LATEST POSTS

Friday, December 14, 2012



 WAFUGAJI WATAKIWA KUFUGA KWA KUZINGATIA IDADI YA MIFUGO KWA ENEO ILI KUEPUKA UHARIBIFU WA MAZINGIRA - URAMBO NA KALIUA
Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mhe. Anna Magowa amesisitiza kuboreshwa kwa sekta ya mifugo kwani ni miongoni mwa sekta za kiuchumi katika Wilaya za Urambo na Kaliua na Tanzania kwa ujumla. Mhe.Anna Magowa aliyasema hayo kwenye kikao alichofanya kati yake na Wadau wa Mifugo kutoka katika Wilaya za Urambo na Kaliua kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
Katika hotuba yake, Mhe. Anna Magowa alisema kuwa, sekta ya mifugo ikiboreshwa, inaweza kumuongezea kipato mfugaji na Halmashauri pamoja na kuinua hali ya maisha kwa wananchi wanaotegemea mifugo katika maisha yao.
 
Mhe. Anna Magowa aliendelea kusema kuwa, ingawa mchango wa sekta hii ni mdogo katika pato la Taifa ukilinganisha na sekta nyingine za kiuchumi, bado sekta hii ni muhimu kwani imeokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingezitumia kwa kuagiza mifugo na mazao yake kama vile nyama, maziwa, mayai na ngozi na bidhaa zinazotokana ngozi.
Mifugo ni muhimu kwa sababu mifugo na mazao yake yanachangia usalama wa chakula kwa kaya za wafugaji, mifugo inatupatia nyama, mayai, maziwa na ngozi. Vilevile, kutokana na mifugo, tunapata ngozi ambazo hutumika kutengenezea viatu na bidhaa zingine zinazotokana na ngozi na pia, mifugo huongeza nguvu kazi kwani matumizi ya wanyamakazi husaidia katika kilimo na usafirishaji wa mazao toka mashambani na kupeleka sokoni.
Mhe. Anna Magowa alisema kuwa, asilimia arobaini kati ya Kaya 62,333 zilizopo katika Wilaya za Urambo na Kaliua ni Wakulima na Wafugaji lakini mifugo bado haijachangia kuinua maisha ya mfugaji.
Aidha, Mhe. Anna Magowa aliyataja matatizo yanayochangia uzalishaji mdogo katika sekta ya mifugo kuwa ni vifo vinavyotokana na magonjwa ya mifugo hasa yale yanayoletwa na kupe, ukosefu wa Wataalamu wa ugani ngazi ya Vijiji umesababisha uboreshaji wa mifugo na mazao yake kuwa duni na pia, koostaafu zaidi ya asilimia 95 ya mifugo katika Wilaya za Urambo na Kaliua ni ile ya asili ambapo ukuaji huchukua muda mrefu.
 
                                                 
Pichani: Kutoka Kushoto Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mhe. Saveli M.Maketta, Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mhe. Anna Magowa, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Eng. Richard Ruyango na wa mwisho ni Daktari wa Mifugo Wilaya ya Urambo Dk. Lyebu Bo
Mbali na matatizo hayo, zipo changamoto mbalimbali zinazosababisha uzalishaji mdogo wa sekta ya mifugo katika Wilaya ya Urambo na Kaliua. Changamoto hizi ni  miundombinu duni ya mifugo mfano machinjio, makaro ya kuchinjia, minada, hakuna mabirika ya kunywea maji mifugo, vibanio vya kutoa huduma ya mifugo, majosho, vituo vya huduma kwa mifugo, njia za kupitishia mifugo na mabanda ya kukaushia ngozi.
Changamoto zingine ni elimu duni katika kaya za wafugaji hali inayopelekea upokeaji wa tekinolojia za ufugaji bora kuwa mgumu, uwekezaji mdogo katika sekta ya mifugo na wafugaji kutokukopesheka hali ambayo inasababisha uanzishwaji wa mashamba ya mifugo kuwa mgumu, mifugo duni na mfumo wa ufugaji bado ni wa huria na kuhamahama ambao huchangia uharibifu wa mazingira na umilikishaji wa ardhi kwa ajili ya maji na malisho bado ni mgumu hivyo kupelekea upatikanaji wa maji na malisho kuwa shida hasa wakati wa kiangazi hali inayosababisha migogoro ya wakulima na wafugaji na wafugaji kuvamia mapori tengefu na kuharibu vyanzo vya maji.
 
                                                      
Pichani: Wadau wa Mifugo Wilayani Urambo wakifuatilia mada mbalimbalimbali zilizotolewa na wataalamu kuhusiana na Sekta ya Mifugo katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
"Wilaya ya Urambo na Kaliua zina zina fursa nyingi za uwekezaji katika mifugo kwa sababu kuna mifugo ya kutosha, ng'ombe 182,963, Mbuzi 130,123, Kondoo 20,000, Kuku 337,390, Bata 1426, Nguruwe 4300, Punda 523, Mbwa 10,350 na Paka 5646. Aidha, Wilaya ina malisho jumla ya Ha.261,625 ambazo kati ya hizi Ha.47,000 zimetengwa na zipo katika mpango wa matumizi bora ya ardhi. Vilevile, kuna fursa ya soko la ndani kwa mifugo na mazao yake - mifugo ya Urambo na Kaliua ina soko nje ya Mkoa, mtawanyiko mzuri wa hali ya mvua (mm900 hadi mm 1200) ambazo zinasaidia upatikanaji wa maji na malisho kwa miezi 7-8 katika mwaka na uwepo wa Wataalamu ngazi ya Wilaya na baadhi ya Kata".Alisema Mhe. Anna Magowa.
Ili Sekta hii iwe endelevu, Wizara ya Maendeleoz ya Mifugo na Uvuvi imetengeneza sera ya Taifa ya Mifugo (2006) ambayo imetamka DIRA ya maendeleo ya mifugo kwamba, ifikapo mwaka 2025, Sekta ya Mifugo kwa sehemu kubwa iwe inaendeshwa kibiashara, iwe ya kisasa, inayozalisha kwa tija, endelevu, kuongeza usalama wa chakula kuongeza kipato ngazi ya Kaya na Taifa na inayozingatia hifadhi ya Mazingira.
Lengo kuu la sera hii ni kuwa na sekta ya mifugo inayokua kutoka (5.9% - 9 ) ifikapo mwaka 2025, yenye ushindani ili kuchangia maendeleo na kuinua hali ya maisha kwa Wananchi ambao shughuli yao kubwa ni ufugaji. Aidha, lengo mahususi ni sekta ya mifugo izalishe kwa tija ili iweze kuchangia usalama wa chakula katika kaya, kuongeza thamani kwa mazao yanayotokana na mifugo ili kuongeza kipato na kuboresha lishe kwa Wananchi, kuongeza uzalishaji na ubora wa mifugo na mazao yake ili kupata malighafi kwa viwanda na viwanda vidogo hapa nchini, kuboresha ufugaji unaozingatia idadi ya mifugo kwa eneo ili kupunguza uharibifu wa mazingira, kuimarisha huduma za ugani na kusambaza teknolojia mpya za uzalishaji wa mifugo na mazao yake, kumuendeleza mfugaji kutoka katika dhana ya mchungaji na kuwa mfugaji, kuendeleza uzalishaji salama wa mazao ya mifugo ili kulinda afya za walaji, kuendeleza matumizi ya wanyamakazi ili kujikwamua na matumizi ya jembe la mkonona kuendeleza matumizi ya nishati inayotokana na kinyesi cha mifugo (biogas) ili kupunguza ukataji holela wa miti.
Akibainisha mikakati iliyopo ya kuendeleza Mifugo katika Wilaya ya Urambo na Kaliua, Afisa Mifugo Wilaya ya Urambo Bw. Abeid Mluge alisema kuwa, Wilaya imeweka mkakati wa kuweka bayana majukumu ya kila mdau, kubaini na kutangaza maeneo tengefu ya uwekezaji wa mifugo, kuhamasisha wafugaji kuchagua na kushughulikia mnyororo wa thamani kwa zao moja au mawili Wilayani kote, na ili kuboresha miundombinu yote muhimu kwa ajili ya maendeleo ya mifugo.
Bw. Mluge aliendelea kusema kuwa, mikakati mingine ni kufufua na kujenga vituo vipya vya maendeleo ya mifugo ngazi ya Kata, kuhamasisha jamii kutumia mazao ya mifugo, kuajiri wataalamu wa Ugani na kuanzisha mashamba darasa ya mifugo, kuimarisha huduma ya uhamilishaji na kuimarisha viwanda na Masoko ya mifugo.
Akifunga kikao Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mhe. Saveli M.Maketta aliwataka wafugaji wazingatie sheria ili kuepuka kuchunga mifugo yao kwenye maeneo ya Wakulima, Wadau watatue migogoro yao kwa amani,  Watendaji wa Kata wasimamie sheria na waache kuwafanya wafugaji kama mradi, elimu itolewe kwa Wafugaji na wafugaji watumie mifugo yao kusomeshea watoto wao.
 

Imeandikwa na:
 
Theresia C. Chacha
Urambo

0 comments: