LATEST POSTS

Monday, December 23, 2013

MADIWANI BADO WAMG'ANG'ANIA MEYA TABORA

SAKATA la madiwani halmashauri ya manispaa Tabora kutaka kumg`oa mstahiki meya wa manispaa hiyo Ghulam Hussein dewji Remtullah limechukua sura mpya baada ya madiwani hao kumuandikia barua mkurugenzi kuitisha kikao cha baraza cha dharura. Madiwani hao wameandika barua hiyo mwezi disemba 10 mwaka huu yenye kichwa cha habari kisemacho ‘ombi la kuitishwa mkutano maalumu wa halmashauri kwa madhumuni ya kumuondoa madaraka mstahiki meya Ghulam Hussein Dewji Remtullah kwa kutokuwa na imani naye’. 
 
Kwa mujibu wa barua hiyo yenye orodha ya madiwani waliojiorodhesha majina na sahihi zao kutaka kumuondoa meya wao,imesema kutokana na kanuni za kudumu za halmashauri ya manispaa Tabora, kanuni namba 80 kifungu a,c na d wako sahihi kufanya hilo. “Sisi madiwani tupatao 28….tukiwa na akili zetu timamu na bila kushawishiwa na mtu yoyote tumeweka sahihi zetu hapo nyuma kutaka kumuondoa mstahiki meya kwa kushindwa kazi na kutokuwa na imani naye.”ilisema sehemu ya barua hiyo. Aidha barua hiyo ya madiwani hao inaeleza zaidi kuwa lengo la kuomba mkutano maalumu wa madiwani ni meya huyo kutumia nafasi yake vibaya,kushindwa kazi na mwenendo mbaya wa kutosimamia na kuheshimu maazimio ya mikutano. 
 
 Barua hiyo ilifafanua kuwa chini ya uongozi wa mstahiki meya huyo ameshindwa kusimamia mapato na matumizi kwa kutofikia malengo katika kujiendesha kiasi cha kuwepo ubadhirifu mkubwa na kupelekea kupata hati chafu mwaka wa fedha wa 2011/212. Aidha tuhuma nyingine ni mstahiki meya na kamati yake ya fedha,utawala na uongozi kutembelea miradi ya maendeleo na kushindwa kutoa taarifa ya ukaguzi kwenye vikao vya halmashauri toka amekabidhiwa kiti hicho. 
Meya huyo anatuhumiwa kufumbia macho ubadhirifu wa jengo la OPD kata ya Itetemia lililojengwa kwa sh milioni 100 badala ya sh milioni 40 kama alivyoelezwa mkuu wa mkoa wa Tabora Fatma Mwassa na kuwepo ubadhirifu wa ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari ya kata ya Ndevelwa. 
 
 Tuhuma nyingine ni safari ya Marekeani ya mstahiki meya akiongozana na mtalaam Deo Msilu mwezi april 2011 ikiwa ni ziara ya urafiki wa Millenium City ambapo safari hiyo iligharimu sh milioni 17 fedha ambazo walitakiwa kupata kibali cha halmashuri alkini hawakufanya hivyo. Aidha barua hiyo imeanisha aliyekuwa mkurugenzi wakati huo Fanuel Senge naye alisafiri kwenda nchini Ethiopia na alitumia fedha za halmashauri bila kufuata utaratibu lakini fedha hizo alirejesha na hii inamlazimu mstahiki meya naye arejeshe fedha hizo lakini amekaidi. 
 
 Katika tuhuma nyingine madiwani hao waliorodhesha jinsi meya huyo alivyojilimbikizia viwanja na kuvitaja ni Plot namba 100 area G 4070 mtrs PB chenye jina Marial Hilal, Plot namba area 158 G 6980 mtrs Ghulamhussein Remtullah, Plot namba 99 area F 3331 mtrs Dewji Ghulamhussein. Barua hiyo ilitaja viwanja vingine kuwa ni Plot namba 206 area C 2252 mtrs Gulan F Gulan,Plot namba 637 Block D 3.11 Heka 8.5 Gulam H Remtullah na hali hiyo inapelekea kuwa meya huyo amekiuka maadili ya uongozi na kutumia cheo chake kujilimbikizia mali. Aidha madiwani hao walisema tuhuma nyingine ni mstahiki meya kutumia nafasi yake kuwagwa madiwani na kutengeneza chuki kiasi cha wengine kujiuzulu nafasi zao za ujumbe wa kamati ndogo. Gazeti hili lilimtafuta mstahiki meya wa manispaa Tabora Ghulamhussein Remtullah kujibu tuhuma hizo lakini alikana na kudai ni chuki za watu, huku mkurugenzi wa manispaa huyo Alfred Luanda naye alikiri kupokea barua hiyo ya madiwani hao. 
 

0 comments: