Mwanamuziki kutoka kundi la weusi ,Nikki wa Pili
Mara nyingi tumezoea kuona wasanii
wakijishughulisha na kazi za sanaa pekee na ni wachache ambao wanafanya
kazi za sanaa na wakati huohuo wakajishughulisha na shughuli nyingine za
kitaalamu.
Wengi wa wasanii wa Tanzania
hawajaenda shule, huku baadhi yao wameishia elimu za sekondari. Hali hii
ni tofauti na msanii Nickson Simon au Niki wa pili ambaye yeye kwa
upande wake amesoma elimu ya juu na kuwa na shahada ya pili na sasa
anaendelea na masomo yake ya shahada ya tatu ya PhD katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM).
Tofauti na usanii
msanii huyu pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa nchini lakini pia ni
mtangazaji mshiriki katika kipindi cha Cloud 360.
Kwa
mujibu wa Niki wa Pili, aliingia katika uchambuzi wa masuala ya kisiasa
bila kutarajia baada ya kualikwa siku moja na kuonekana kwamba alifaa,
hivyo waandaaji waliomwomba ili awe mchambuzi ndani ya kipindi hicho cha
runinga.
Anasema kwa kuwa shahada zake amesomea
masuala ya maendeleo, imemuwia rahisi kwake kuchambua masuala ya kisiasa
ingawa yeye si mwanasisasa na hatarajii kuingia huko.
“Haukuwa
mpango wangu ni kitu ambacho kimetokea ghafla, sijawahi kujiona kama
mchambuzi lakini kumbe vile unavyotoa mawazo yako kuna mapokeo ambayo
wengi wanayapokea inakuwa tofauti,” anasema.
Hata
hivyo, Nikki wa Pili anasema anapenda vijana wenye uthubutu, hata
alivyosikia idadi kubwa ya wasanii wanajiunga katika siasa aliwaunga
mkono.
Anasema ni kitu kizuri kwani inaonyesha kwamba
vijana wapo tayari kwa mawazo mapya, lakini jambo la msingi ni lazima
watu wawe makini wachunguze na watambue au wafanye utafiti kujua
historia zao zikoje na je? Kilichowavutia ni kwenda kuitumikia jamii au
kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
“Nafikiri kwa
wabunge vijana wameonekana wakichapa kazi, ukiangalia mfano kina January
Makamba, David Kafulila, Zito Kabwe, Halima Mdee na hata John Mnyika
wamefanya vizuri, kwa hiyo unajua vijana wana mwamko wapo tayari kupokea
mambo mengi kufanya mabadiliko,” anasema Nikki na kuongeza kwamba ni
vizuri kuwa na rais kijana kwa sababu asilimia kubwa ya taifa ni vijana
hivyo kiongozi anatakiwa kufanana na wale anaowaongoza.
Mchango alioutua kuendeleza muziki
“Nimejaribu
kufanya kwa kiwango fulani katika ushawishi. Kwanza, nimeshiriki
harakati za kuishawishi Serikali itambue kikatiba umuhimu wa sekta ya
sanaa.”
Anasema pia kuwa ameshiriki mstari wa mbele
kama mfano kupinga unyonyaji unaofanywa kupitia milio ya simu na
alitangaza kujiondoa Kampuni ya Spice VAS Africa na Push Mobile mwaka
jana na baadhi wakafuata baada ya kuelimisha kuhusu unyonyaji huo.
Kwa
mujinu wa Niki wa Pili, wasanii wengi bado hawafahamu hata makadirio ya
faida au mapato yanayoingia kupitia milio ya nyimbo zao jambo ambalo ni
hatari sana kwani kampuni za simu zinachukua asilimia 60, mzalishaji
anachukua 31 na mpaka hatua ya mwisho msanii anapata asilimia mbili hadi
sita pekee.
“Harakati za kujiondoa huko zinaathiriwa
na mfumo, inahitaji safari ndefu ya ushiriki wa Serikali na uamuzi wa
wasanii wenyewe. Kwa hivyo, akimaliza PhD nitakuwa na nafasi nzuri zaidi
ya kuendeleza harakati hizo, ili siku moja tuone muziki wetu
unaondolewa mizizi ya unyonyaji.
“Anasema mbali na harakati hizo, amekuwa muelimishaji wa fursa za ajira kupitia semina iliyoandaliwa na Clouds Media Group.
Semina
hiyo iliitwa Fursa, pia ni balozi wa kupinga rushwa, mtetezi wa haki za
binadamu na mwanaharakati wa ulinzi wa mtoto dhidi ya unyanyasaji.
Harakati alizowahi kuzifanya
“Baada
ya kumaliza Shahada yangu ya Uzamili, nilipata nafasi ya kufanya kazi
katika shirika la kimataifa linalojihusisha na Ulinzi wa Mtoto Dhidi ya
Unyanyasaji na Utelekezwaji barani Afrika (African Networking for
Prevention and Protection Against Childrens).
Muziki
Niki wa Pili anasema ili muziki wa Tanzania usonge mbele na kuchuana na ule wa kimataifa unahitaji kufanyiwa utafiti wa kina.
Anasema
iwapo taasisi zilziowekwa kusimamia sanaa hapa nchini zitaifanyia kazi
mikakati hiyo, sekta hiyo itaingiza pato kubwa la taifa na kuongeza
ajira kwa vijana walio wengi.
Nikki anasmea licha ya
wasanii mbalimbali kujitangaza kimataifa, wanatumia nguvu kubwa sana
ambayo iwapo utafiti ungefanyika nguvu hizo ingekuwa ni ziada kwa kuvuka
mipaka zaidi.
“Hakuna utafiti, ukitaka kuongelea
muziki wa Tanzania ni ngumu kwa sababu hakuna takwimu, huwezi kujua
baadhi ya mambo yahusuyo sanaa kwa kuwa kuna vitu vya msingi vya kuweza
kufanyiwa kazi lakini vimeachwa tu,” anaanza kwa kusema Nikki.
Nyota
huyo anasema wasanii nchini wana malengo ya kuwa namba moja Afrika
ndiyo maana wanahangaika kwa fedha ndogo wanazozipata kupitia shoo za
kila siku.
Anasema hiyo ndiyo sababu ambayo hata kundi
la Weusi wameamua kusaidia, huku wasanii wengine wakiangalia namna ya
kutoka kwa kutafuta kolabo na wasanii wa kimataifa ili kuzifikia ndoto
zao kwani wanahitaji kufika mbali zaidi ili muziki upanuke, hivyo nguvu
za ziada kutoka kwa taasisi hiyo zikiongezwa lengo litafikiwa.
Hata
hivyo, Nikki anasema changamoto za mitandao kuzikabili ni mtihani,
lakini pia imefungua kitu kipya kwao ambapo sasa wanaweza kuuza muziki
wao online, “zamani ilichukua wiki moja muziki kufika vijijini lakini
kwa sasa ndani ya sekunde kadhaa unaweza kuwauzia mamilioni ya watu
muziki wako.
“Kinachotakiwa kufanya ni namna
tunavyotumia faida katika teknolojia hizi lakini pia vilevile kuangalia
namna ya kupunguza madhara ya teknolojia.”
Nikki
anasema ili kufikia katika viwango vinavyofaa kuna mambo ambayo
yanatakiwa kufanywa na taasisi zilizopewa dhamana ikiwamo kuangalia
namna soko linakoelekea wapi na namna ya kuweza kuingia huko, mfano soko
la muziki wa Afrika lakini ili uweze kuingia huko msanii anatakiwa awe
na video nzuri, nchi ina maprodyuza lakini bado hawana viwango.
“Mfano
Diamond au Weusi wakienda kutengeneza video Afrika Kusini wanalipa
mamilioni ya fedha, lakini bado hatupati kitu wala nchi haipati kitu
fedha ya ndani inatoka nje ya nchi, kuna kila sababu sasa Tanzania
isomeshe maprodyuza wakubwa wawasomeshe wakafikia viwango fulani ili na
sisi tupate watu wanaoweza kufanya kazi kubwa zaidi ili hata wasanii wa
nje nao pia watamani kufanya kazi na sisi wakaja kufuata ule ubora wa
video kwa hiyo nchi itaingiza kipato kikubwa,” anasema Nikki.
Licha
ya hayo aliyoyaongea, Nikki anasema Rais atakayepewa ridhaa na
Watanzania, anatakiwa kuzingatia kwamba robo ya Watanzania wamejiajiri
kupitia sekta ya sanaa.
“Rais ajaye nataka nimwambie
kwamba kuna zaidi ya wasanii milioni moja Tanzania, ambayo ni asilimia
kubwa ya nchi sanaa inaweza kuajiri watu wengi, ninapopiga muziki wangu
Dj anapata kipato, prodyuza na wengineo kwa hiyo kuna mzunguko mkubwa,
hivyo ana uwezo wa kuutumia muziki ili kutatua tatizo la ajira nchini.”
0 comments:
Post a Comment