Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko 13 kwenye
Baraza la Mawaziri yaliyohusisha mawaziri nane, manaibu watano, wakiwamo
wapya wawili, ikiwa ni siku mbili kabla ya kuanza kwa Bunge, na ndani
ya saa 48 kama gazeti hili lilivyoripoti Ijumaa iliyopita.
Rais pia aliwaapisha mawaziri wote 13 akiwamo
waziri mpya wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ambaye
alisababisha hafla hiyo kuchelewa kwa kuwa alikuwa akitokea Davos,
Uswisi.
Mabadiliko hayo, yanayoweza kuwa ya mwisho kwa
Rais Kikwete, yamefanyika ikiwa imesalia miezi sita kabla ya kuvunjwa
kwa Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
Rais amelazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya
mawaziri wawili, Profesa Anna Tibaijuka na Profesa Sospeter Muhongo,
kuondoka kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye
akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo pia imesababisha Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi kusimamishwa kazi, huku waziri wa
zamani wa wizara hiyo, William Ngeleja akivuliwa uenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Sheria.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Kikwete amewaondoa
mawaziri wawili wazoefu kutoka Ofisi ya Rais, Steven wasira na Ofisi ya
Waziri Mkuu, William Lukuvi, kuwapangia wizara nyingine, huku
akimhamishia Dk Mary Nagu kwenye Ofisi ya Rais na Jenister Mhagama
(Waziri Mkuu).
Akitangaza mabadiliko hayo jana, Katibu Mkuu
Kiongozi Ombeni Sefue alisema mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene,
ambaye alikuwa naibu wa wizara ya Nishati na Madini kuanzia mwaka 2012
hadi 2014 na ambaye hadi jana alikuwa naibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, ameteuliwa kumrithi Profesa Muhongo kwenye
wizara hiyo tata ya Nishati na Madini.
Simbachawene anakuwa waziri wa nne kushika wizara
hiyo tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani na anaingia wakati
Steven Masele, aliyekuwa naibu Waziri wa Nishati na Madini, akiwa
amehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano). Nafasi ya Masele
imechukuliwa na mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ambaye
ameteuliwa kwa mara ya kwanza.
Sefue alisema mbunge wa Ismani, William Lukuvi,
ambaye tangu mwaka 2010 amekuwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Utaratibu na Bunge), ameteuliwa kuziba nafasi ya Profesa Tibaijuka ya
uwaziri wa Kazi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Sura nyingine ngeni kwenye baraza hilo, kwa mujibu
wa Sefue, ni ya mbunge wa Same, Anne Kilango Malecela, mmoja wa
wazungumzaji wakubwa bungeni, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Wizara ya Elimu.
Alisema aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Jenista Mhagama amepanda kuwa Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu
na Bunge, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Lukuvi.
Nagu amehamia Uhusiano na Uratibu (Uwekezaji na Uwezeshaji) na Dk Harrison Mwakyembe anayehamia Afrika Mashariki (Uchukuzi).
Wengine ni mwanasiasa mkongwe, Steven Wasira
aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo akitokea Ofisi ya Rais, Uhusiano na
Uratibu, wakati Samuel Sitta anakwenda Uchukuzi akitokea Wizara ya
Afrika Mashariki.
Manaibu waziri wengine waliohamishwa ni Angella Kairuki, ambaye
anakwenda Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitokea Katiba na
Sheria.
Ummy Mwalimu anakuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akitokea Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge, kutaka uteuzi wa Profesa
Muhongo na Profesa Tibaijuka kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Akaunti
ya Tegeta Escrow.
Bunge liliagiza mamlaka ya uteuzi kutengua
nyadhifa hizo pamoja na wenyeviti wa Kamati za Bunge, Nishati na Madini
iliyokuwa chini ya Victor Mwambalaswa.
Wengine waliotakiwa kuvuliwa nyadhifa za Kamati
kutokana na kashfa hiyo ni Andrew Chenge (Bajeti) na Kamati ya Sheria na
Katiba iliyokuwa chini ya William Ngeleja.
Akizungumzia uteuzi huo, Kilango alisema:
“Ninayajua matatizo ya walimu wenzangu na kwa kushirikiana na wenzangu
tutaweza kuyatatua, kikubwa ni kushirikiana.”
Alisema kuwa kwa kushirikiana na Waziri wa Wizara hiyo watakuja na mipango na mikakati itakayolenga kuboresha sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Lukuvi alisema kuwa anafahamu
changamoto zinazoikabili wizara hiyo na atashirikiana na wananchi ili
kuzitafutia ufumbuzi.
“Ninachoomba ni ushirikiano kutoka kwa wananchi
kwa kuwa ni imani yangu kuwa tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja kazi
itafanyika vizuri”alisema Lukuvi.
Naye Waziri wa Nishati na Madini George
Simbachawene alisema anatambua fika kuwa uchumi wa nchi yeyote
unategemea nishati hivyo atahakikisha sekta hiyo inawaletea manufaa
watanzania wote.
Simbachawene alisifu kazi ya Profesa Muhongo ana akasema atahakikisha anaikamilisha kwa kufikisha umeme kote vijijini.
Dk Slaa alonga
Akizungumzia mabadiliko hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa alisema: “Hakuna jipya katika hayo mabadiliko, kwani
tatizo lililopo ni mfumo na si viongozi, Watanzania wasitegemee lolote
kutoka kwao.
“Kitendo hiki cha watu wanafanya makosa halafu wanaachiwa wanajiuzulu na kubaki na sifa zao.
Kama taifa hatuwezi kusonga mbele. Tunahitaji kuwashughulikia wanaorudisha nyuma maendeleo ya nchi.”
Katibu huyo aliongeza kusema: “Wahalifu bado
wanapata fursa ya kukaa na kujadiliana na rais, hii haikubaliki.
Washabainika wamefanya makosa kwa nini wasiwajibishwe mapema?”
TBC yawa kero
Shirika la Habari Tanzania (TBC) jana liliwakera
Watanzania waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya
mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Mabadiliko hayo yalikuwa yakitangazwa na Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kutoka Ikulu jijini Dar es Salaam
ambapo yalihusisha mawaziri na manaibu mawaziri.
Matangazo hayo yalikuwa yakikatika mara kwa mara
na wakati mwingine yakionyesha picha bila sauti jambo lililokuwa kero
kwa watazamaji.
Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa TBC, Clement
Mshana alipotafutwa kuzungumzia matatizo yaliyojitokeza, alisema kwa
kifupi “mimi sijui na nipo mkoani ninaendelea kufuatilia matangazo ya
mabadiliko hayo” na kukata simu.
Katika hatua ya uapishwaji wa mawaziri na manaibu
mawaziri hao ulioanza Saa 12.14 jana jioni muda mfupi baada ya kumalizwa
kutangazwa matangazo yaliendelea vizuri.
Hali hiyo si ya kwanza kutokea kwani katika
mijadala kadhaa ya mikutano ya Bunge matangazo yamekuwa yakikatika jambo
lililokuwa likilalamikiwa na baadhi ya wabunge na wananchi kwa
kukoseshwa fursa ya kutazama muhimili huo wa ukiendelea na shughuli
zake.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment