LATEST POSTS

Wednesday, July 8, 2015

Wiki ngumu kwa CCM Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitafanya maamuzi yake kwa presha ya watangaza nia ya kutaka kuteuliwa kuwa wagombea wa CCM ili kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwani mfumo wake wa kumpata mgombea uko wazi na ni wa miaka yote.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema kumekuwa na taarifa nyingi za mtaani juu ya kumpata mgombea Urais wa chama hicho lakini wao kama chama hawafanyi kazi kwa shinikizo kwani kanuni zake ziko wazi za kuanza na wagombea watano baadaye watatu na mwisho mmoja.

Alisema kwa sasa hakuna mgombea wa kuondoka katika chama hicho baada ya jina lake kutoonekana katika wagombea watano baadaye watatu hadi mwisho kupata jina moja kwani wagombea wote 38 walichukua fomu waliapa kutohama ikiwa majina yao hayataonekana kwenye kinyang'anyiro hicho.

"Hatufanyi kazi kwa presha za nje bali tutafuata taratibu zote zinazotakiwa na kwa sasa hivi hata ikiwa mtu jina lake halitaonekana basi muda wa kukata rufaa hakuna, lakini sio kwamba tunawakataza wasikate rufaa lakini wanakata rufaa kwa nani, wakati wote ni wana-CCM na mimi simuoni mtu wa kuondoka CCM kwani hata huko nyuma hata mawaziri walikatwa lakini wote walikuwa pamoja na ninaamini hata mchakato huu kila mtu atatendewa haki na tutabaki wamoja," alisema Nnauye.

Alisema kila mgombea anajua wazi kuwa kuna kushinda na kushindwa na kuna kuteuliwa na kutokuteuliwa na asiyekubali kushindwa si mshindani.

Alisema jana ndio mchakato rasmi wa kumpata mgombea urais wa CCM umeanza ambapo Kikao cha kwanza kitakuwa ni Sekretarieti ya Maadili ya Chama hicho ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana huku ajenda kuu ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu wa chama hicho pamoja na mambo mengine ya ratiba, malazi ya wajumbe.

"Julai 8, 2015 kutakuwa na Kikao cha Usalama na Maadili ambacho kitaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo Julai 9, 2015 kutakuwa na uzinduzi wa ukumbi mpya wa CCM ulioko nje kidogo ya mji wa Dodoma kabla ya Rais Kikwete kwenda kuvunja Bunge na baadaye kitafanyika kikao cha Kamati Kuu ya CCM, "alisema Nnauye.

Nape alisema Julai 10,  Halmashauri Kuu ya Chama hicho itakutana kwa mambo makuu matatu ambayo ni kupitisha jina la mgombea urais Zanzibar lakini pia itapitia ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo iliandaliwa na Kamati iliyoongozwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira na ambayo itapelekwa kwenye Mkutano Mkuu.

Alisema Halmashauri Kuu itapokea majina matano ya wagombea na kisha kupigiwa kura ili kupata majina matatu. Aliongeza kuwa Julai 11, 2015 Mkutano Mkuu wa CCM utafanyika ili kupitisha ilani ya CCM  lakini pia kupiga kura ili kupata jina moja kutoka majina matatu  ambapo ndio litakuwa jina la mgombea Urais kupitia CCM.

Akizungumzia maandalizi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao wanakadiriwa kufikia zaidi ya wajumbe 3,000, alisema wamejipanga vizuri na wajumbe wote wasiwe na wasiwasi ya maandalizi yakiwemo malazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa alisema Mkoa huo kwa sasa unatarajiwa kuwa na wageni zaidi ya 3,000 ambao watakuwepo kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa CCM hivyo kwa sasa wao kama Mkoa wamejipanga vizuri kuhakikisha wageni wote wanafika na kuondoka salama.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Gallawa alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama utakuwepo wa kutosha hasa katika kipindi hiki ambacho kuna ongezeko la wageni.

"Nawatahadharisha wale wote wanaojipanga kwa namna moja ama nyingine kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani  tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi na yule ambaye asiyekuwa mjumbe wa mikutano na wala sio mwalikwa ni bora asiende kabisa Dodoma, "alisema Gallawa.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: