Nyumba ya Paul Sozigwa iliyopo Kurasini jijini Dar es Salaam
Nyumba ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Mwalimu Julius
Nyerere, Paul Sozigwa imeuzwa katika mazingira ya kutatanisha na mke
wake Monica Kuga baada ya mwanahabari huyo kupata maradhi ya kupoteza
kumbukumbu.
Kuga aliiuza nyumba hiyo kwa Mahamood Duale kwa
Sh600 milioni mwaka 2010, huku watoto wake wanne wa Sozigwa wakipinga
uuzwaji huo wakidai kuwa baba yao aliwakabidhi nyumba hiyo mwaka 1998.
Mtoto wa mwisho wa Sozigwa ambaye pia ametajwa
kama msimamizi wa mirathi, Moses alisema wana vielelezo vya wosia
aliowaachia baba yao akiwa Finland kabla ya tatizo lake la kupoteza
kumbukumbu halijawa kubwa.
“Tulirekodi kila kitu na ushahidi wa maandishi
upo, baba alisema nyumba ile ni ya watoto na siyo yake wala ya mke wake.
Lakini pia tulirekodi sauti yake, tunashangaa kwanini mama ameiuza,”
alisema Moses.
Kwa maelezo ya wanafamilia hao, Kuga aliachana na
Sozigwa mwaka 1974 na kufungua kesi ya kudai talaka mahakamani jambo
ambalo baba yao alilipinga.
“Alitaka kuachana na baba tena sisi tukiwa wadogo
ili wagawane mali, lakini baba hakukubali, tunashangaa iweje leo
arudiane naye halafu auze nyumba?” alihoji Moses.
Moses alieleza kuwa mama yao alimchukua Sozigwa na
kuishi naye kama kisingizio cha kujihalalishia uuzwaji wa nyumba hiyo
iliyopo maeneo ya Kurasini, karibu na shule ya Sekondari ya Jitegemee.
“Mama alimkana baba na wameachana kwa miaka zaidi
ya 34 na aliidai talaka hadi mahakamani kwa nguvu, halafu baba alipoanza
kuumwa anadai anataka kumlea kumbe ni ujanja wake tu, alitaka kuuza
eneo la familia,” alidai mtoto huyo.
Kwa mujibu wa wanafamilia hao, Kuga alighushi hati
ya nyumba hiyo na kuiuza kwa Duale lakini baadaye aliwataka wampe hati
halisi ili amkabidhi Duale.
Lakini baada ya kuona kuwa hawezi kuipata, kwa
kushirikiana na Duale walianza kumsumbua Moses na hatimaye walimfungulia
kesi mahakamani.
Hata hivyo, baada ya Duale kuzungumza na wakili wa
familia ya Sozigwa, aliambiwa ukweli kuwa hiyo nyumba ina utata wa
wanafamilia hali iliyomsababishia Duale mshtuko hadi kupooza.
“Huyu Duale alizungumza na wakili wetu, akaambiwa
ukweli kuwa asinunue hiyo nyumba kwa kuwa haina hati na alipoonyeshwa
hati halisi alishtuka na kupata kiharusi kwa sababu alikuwa ameshalipa
fedha zote,” alisema Moses.
Akiendelea kusimulia, Moses alisema mauzo ya nyumba hiyo yana
utata na kuna dalili ya rushwa kwani yameidhinishwa na baraza la ardhi
la Wilaya ya Temeke ambalo kwa kawaida, lina haki ya kuidhinisha mauzo
ya nyumba yenye thamani ya Sh50 milioni na chini ya hapo, wakati thamani
halisi ya nyumba hiyo ni Sh900 milioni.
“Tunashangazwa na kitendo cha mama kuuza nyumba
hiyo kwa Sh600 milioni wakati tathmini iliyofanywa mwaka 2010 ilionyesha
kuwa ina thamani ya Sh900 milioni,” alisema Moses.
Moses ambaye alizungumza kwa niaba ya ndugu zake
watatu, Salome, Irene na Ephata alisema licha ya mama yao kuuza nyumba
kwa mamilioni ya fedha lakini alikataa kusaidia kutoa fedha za kumpeleka
baba yao nchini Finland kwa matibabu. “Ilitubidi kutembeza bakuli hadi
kwa Rais Jakaya Kikwete ili tupate msaada wa matibabu ya mzee,” alisema.
Mwananchi lilizungumza na Kuga ambaye alisema
anawashangaa watoto wake kwa kushindwa kujua sheria zinavyofanya kazi na
kuanza kumrushia tuhuma zisizo na ukweli kuwa ameuza nyumba kwa ujanja.
“Hii kesi imeenda mahakamani hadi mahakama kuu na
nimeshinda mara tatu, lakini hawa wanaona kuwa wao ndiyo wana haki ya
nyumba ambayo mimi na baba yao tuliijenga, wanakata rufaa kila siku,”
alisema. Alieleza pia sababu za kuishi na Sozigwa licha ya kuwa
walitengana kwa zaidi ya miaka 34.
Alisema baada ya kuona hali ya mumewe huyo siyo ya
kuridhisha aliamua kurejea kumtunza na siyo kwa ajili ya nyumba.
“Nilimhurumia mzee nikaamua kuishi naye ili nimlee na ndiyo hapo
tulipokubaliana naye tuiuze nyumba,” alisema.
Kuga ambaye aliwahi kugombea ubunge wa Temeke kwa
tiketi ya DP mwaka 1995, alisema watoto wake hao walifikia hatua ya
kuficha hati halisi ya nyumba hiyo ili kuzuia uuzwaji.
Lakini hata hivyo, Kuga alisema yeye na wakili
wake walitoa matangazo kwenye magazeti kuwa hati hiyo imepotea ili
kupata kibali kutengeneza hati mpya ili waweze kuiuza nyumba hiyo.
“Hali ya baba yao ni mbaya lakini naona na hawa
watoto hali yao ni mbaya zaidi kwa sababu hawajui kitu wanachokifanya;
nyumba ni yetu mimi na mzee wao kinawauma nini? Alihoji.
Kadhalika Kuga alisema mpaka sasa Duale tayari ana hati na ameshakuwa mmiliki kamili wa nyumba hiyo.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment