LATEST POSTS

Friday, July 25, 2014

Sababu 10 zinazotia moyo dawa mpya ya Ukimwi

 
Dk Kamel Khalili (katikati)  wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple nchini Marekani akiwa ameshika  zawadi aliyokabidhiwa kutokana na umahiri wake katika utafiti wa VVU.

Wiki hii imekuwa na habari njema na ya faraja kwa dunia katika kupambana na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Wengi wanaweza kujiuliza mbona mambo ya ugunduzi wenye kutia matumaini yamewahi kutangazwa siku za nyuma, lakini yakaangukia pua? Kwa nini hata huu wa sasa usifuate mkondo huo?
Haya ni mambo ya kisayansi ambayo yanaaminika kila hatua inayopigwa inamsogeza mtafiti kwenye kupata jawabu hata kama hakufaulu.
Wanachofanya wanasayansi ni kutumia udhaifu uliojitokeza katika tafiti moja kuwa ni faida ya kumfanya afanye vizuri katika nyingine atakayofanya.
Utafiti uliotangazwa wiki hii umeonekana kutegua kitendawili ambacho kilionekana kuwatatiza wanasayansi wengi.
Huu ni utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple nchini Marekani kilichopo katika mji wa Philadelphia.
Wao wamegundua tiba ya kuangamiza VVU ambayo wanaielezea kuwa ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na tafiti nyingine zilizowahi kufanyika duniani.
Dawa hii inaweza kutumika kama tiba kwa wale ambao wanaishi na VVU pamoja na kuwa kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili anasema wao wamegundua namna ya kuweza kukiondoa kirusi cha Ukimwi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua.
Anasema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuiathiri seli ya mwili wa binadamu iliyoingiliwa na kirusi.
Dk Khalili anasema kuwa ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia nyingine ambazo tayari zimegunduliwa zimekuwa haziwezi kupenya ndani ya seli ya binadamu bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake; ndani ya mfumo wa damu. “Dawa zilizopo haziwezi kukiathiri kirusi cha Ukimwi kilichopo ndani ya seli, bali kile ambacho kimezalishwa na kuingia kwenye mfumo wa damu tayari kwenda kushambulia seli (CD4) nyingine,” anasema Dk Khalili.
“Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo ARV (dawa ya kufubaza VVU).”
Kwa namna ARV zinavyofanya kazi, huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kushindwa kuvikabili vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4 hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi muathirika akiacha kutumia dawa.
Kutokana na maelezo ya Dk Khalili, dawa hiyo ina sifa 10 muhimu ambazo zinadhihirisha kuwa ni ya matumaini.
Sifa hizo ni dawa kuweza kugundua seli iliyoingiliwa na kirusi, kutoboa seli kwa usalama na kuvuta nje ya seli kirusi kwa kuking’oa kwenye DNA.
Dawa hiyo huiacha DNA; sehemu iliyong’olewa ikijitengeneza huku seli nayo ikijitengeneza palipobomoka. Kirusi kufa baada ya kutoka nje ya seli, seli iliyoondolewa kirusi hubaki salama na kuendelea na kazi ya kinga kama kawaida.
Sababu nyingine ni dawa kuweza kufanya kazi pamoja na ARV na vilevile ugunduzi huu umeweza kutegua kitendawili kilichowatatiza wanasayansi wengi cha kuweza kushambulia kirusi ndani ya seli bila kuiathiri.
Mpaka sasa dawa nyingi zilizogunduliwa zinapambana na virusi walioko nje ya CD4. Jambo jingine muhimu ni dawa hiyo mpya kuweza kufanya kazi vizuri kwenye damu ya binadamu bila dalili za kuathiri seli nyingine.
Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani anaelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU. “Kama imepatikana teknolojia ya kuweza kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili limeonekana kuwa gumu kwa muda mrefu,” anasema Majani.
Anasema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo limekuwa gumu.
“Maana inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo ki tiba halikubaliki,” alisema Majani.
“Kikubwa katika ugunduzi huo ni kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa; ikiwepo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani anasema changamoto ambayo inaweza kujitokeza ni ya majaribio ya usalama wa dawa wakati wa matumizi.
“Lazima ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na utendaji wa mwili kwa jumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi zinashindwa… Tusubiri tuone labda hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” anasema Majani.
Uwezo wa dawa
Dk Khalili anasema wameitengeneza kwa protini maalumu ambayo inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta nje.
Baada ya kukivuta nje kirusi, huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga ya mwilini kama kawaida.
VVU kwa kawaida wanashambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama koloni la kuzalishia virusi wengine.
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kiumakini na bila kuathiri seli,” anajigamba Dk Khalili.
Anasema tayari dawa yao imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama. Katika maabara, anasema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Anasema anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache lakini anaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu.
Dk Khalili alisema wanachofanya kwa sasa ni kuangalia mfumo bora ambao utatumika katika kutibu binadamu.
Mkutano wa Ukimwi 2014
Ugunduzi huo umekuja wakati ambapo wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli ambazo hazina matumaini ya asilimia 100 ya kupatikana tiba au chanjo, ukilinganisha na mkutano wa mwaka uliopita.
Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za tafiti za VVU waliweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio.

Tafiti nyingi zikiwa ni za chanjo pamoja na tiba zimeshindwa kupata suluhisho la kudumu kwa sababu dawa zake zinapotumika vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya.
“Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili visiathirike kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” anasema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty nchini Australia, Professor Sharon Lewin.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa mkutano huo wa Ukimwi 2014, Profesa Françoise Barré-Sinoussi anasema ARV imewezesha kubadili kasi ya VVU na kinachoonekana sasa ni kiwango cha maambukizi kinapungua kadri miaka inavyoenda.
Profesa Barré-Sinoussi anasema: “Hatuna budi kusema programu hii ya kukabili imefanya mambo makubwa katika kukabiliana na janga hili na kubadili mwelekeo.”
Anasema takwimu zinaonyesha kuwa karibu waathirika 14 milioni ambao ni wa kipato cha chini na cha wastani, wanatumia ARV, hali ambayo imesaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa VVU.
Pamoja na hali hiyo, Profesa Barré-Sinoussi anasema kazi iliyopo mbele kwa sasa ni kupata tiba na chanjo na kwamba anaamini mafanikio yatapatikana.
Hali ya Ukimwi duniani
Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty nchini Australia, Professor Sharon Lewin anasema tafiti za sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 34 duniani wanaishi na VVU. Anasema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambapo bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Profesa Lewin anasema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, wanasayansi wamepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU.
Anasema anaamini juhudi za kisayansi zitawezesha dunia ifikie mahali ithubutu kusema “HIV havina nafasi katika mwili wa binadamu.”
Kwa sababu hiyo, anaamini ipo siku mafaniko yatapatikana kwa kupata chanjo na tiba.
Ukimwi ulianza kuisumbua dunia miaka 30 iliyopita ambapo miaka ya 1980 ulisababisha vifo vya mamilioni ya watu huku kukiwa hakuna aina yoyote ya tiba.
Mwishoni mwa miaka ya 90 zilianza kutumika ARV ambazo zimesaidia waathirika wengi wasifikia hatua ya kuugua Ukimwi.
Awali waathirika waliofikia hatua ya kuugua Ukimwi walionyesha kuishiwa nguvu, kudhoofika kiafya, nywele kunyonyoka, kupata vidonda sehemu mbalimbali za mwili na kuharisha.
Kauli ya wanasayansi kwenye mkutano huo ni kwamba “mwathirika wa VVU ametoka hatua ya kuhesabu ni ugonjwa unaomhukumu kufa hadi kufikia kwenye faraja ya kudhibiti virusi ili aendelee kuishi.”
VVU inaaminika ni kirusi aliyetoka katika jamii ya nyani akajibadili kitabia akaweza kumtumia binadamu kama sehemu ya kumuwezesha aishi na kuzaliana.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: