Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Alitoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mjini Nzega katika Jimbo la Nzega wilayani hapa ikiwa ni mfululizo wa ziara zake ya siku 20 katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Singida.
Dk. Slaa ambaye hata hivyo, hakufafanua ushabiki unaofanywa katika suala hilo, alisema Zitto alivuliwa nyadhifa za Naibu Katibu Mkuu na Naibu Mkuu wa Kambi ya upinzani Bungeni kwa misingi ya maadili kama katiba ya Chadema inavyoelekeza.
Alisema kuweka ushabiki kwa masuala ya maadili haitamsaidia Zitto bali ni kumharibia zaidi kwa kuwa chama kinaweza kuchukua hatua zaidi dhidi yake kwa kumfukuza kabisa.
Alisema msimamo wa Chadema unajulikana kutoka mwaka 2010 kwamba kabla ya kuiingia Ikulu hatua ya kwanza ni kusafisha ubovu wa maadili katika nchi hii.
“Ubovu wa maadili tusipousafisha ndani ya Chadema hatutausafisha hata tukiingia Ikulu, kama tutashindwa kusimamia maadili ndani ya Chadema basi na Ikulu tusiende sababu hatutastahili kwenda Ikulu,” alisema.
Dk. Slaa alimtaka Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kigoma, Shaban Mambo, kusaidia kumshauri Zitto ili kumsaidia vinginevyo ushabiki ukiingia itakuwa ni kummaliza.
Alisema Kamati Kuu ya Chadema ilimpa siku 14 Zitto na wenzake kujieleza kutokana na tuhuma zinazowakabili ambazo zimekwisha na ameshajibu.
“Naomba nitoe tahadhari msipoangalia mtamfanya afukuzwe kweli, kama mnaomshauri hamuwezi kumshauri vizuri ikifika mahali mimi kama Katibu Mkuu ninapoona mambo yanaendelea ni lazima nitoe ufafanuzi,” alisema.
Alisema amepata taarifa kuwa baadhi ya wenyeviti wa mikoa na wilaya wameanza kupelekewa barua na fomu wazisaini ambazo wanadai zimetoka ofisi ya Katibu Mkuu wakati siyo kweli na kutaka watu wasisaini vitu wasivyovijua.
“Hizo fomu zikishasambazwa wanasema zimetoka makao makuu kwa Katibu Mkuu, msidanyanywe sijatoa fomu, sijaagiza chochote, chochote mnacholetewa kama hicho kataeni kwa sababu katiba ya chama na kanuni inaelekeza taratibu za vikao.
Tukifika mahali baadaye na haya yakiendelee mimi nisilaumiwe, nitalazimika kuyajibu,” alisema.
Kauli hiyo ya Dk. Slaa imekuja siku mbili baada ya Zitto kupokelewa kwa maandamano na wananchi wa jimbo lake juzi akitokea Bungeni mjini Dodoma.
Zitto katika maandamano hayo aliwaeleza wanachama na wakazi wa Kijiji cha Mwandiga kuwa wawe wavumilivu ili aweze kupambana hadi haki ipatikane.
“Wananchi msisikitike kwamba mtoto wenu anaonewa kwa sababu mtoto wenu ni mpambanaji.
Mimi nimevumilia sana mishale ninayorushiwa mimi kama mwanasiasa mdogo kabisa ni mingi mno, kinachoniuma mimi wananchi wangu ni kwamba mishale hii narushiwa na wenzangu wa ndani ya chama, hicho ndicho kinachoniuma, lakini kinachonitia moyo ni nyinyi wanananchi wangu,” alisema.
Alisema kila akifikiria kukata tamaa anawaza watu wa Kigoma. “Nasema watu wa Kigoma watasikitika sana acha nipambane na nitapambana, muhimu ni sharti haki kutendeka na nitahakikisha haki inatendeka.”
Aidha alisema wao walishiriki kujenga chama na wameumia kwa ajili ya chama na watakuwa wa mwisho kutoka.
Zitto alisema ni lazima waende kwa utaratibu ule ule kwa sababu wao wameweka misingi ya hicho chama na kwamba wakikimbia watakuwa wanawachia watu ambao wamekuja badaye kuja kula matunda ya kazi ambayo wameifanya.
Alisema kuvuliwa nyadhifa zake za chama siyo sahihi wala usaliti ni kwa sababu ya kutaka kugombea uenyekiti wa chama hicho Taifa na kutaka matumizi bora ya chama.
Alisema wanachama wa vyama vya siasa wanapojenga uoga kwa viongozi wao ni udikiteta, lakini viongozi wanapojenga uoga kwa wanachama hiyo ndiyo demokrasia.
Novemba 22, mwaka huu Kamati Kuu ya Chadema iliwavua uongozi Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kwa madai ya kukisaliti chama kwa kuanaa waraka ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa unawakashfu viongozi wakuu wa chama hicho.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment