LATEST POSTS

Saturday, July 26, 2014

Serikali yaifunga Hospitali ya IMTU

 
Lango kuu la Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU). Picha na Maktaba
 
Dar es Salaam. Serikali imeifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), baada ya kuifanyia ukaguzi na kubaini kasoro kadhaa za uendeshaji wake.
Ukaguzi huo ulifanywa jana na jopo la wataalamu kutoka Manispaa ya Kinondoni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya IMTU kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hospitali hiyo imefungiwa wakati Kamati ya Watu 15, iliyoundwa na Serikali ikiendelea kuchunguza kashfa hiyo.
Hata hivyo, wakati taarifa za kufungiwa zikitolewa habari za ndani zinaonyesha kuwa hapakuwa na mgonjwa yeyote hospitalini hapo, ikielezwa kuwa wagonjwa wote waliondoka baada ya kuibuka kwa kashfa ya viungo IMTU ikihusishwa.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Bunini Kamba alisema kuwa wameamua kuifungia hospitali hiyo kwa muda usiojulikana, baada ya kukuta upungufu mbalimbali katika maeneo ya kutolea huduma, jambo linalohatarisha usalama wa wagonjwa.
“Maabara tumekuta dawa ambazo muda wake wa kutumika umepita na hazikuwa katika mpangilio maalumu. Wodini hakuna usimamizi maalumu, hasa kwa wagonjwa wenye majeraha,” alisema Dk Bunini.
Aliongeza: “Hakuna wauguzi wa kutosha na mashine ya kuchoma taka ngumu haifanyi kazi vilivyo. Tumeona kuwa hospitali hii haistahili kuendelea kutoa huduma kwa jamii.”
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Yasin Mgonda alisema: “Tumesikia uamuzi huo uliotolewa baada ya kufanyika ukaguzi. Tutajirekebisha na tutakapokamilisha tutawaita kuja kutukagua tena.”
Alisema kuwa pamoja na sababu nyingine, hospitali yake imefungiwa baada ya kubainika kuwa bomba la maabara limeharibika na halitoi maji.
Nyingine ni kutojaza vitabu vya wagonjwa kwa mujibu wa taratibu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pia duka lake la dawa kuwa halijasajiliwa lakini akasema sababu hiyo imewashangaza kwani wanachojua wao duka hilo limesajiliwa.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia aliliambia gazeti hili kwamba anaipongeza Serikali kwa uamuzi huo akisema utanusuru maisha ya wananchi waliokuwa wakipata huduma hospitalini hapo. 
“Tunaipongeza Serikali, ila tunaiomba iwatafutie wanafunzi wa chuo hicho maeneo mengine ya kujifunzia,” alisema Dk Saidia.
Juzi, Dk Saidia alisema kuwa wote waliohusika na kashfa ya utupaji mabaki ya viungo vya binadamu wanastahili kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kitendo hicho kimekiuka sheria, taratibu, haki za binadamu, maadili ya ufundishaji na taaluma ya udaktari.
“Kama ni taasisi ya utafiti imepoteza sifa ya kufanya utafiti na kama ni ya mafunzo basi imepoteza sifa ya kutoa mafunzo ya tiba. Kama ni hospitali itakuwa imepoteza sifa za kutoa tiba kwa binadamu,” alisema Dk Saidia.
Naye spika wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (IMTUSO), William Mapunga alisema kuwa kufungiwa kwa hospitali hiyo kutawaathiri, kwani watakosa sehemu ya kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo, akiiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwa mapana.

0 comments: