LATEST POSTS

Saturday, March 9, 2013

SHEREHE ZA WANAWAKE ZAFANA URAMBO

Machi nane ya kila mwaka ni Siku ya Wanawake Duniani ambayo husherehekewa ulimwenguni kote. Katika kuazimisha siku hii muhimu, Wanawake wa Urambo nao waliungana na Wanawake wenzao ulimwenguni kote kusherehekea siku hii muhimu.
Kwa mwaka huu, sherehe hii Kiwilaya ilifanyika katika Kata ya Nsenda iliyopo katika Tarafa ya Urambo. Kaulimbiu ya maazimisho ya siku ya Wanawake kwa mwaka huu ni "UELEWA WA MASUALA YA KIJINSIA KATIKA JAMII ONGEZA KASI".
Mwitikio wa Wananchi ulikuwa ni mkubwa sana kwani Wanawake wengi walijitokeza katika uwanja wa shule ya Msingi Nsenda ambapo ndipo sherehe hii ilifanyika.
Wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mhe.Saveli Maketta Wanawake walisema, matukio ya unyanyasaji wa kijinsia bado yapo ambapo kesi za Wanaume kutelekeza familia zao na kuoa wanawake wengine bado zipo nyingi. Aidha, tatizo la Wanaume kutokuwahusisha wanawake katika masuala ya kiuchumi bado yanaendelea.
Akitoa hotuba yake katika maazimisho hayo mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mhe. Saveli M.Maketta alisema, masuala ya kijinsia katika jamii yameanza kueleweka ila kinachohitajika ni kuongeza kazi zaidi ya uelewa wa masuala ya kijinsia katika kuleta maendeleo katika jamii.
Aidha, alisisitiza utaratibu wa kuwapa nafasi wanawake katika maamuzi nao uoneze kasi ili kuondoa mfumo dume katika jamii yetu. Aliwataka Wanawake wajitokeze kuwania nafasi mbalimbali katika ngazi ya Serikali ya Kijiji, Kata, Wilaya na Kitaifa wasisubiri nafasi za kupewa.
"Umefika wakati sasa wa Wanaume kubadili mwelekeo na mtazamo wao kwa kuwashirikisha Wanawake katika maamuzi ya mipango ya maendeleo ili kuleta maendeleo chanya katika jamii". Alisema Mheshimiwa Maketta.
Mheshimiwa Maketta aliendelea kusema kuwa, Wanaume wamekuwa chanzo cha ongezeko la idadi ya Watoto wa mitaani kutokana na tabia ya kuoa Wanawake wengi. Aliwataka waache tabia hiyo na badala yake wasomeshe watoto wao ili kuwajengea mazingira mazuri ya maisha kwani mtoto bila elimu, maisha yake yatakuwa ni magumu.
Kwa upande wa umilikishwaji wa ardhi, Mheshimiwa Maketta alisema, kwa sheria ya sasa, Mwanamke anaruhusiwa kumiliki ardhi ya wazazi au ya mume wake. Na kwa mwanamke yeyote atakedhulumiwa haki yake hii ya msingi, afikishe suala hilo kwenye vyombo vya sheria ili kupata msaada wa kisheria.
Akihitimisha hotuba yake, aliwataka Wanawake wapendane wenyewe kwa wenyewe ili kujenga umoja kwa maslahi ya Wanawake na Jamii nzima kwa ujumla.


Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Urambo (Mwenye suti ya kijivu) na Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Nsenda Mhe. Kadada wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakijiri katika sherehe hizo.
 
                                   



Waheshimiwa Madiwani wa Viti maalum Urambo pamoja na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo wakifuatilia maazimisho hayo.



Wannchi waliojitokeza wakifuatilia maazimisho ya Siku ya Wanawake duniani katika uwanja wa Shule ya Msingi Nsenda






Akina mama wakisherehekea siku kuu ya Wanawake katika uwanja wa Shule ya Msingi Nsenda

Wananchi wakijikinga mvua kwa viti baada ya mvua kuanza kunyesha ghafla. Lakini baada ya mvua kukatika, mambo yaliendelea kama kawaida. Hakuna kilichoharibika.

Imeandikwa na Theresia Chacha

0 comments: