Dodoma. Kisu kikali cha Kamati Kuu ya CCM (CC) leo kitaondoka na vichwa 33 kati ya 38 vya walioomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake.
Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika
kwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huku kikitawaliwa na usiri mkubwa,
kuhama ukumbi na kila dalili za kubadili ratiba iliyopangwa awali ili
kuvuruga mipango ya kambi za wagombea.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kulikuwa
na uwezekano wa kubadili ratiba ili vikao vya Kamati ya Maadili na CC
ama vifuatane au vifanyike usiku ili kuyanyima makundi nafasi ya
kujipanga.
Alipoulizwa jana kuhusu vikao hivyo, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alidai kuwa hata yeye hakuwa na
uhakika wa lini na muda gani hasa kikao cha Kamati ya Maadili
kingefanyika.
Awali, vifaa vya ukaguzi wa wajumbe vilikuwa
vimewekwa katika Makao Makuu ya CCM, White House lakini baadaye jioni
viliondolewa na hapakuwa na taarifa zozote zilizotolewa.
Habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kikao
hicho cha Maadili kilitarajiwa kufanyika Ikulu ya Dodoma kuanzia saa nne
usiku wa jana.
Haya yanajitokeza wakati macho na masikio ya
Watanzania yakiwa hapa Dodoma kusikiliza namna kazi ya kuchuja wagombea
itakavyofanyika na kujua ni watu gani 33 watakaoanza kulambwa na kisu
cha CC, hasa kwa majina makubwa yanayotazamwa na wengi, mara tu baada ya
kujadiliwa na Kamati ya Maadili.
Kazi za Kamati Kuu leo
Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni
kufikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC),
majina yasiyozidi matatu ya walioona kuwania urais wa Zanzibar ambayo
imeombwa na Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa
mapendekezo kwa NEC majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania urais
wa Muungano na kuandaa mkutano wa NEC.
Vigezo vya maadili
Kulingana na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo
la 2012 kifungu cha 4(ii), kuhusu taratibu za kuomba uongozi, wanachama
wanaogombea uongozi ambao uteuzi wao hufanywa na vikao vya kitaifa,
watachunguzwa kwanza uadilifu wao na chombo cha maadili cha CCM kwa
ushirikiano na vyanzo vingine.
Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba
uongozi katika ngazi yoyote, itikadi na mwenendo wake vitachunguzwa
kwanza na Kamati ya Usalama na Maadili inayohusika, ndipo maombi hayo
yaliyoambatanishwa na mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele
ya kikao chenye madaraka ya kutoa uamuzi.
Ikiwa mwanachama hakupendekezwa kwa sababu ya kukiuka Katiba ya
CCM, Kanuni za CCM na sheria ya nchi, hatakuwa na haki ya kukata rufaa
kwa mtu yeyote au kikao chochote. Lakini ikiwa mwanachama atakataliwa
kugombea kwa sababu ya madhambi yake katika chama, basi ni wajibu wa
Kamati ya Usalama na Maadili kumjulisha makosa yaliyomnyima haki ya
kugombea, naye anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa haki zake kikatiba.
Mtu yeyote anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya
Usalama na Maadili ya ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na
maadili au nidhamu ya chama atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma hizo
mbele ya wajumbe wa kamati hiyo ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa
maandishi, lakini hataambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa
kama imekwishajulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya
sheria au vyombo vya habari.
Kanuni ya maadili inaendelea kusema kuwa uchambuzi
wa tuhuma hizo utafanywa kwa kutumia njia mbalimbali pamoja na
mashahidi watakaopatikana.
Uchunguzi utakapokamilika na endapo itadhihirika
kwamba tuhuma zina uzito, mtuhumiwa ataitwa mbele ya kikao cha Kamati ya
Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika, kama ni lazima, ili apate
kuhojiwa ana kwa ana.
Pia, kanuni inasema Kamati ya Usalama na Maadili
ya ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu suala hilo kwenye
kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa nakala ya uamuzi kwa
maandishi.
Wagombea wanne kukosa CC
Katika kikao cha CC kinachofanyika leo, wajumbe
wanne ambao ni miongoni mwa majina 38 yatakayojadiliwa katika mchujo huo
watalazimika kukaa kando ili kukwepa mgongano wa masilahi.
Wajumbe hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri
wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Makamu wa Rais, Dk Mohamed
Ghalib Bilal na Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM
katika Vyombo vya Dola, Toleo la Pili – Februari, 2005, ukurasa wa 25,
kifungu cha 21 (3); wajumbe wa vikao vya uchujaji na uteuzi wa wagombea
kwa ngazi inayohusika hawaruhusiwi kuendelea na kazi ya uchujaji na
uteuzi iwapo wao ni wagombea katika ngazi hiyo.
Kanuni hiyo pia imetoa miiko ya shughuli za
uchujaji na uteuzi wa wagombea na wajumbe wote wanatakiwa na kanuni
kuzingatia maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza
shughuli za uteuzi.
Kanuni hizo zinasema ni mwiko kwa kiongozi yeyote
kwa maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi
mwombaji mmoja dhidi ya mwingine, kutumia au kuhusisha ukabila, dini,
rushwa, rangi, hila na eneo analoishi au anakotoka katika shughuli
yoyote ya uchaguzi.
Pia, ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji
yeyote wa nafasi ya uongozi au mwanachama yeyote aliyekabidhiwa dhamana
ya usimamizi au uangalizi au uratibu wa kura za maoni, uchujaji na
uteuzi, kufanya vitendo
Kuhusu misaada, kifungu cha tano (a) kinasema ni marufuku kwa
mgombea yeyote mtarajiwa au wakala wake, kufanya vitendo vyovyote
vinavyoonekana dhahiri kuwa ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi
anayoitafuta kabla ya muda rasmi wa uongozi unaohusika haujamalizika.
Kanuni imetoa adhabu kwa watakaovunja miiko hiyo
na kwa kiongozi atakayethibitika kuivunja atavuliwa uongozi na kwa
mwanachama anayeomba kugombea nafasi yoyote atakayethibitika kuivunja
hiyo hatateuliwa kugombea nafasi anayowania.
Chanzo: Mwananchi
vya ukiukwaji wa kanuni.Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment