Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli
amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo maamuzi mengine
yatakapotolewa.
Dk Magufuli ameagiza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi
zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za
nje.
Uamuzi huo wa rais ameutoa Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao
kilichojumuisha watendaji mbalimbali wa serikali wakiwemo Makatibu
wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu na Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ruhusa ya safari
nje ya nchi inaweza kutolewa kwa jambo la dharura ambalo hata hivyo
jambo hilo lazima lipate kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi.
“Badala yake rais ametaka ziara nyingi zielekezwe kwenda vijijini ili
kuwawezesha watendaji kujua na kutatua kero za wananchi” imesema
taarifa hiyo.
Katika kikao hicho, rais ameelekeza pia mambo kadhaa ambayo watendaji
hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili
yasimamiwe mara moja na Baraza la Mawaziri atakaloliteua.
Mambo hayo ni pamoja na kuanza kwa mikakati ya kuhakikisha wanafunzi
wote wanaanza kupatiwa elimu ya bure kuanzia Januari mwakani.
Taarifa hiyo imetaja jambo la pili kuwa ni suala la uratibu wa mikopo
ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo ameagiza lifanyiwe kazi na mipango
yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais amemuagiza Kamishna wa TRA kusimamia
kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kero ndogo
ndogo zinazowakabili wananchi zinaanza kushughulikiwa mara moja.
Ameitaka TRA kukusanya mapato toka kwa wafanya biashara wakubwa na
wakwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote na kusisitiza kuwa
hakuna mwenye mamlaka ya kubatilisha maamuzi hayo zaidi yake.
Chanzo: Global publishers
0 comments:
Post a Comment