Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania ( TFDA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Baraza la Famasi, imetoa mafunzo kwa watoa dawa watarajiwa katika maduka ya dawa muhimu Wilayani Urambo.
Mafunzo hayo yana lengo la kuboresha maduka ya dawa baridi kwa kuyapindisha hadhi kuwa maduka ya dawa muhimu mpango ujulikanao kwa jina la ADDO mpango ambao ulibuniwa na Serikali kupitia Wizara ya Ustawi na Jamii kwa kushirikiana na MSH.
Lengo kuu la mpango huu wa ADDO ni kupata ufumbuzi wa matatizo yaliyobainika katika tathmini iliyofanywa katika huduma ya dawa itolewayo na maduka ya dawa baridi nchini. Kimsingi matatizo yaliyojitokeza wakati wa tathmini ni wauzaji wa maduka kutokuwa na elimu ya dawa au tiba, kuuza dawa moto na zisizosajiriwa, kutoa huduma za tiba kama vile kuchoma sindano na kufunga vidonda kwenye maduka .
Msimamizi wa mafunzo hayo Bi Grace alisema kuwa, hayo yametolewa kwa muda wa wiki tano kuanzia tarehe 4.6.2012 hadi tarehe 6.7.2012 ambapo watoa dawa wapatao mia moja na nne (104) wamefundishwa masomo ya sheria, utoaji sahihi wa dawa pamoja na kujifunza elimu ya magonjwa ya yatokeayo mara kwa mara katika jamii. Aidha, washiriki walifundishwa utoaji huduma kwa magonjwa ya watoto kwa uwiano yaani (IMCI), stadi za mawasiliano na elimu ya UKIMWI na ushauri nasaha.
Wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi wakati wa sherehe za kufunga mafunzo hayo zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilayawahitimu wa mafunzo hayo waliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kubuni na kuanzisha mpango wa mafunzo hayo ya ADDO ili kuboresha huduma kwa wananchi wengi waishio Vijijini na kwenye Miji midogo. Aidha, waliishukuru Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania kwa kusimamia na kuendesha mafunzo hayo ya utoaji dawa katika Wilaya ya Urambo.
Risala iliendelea kusema kuwa, changamoto zilizopo hapa Wilayani ni idadi ya wamiliki waliohudhuria semina ya umiliki na mafunzo ya ujasiliamali ni kubwa kuliko idadi ya watoa dawa, hivyo, bado Wilaya haijakidhi mahitaji ya watoa dawa. Vilevile, muda wa mafunzo ulikuwa mfupi ukilinganisha na mada za mafunzo zilizotolewa na pia, mazingira ya kujifunzia watoa dawa hayakuwa rafiki kwa matumizi ya vifaa vya kisasa kulingana na karne ya Sayansi na Technolojia.
Wahitimu hao walipendekeza mafunzo hayo yawe endelevu na kwa kuwa watoa dawa nao ni watoa taarifa, ni vizuri nao wawe wanashirikishwa kwenye mafunzo mbalimbali yanayogusa utendaji kazi wa huduma za afya.
Akifunga mafunzo hayo mgeni Rasmi ambaye alikuwa ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bw. Florence Mwalle aliishukuru Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa na Baraza la Famasi kwa kutoa mafunzo hayo yenye nia ya kuboresha sekta ya Dawa ikiwa ni pamoja elimu endelevu kwa watoa dawa katika maduka ya dawa baridi yaliyopo sasa.
" Naamini mafunzo haya yamesaidia kupata watoa dawa wenye elimu bora ya utoaji sahihi wa dawa kiatu ambacho kitachangia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo ya huduma ya dawa Wilayani Urambo". Alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji.
Aidha aliwapongeza wahitimu kwa kuweza kufikia hatua muhimu kwa kuwa walizingatia yote waliyokuwa wakifundishwa pamoja na kuhudhuria bila kukosa madarasani, kuwa wasikivu, kufanya mazoezi na majaribio na ndio maana sasa wanaitwa wahitimu na si Washiriki.
Akieendelea kutoa hotuba yake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri aliwashukuru wawezeshaji wote kwa kukubali kuja kutoa mafunzo hayo Wilayani Urambo. Aliwataka waendelee na ujasiri huo wa kulitumikia Taifa.
Akimalizia hotuba Mgeni Rasmi aliwaeleza wahitimu wa mafunzo hayo kuwa, mambo yote waliyofundishwa ni ya msingi na yataimarisha utendaji kazi wao wa kila siku kwani dawa zikitumika kwa usahihi huleta matunda yaliyokusudiwa lakini pia, dawa ni sumu na huleta madhara ambayo hayakutarajiwa iwapo haitatumika kama ilivyokusudiwa. Hivyo aliwataka elimu waliyoipata waitumie katika kuleta mabadiliko katika utoaji wa huduma ya dawa Wilayani Urambokatika maduka yao ili matunda yaliyokusudiwa yapatikane na hatimaye baadaye maduka ya o ya dawa baridi yapandishwe hadhi na kuwa maduka ya dawa muhimu.
Wahitimu wa mafunzo ya utoaji dawa wakiwa katika sherehe za kufunga mafunzo hayo zilizofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.
Wahitimu wakionyesha mmoja ya mabango waliyokuwa nayo kwa mwandishi wa ladytheresa.blogspot
Wahitimu wakisherehekea kufungwa kwa mafunzo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya
Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo
aliyekuwa Mwenyekiti wa mafunzo Bw. Marisa Chapuchapu
Kushoto ni aliyekua msimamizi wa mafunzo Bi Grace toka Mbalali Mbeya
Mgeni rasmi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. Florence Mwalle akigawa vyeti kwa wahitimu
Muhitimu wa mafunzo mwenye umri mdogo kuliko wote na mmoja kati ya wahitimu waiofanya vizuri akitoka kupokea cheti kwa Mgeni rasmi.
0 comments:
Post a Comment