Mwakalinga.
Alisema fedha ambazo TBA inadai hadi sasa
zimefikia jumla ya Sh 800 milioni ambazo kama zingekuwa zimelipwa
zingewasaidia kutimiza wajibu wao wa kujenga baadhi ya nyumba mpya au
kukarabati zile zinazotakiwa kufanyiwa hivyo.
“Walipewa notisi na ofisi yetu kule Dodoma baadhi
yao waliitikia wito kwa kulipa madeni yao, wakiwamo hata maofisa wa
Ikulu, walitoa ushirikiano mzuri, nafikiri kwa kutambua wajibu tulio nao
TBA,” alisema.
Mwakalinga alisema kuwa TBA imeona iwahusishe
kampuni ya udalali ya Yono Action Mart kwa sababu wao wana majukumu
mengi ya ujenzi wa nyumba mpya za watumishi wa Serikali.
“ Gharama za kumlipa dalali huyo, watatakiwa
kulipa hao hao wanaodaiwa kwa mujibu wa sheria, sisi hatuna bajeti
hiyo,” alisema Mwakalinga ambaye alikataa kuwataja wadaiwa hao akieleza
kuwa jukumu hilo tayari lipo kwa Yono.
Mkurugenzi wa Yono Action Mart, Yono Kevela, kwa
upande wake alisema baada ya kupokea kazi hiyo, walitoa notisi ya siku
14 kwa wahusika ili kuwapa nafasi ya kulipa madeni yao.
“ Wale ambao wamelipa kutokana na ile notisi
wamejinusuru, lakini wale ambao hawajalipa kwa kweli nimetuma kikosi
kazi changu ambacho ninakiamini, kwamba hakina woga katika kutimiza
majukumu tuliyopewa, natarajia kesho wataanza kazi, hiyo,” alisema
Kevela. Baadhi ya mawaziri waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Waziri wa
Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda, anayedaiwa Sh7.5 milioni, ambaye
alipohojiwa na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu deni hilo alisema:
“Mimi sina habari hiyo nipo Nairobi, Kenya,”.
Mwingine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu anayedaiwa Sh 9.4 milioni, ambaye aliliambia gazeti hili kuwa
ana taarifa ya deni hilo, lakini kwa wadhifa wake hawajibiki binafsi.
“ Nakumbuka niliona barua, lakini kwa utaratibu
ninaoujua ni kwamba mawaziri wote hatujigharamii kwa hilo , bali
tunalipiwa na Serikali sasa nafikiri labda wizara ilijisahau,
nakuhakikishia binafsi siwajibiki,” alisema Nyalandu.
Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na mawaziri wengine wakiwamo
na naibu mawaziri ambao majina tunayo, zilikwama baada ya baadhi yao
kushindwa kupatikana ofisini na simu zao kuita bila majibu huku wengine
simu hazikupatikana.
Wabunge
Kwa upande wa wabunge ni mbunge wa Bariadi John
Cheyo(UDP) ambaye anadaiwa Sh 4.2 milioni, alipohojiwa kuhusu deni hilo
alishtuka na kueleza kuwa TBA wamfuate, badala ya kudai kupitia
magazeti.
“He! ndiyo unaniambia wewe, sina taarifa kama wana madai, waje tu siyo kudai kwenye magazeti.” alisema.
Mwingine ni mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo
Makani (CCM) anayedaiwa zaidi ya Sh2.5 milioni, alipoulizwa na
alijitetea kuwa hana taarifa, kwa kuwa alikuwa safarini Masasi Mkoani
Mtwara kwenye msiba.
“ Hapa ninapozungumza nawe nipo njiani naelekea
Dodoma, sina habari hiyo wewe ndiyo kwanza unaniambia, natoka kuzika,”
alisema Makani.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye
(CCM), ambaye kwenye orodha hiyo inaonyesha anadaiwa Sh2.4 milioni,
alisema kwamba hajawahi kuwa na mkataba na TBA.
“ Eeh! Labda wamekosea sijawahi kuwa na mkataba na TBA mimi,” alijibu Ole Medeye kisha akakata simu.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment