“Natamani kuondoka eneo hili lenye mila na desturi nyingi potofu
zinazoninyima haki, sina amani hata kidogo na moyoni mwangu sioni nuru
ya maisha yangu”
“Kwa mfano tarehe 11.06.2014 alikuja mwanamume
mmoja nyumbani kwetu akampa mama kilo moja ya sukari na Sh500 kama
kishika uchumba ili anioe katika umri huu mdogo”.
Maneno haya ya kukata tamaa yanatoka kinywaji mwa
Roda Damas (jina halisi limefichwa), mwanafunzi wa Shule ya Msingi
Oldonyomurwa iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Roda mwenye umri wa miaka 15 ni miongoni mwa
watoto wa kabila la Wamasai ambaye anatakiwa kuolewa katika umri mdogo,
baada ya wazazi wake kupewa kishika uchumba na mwanamme anayenuia
kumuoa.
Hofu hii ya watoto wa jamii ya kifugaji ndiyo
inayonifanya nitembelee maeneo yao kuujua ukweli wa yanayozungumzwa na
nina bahatika kukutana na Roda anayezungumza nami huku akibubujikwa
machozi.
Wilaya ya Siha hususan Kata za Orkolili, Makiwaru,
Karansi, Gararagua na Biribiri, zina watoto wa kike wanaoishi kwa hofu
ya kuolewa katika umri mdogo. Wengine wanaanzia hata miaka mitano.
Ndoa za utotoni
Roda anasema kwa jamii ya kifugaji si jambo la
ajabu mtoto kuchumbiwa hata akiwa na umri wa miaka mitano, umri ambao
hata anayechumbiwa hajui nini kinaendelea.
“Mwanamume anaweza kuja na kutoa kishika uchumba
na mtoto ataendelea kuishi kwa wazazi wake na siku akimhitaji humchukua
baada ya kutoa ng’ombe waliohitajika kama mahari.
“Kila nikipita nikikutana na huyo baba huniita mke
wake na hata mama yangu huniambia huyo ndiye mume wako. Hii inaniumiza
kwa sababu mimi nataka kusoma sitaki kuolewa.”
Hawa nao wako mtegoni
Roda ananisaidia kukutana na watoto wengine
wawili, Neema na Evelyn wote wana miaka 14 na wana masaibu kama yake
kwani tayari wameonyeshwa wachumba na wanatakiwa kukeketwa ili waolewe.
“Muda mwingi tunautumia kufikiria ni jinsi gani tutajitoa kwenye mikono ya wanafamilia wanaotaka kutuozesha,” anasema Neema.
Ndoa za utotoni Tanzania
Tanzania ni moja ya nchi zilizokithiri kwa ndoa za
umri mdogo duniani. Kwa wastani, wasichana wawili kati ya watano
huolewa kabla ya kufikisha miaka 18 .
Kwa takwimu za mwaka 2010 kutoka mashirika
mbalimbali ya kijamii, asilimia 37 ya wanawake wenye umri wa miaka 20
hadi 24 waliolewa kabla ya kufikia miaka 18.
Mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga
asilimia 59, Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55 na takwimu hizo
zikionyesha Mkoa wa Kilimanjaro una tatizo hilo kwa asilimia 25.
Serikali inasemaje?
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na
Watoto, Pindi Chana amewahi kunukuliwa akisema mkoani Mara kuwa suala la
ndoa za utotoni na ukeketaji linatoa dosari kubwa katika harakati za
kumkomboa mtoto wa kike.
Anasema Taifa linahitaji mchango wa kila mwananchi
ili kufikia malengo ya mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini (Mkukuta) na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
Alisema ndoa za utotoni na ukeketaji vinapaswa
kupigwa vita kwa nguvu zote na kuwa jamii inaweza kuondoa tatizo hilo
kama italichukulia kwa uzito wa juu.
0 comments:
Post a Comment