LATEST POSTS

Monday, July 9, 2012

IMANI ZA KISHIRIKINA ZAHATARISHA MAISHA YA VIKONGWE - URAMBO

Suala la mauaji ya vikongwe kwa sababu ya imani za kishirikina limekuwa likipigiwa kelele na wanaharakati mbalimbali wanaopingana na vitendo hivyo nchini Tanzania. Wapo watu ambao wamekuwa wakiendekeza vitendo hivyo vya kikatili kwa wazee ambao hawana hatia kwa kuwatuhumu kuwa ni wachawi pasipokuwa hata na ushahidi. Hivi ni nani anaweza kusimama hadharani na kutoa uthibitisho wa kuonyesha kuwa bi mkubwa fulani ni mchawi. Suala kubwa la kujiuliza hapa ni wauaji hawa wanajuaje kuwa kikongwe fulani ni mchawi kama na wao si wachawi. Eeh! Kwa maana ili ujue fulani ni mchawi si ni lazima umshuhudie huyo mtu akiroga jamani. Na utamwonaje basi kama wewe si mchawi maana kwa macho ya kawaida huwezi kumwona mchawi. Kwanini jamii imekuwa ikijichukulia sheria mkononi na kufanya kazi ya kutoa hukumu kwa watu hawa ili hali wao si mahakimu au Mungu. Wao ni wasafi kiasi gani hadi wafikie kutoa hukumu kwa binadamu wenzao. Inatia uchungu jamani. Hali hii itaendelea hadi lini? Kwanini watu wameuweka ushirikina mbele na kusahau amri za Mungu. Tunaambiwa tusiue lakini watu wanajifanya hamnazo wanaendelea kuua wenzao bila hata ya huruma.
Jamani, msinishangae kwa sababu, nimejikuta nimepatwa na uchungu sana baada ya kupata taarifa kuwa, katika Kijiji cha Majengo Mapya kilichopo katika Wilaya ya Urambo nje kidogo ya Mji wa Urambo  kuna tukio la Wazee wawili mtu na mkewe kuchomewa nyumba yao alfajiri ya tarehe sita mwezi wa saba mwaka 2012 kwa sababu ya imani za kishirikina. Siyo siri, imani iliniingia na pamoja na kuwa nilikuwa nimechoka kwa mihangaiko ya kutwa nzima ya kujitafutia ridhiki, imani nilijikuta  nachukua usafiri na kuelekea katika Kijiji hicho ili kushuhudia tukio hilo kwa macho yangu. Sikutaka kuhadithiwa. Baada ya mwendo wa dakika kumi na tano hivi, nilifika kwenye makazi ya wazee hao na kumkuta bi mkubwa wa watu amejishika tama huku akiangalia upande wa nyumba yake uliokuwa umeungua.
"Pole bibi'. Ndio neno nililojikuta nikilisema mara baada ya kumwona bi mkubwa yule amejikunyata kwa masikitiko.
"Asante mama yangu, karibu". Alijisemea mama wa watu huku akinipa kiti kilichokuwa pembeni niketi. Nilikipokea na kuketi.
"Shikamoo bibi". Nilimsalimia.
"Marahaba mjukuu wangu, karibu".
"Asante sana.
Baada ya kusalimiana na bibi huyu, nilimtaka anieleze jinsi hali ilivyokua ndipo aliponieleza kuwa, walikuwa wamelala na shemeji yake. Yeye alikuwa amelala chumbani kwake na shemeji yake alikuwa amelala chumba cha pili. Mume wake hakuwepo nyumbani kwani anafanya kazi ya ulinzi hivyo alikuwa kazini kwake. Akiwa usingizini mida ya saa kumi alfajiri, ghafla alisikia sauti ya binti yake ikimwita kwa nje ikisema " Mama mnaungua, mama mnaungua huku akigonga dirisha la chumba chake kwa fujo. Ndipo alipokurupuka na kumwamsha shemejie kisha wakatoka nje.
"Nakwambia mjukuu wangu, kama sio juhudi za majirani zangu, saa hizi tungekua ulimwengu mwingine. Tungekua maiti". Alisema bibi wa watu kwa uchungu.
"Pole bibi jamani". Nilimliwaza. Lakini sikuishia hapo, niliendelea kumuuliza kama kuna mtu yeyote ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo ndipo aliponieleza kuwa, katika tukio hilo hakuna mtu aliyejeruhiwa isipokuwa wameunguza baadhi ya vitu  na kiasi cha pesa ambacho mumewe alikuwa ametunza ndani humo.
Naye mume wa mama huyu alisema kuwa, nyumba yetu ni ya nyasi, na kama ujuavyo kipindi hiki ni cha kiangazi hivyo upatikanaji wa nyasi kwa ajili ya kuezeka nyumba ni mgumu. Sijui tutafanyaje na hela hatuna. Kusema ukweli, wameturudisha nyuma sana. Na pia, tunaogopa kulala ndani humu kwani usalama wa maisha yetu ni mdogo.
Sikuishia hapo kwani niliendelea kudodosa zaidi ili kujua kama kuna watu wowote ambao wanawahisi kuhusika natukio hilo lakini walisema hakuna wanaemhisi na hadi sasa hakuna aliyekamatwa. Lakini kubwa zaidi na lililonishtua ni baada ya kuelezwa kuwa, tukio la kuchomwa kwa nyumba ya wazee hao sio la kwanza katika kijiji hicho. Inaelezwa kuwa, tukio hilo ni la nane kwa kipindi cha kuanzia mwezi june hadi tarehe 6 mwezi Julai 2012 na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo. Hata hivyo, wazee hao walisema kuwa, wamelipoti tukio hilo katika kituo cha polisi Urambo na wameahidi kuwa watalifanyia uchunguzi.
Ndugu zangu, hayo ndiyo yaliyojiri ndani ya Urambo. Je, nini maoni na ushauri wako juu ya jambo hili. Unafikiri nini kifanyike ili kukomesha vitendo hivi vya kikatili?


Pichani: Bi mkubwa aliyejitambulisha kwa jina la mama Bahati akiwa ameshika tamaa akiwaza kitendo alichofanyiwa na watu wasiojulikana kwa tuhuma za uchawi.



Pichani: Mama Bahati akionyesha fedha ambazo mumewe alikuwa amezitunza ndani zikiwa zimeungua moto. Hapo ndio umuhimu wa kuweka fedha benki unaonekana. Kwani kutokana na ajali hii, bi mkubwa huyu na mumewe wamejikuta wakibaki weupee pasipo hata na senti moja mfukoni.


Picha zinazofuatia chini, zinaonyesha namna nyumba ya wazee hawa ilivyobakia baada ya kuchomwa alfajiri na watu wasiojulikana.


 

 



Pichani: Mume wa mama Bahati akiitazama nyumba yao kwa masikitiko



Kwa ushauri, kutoa maoni yako kuhusiana na blog hii ili kuweza kuiboresha zaidi tuma kwenda theresiachacha@gmail .com. Aidha kama una habari au tukio lolote nitumie kupitia email hiyo. Ikiwa na picha, itapendeza zaidi.

KWA PAMOJA TUJENGE NCHI YETU.

KARIBUNI SANA.

 

0 comments: