LATEST POSTS

Monday, December 23, 2013

SLAA AMLIPUA MAKAMU MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA URAMBO

 
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Dk.Willbroad Slaa akiwahutubia wananchi wa mji wa Tabora,katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui jana,akiwa ni mfululizo wa Ziara yake ya kujenga chama katika mikoa ya Kigoma,Tabora na Singida.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbrod Slaa, amemshukia Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Elias Kafyenda, kutokana na tabia ya kutumia magari ya serikali kwenye shughuli zake binafsi kwa lengo la kujijenga kisiasa.
Amesema atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.

Dk. Slaa alilazimika kulizungumzia suala hilo baada ya kupewa taarifa kuwa Mwenyekiti huyo anatumia magari ya serikali kubeba wanachama wa CCM kijijini kwake kuwapeleka kwenye msiba na shughuli mbalimbali za kichama.

Taarifa ambazo zilipatikana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, Makamu Mwenyekiti huyo aliamua kuwabeba wananchi kwa magari ya halmashauri ili kuhujumu mkutano wa Chadema usiweze kufanikiwa.

“Diwani anabeba watu kwenda kwenye msiba kijiji jirani kila kunapokuwa na mkutano wa Chadema, kwanini habebi wananchi kunapotokea misiba ya walalahoi hafanyi hivyo?”alihoji.

Dk. Slaa alisema waraka wa serikali unakataza kutumika kwa magari ya serikali kwenye shughuli binafsi na kwamba CCM imekumbatia yote hayo bila kuchukua hatua kwa viongozi wanaokiuka utaratibu wa serikali.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Shaban Mambo, alisema Makamu Mwenyekiti huyo ni dhaifu ndiyo maana anakimbiza watu wasiweze kushiriki mkutano wa Chadema.

Naye Afisa wa Chadema anayeshughulikia Sera na Utafiti, Waitara Mwita, alisema diwani huyo ni mzigo ndani ya halmashauri hiyo, hivyo wananchi wasikubali kumchagua kiongozi kama huyo kwa mara nyingine.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kafyenda, akizungumza na NIPASHE kwa simu alipoulizwa alisema madai hayo hayana msingi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: