LATEST POSTS

Tuesday, November 12, 2013

WAZIRI KENYA ASIFIA HOTUBA YA KIKWETE

Wizara ya Mambo ya Nje nchini Kenya, imesema bila Tanzania, hakuna Jumuiya ya Afrika Mashariki na bila Afrika Mashariki hakuna Tanzania.
Waziri wa Wizara hiyo, Amina Mohamed, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, jambo lililomsukuma kufika Tanzania ni kuunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa bungeni mjini Dodoma, Novemba 7 mwaka huu.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema Tanzania haiwezi kujitoa katika jumuiya hiyo au kuwa chanzo cha kuvunjika kwake.
Mohamed alisema amefikisha salama za nchi yake kwa Tanzania kutokana na hatua yake ya kutokuwa tayari kujitoa kwenye jumuiya hiyo kama ilivyodhaniwa awali.
"Tanzania na Kenya zimejiunga na jumuiya hii kwa muda mrefu na zina mafanikio mengi hivyo haziwezi kutengana hata kidogo," alisema Mohamed.
Aliongeza kuwa, Kenya inaamini nchi hizo zitaendelea kuijenga Afrika Mashariki kwa nguvu zote. "Nimetumwa na Rais Uhuru Kenyatta kuja kutoa ujumbe huu ambao ni wakati mwafaka wa kuimarisha zaidi uhusiano.
"Tulikuwa na wasiwasi wa Tanzania kujitoa katika jumuiya kutokana na hali iliyojitokeza kwa baadhi ya nchi kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha pamoja na Burundi.
" H a k u n a a n a y e w e z a kuitenganisha Tanzania na Kenya kwani zimejenga uhusiano wa karibu kijamii na kiuchumi," alisema Mohamed.
Aliiomba Tanzania kuisaidia Kenya ili kusukuma ombi lao la kutaka kesi inayomkabili Rais Kenyatta ihairishwe kwa mwaka mmoja ili kumpa fursa ya kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, alisema Serikali yake imefurahi kuona Kenya ni nchi ya kwanza kutoa pongezi zake ili kuinusuru jumuia hiyo.
"Hili ni jambo la busara linalopaswa kupongezwa , Tanzania itaendelea kushirikiana na Kenya katika masuala mbalimbali likiwemo la kutaka kesi inayomkabili Rais Kenyatta katika Mahakama ya ICC, iahirishwe mwaka mmoja," alisema.
 
SOURCE: MAJIRA

0 comments: