LATEST POSTS

Friday, January 10, 2014

Abiria wa treni wakwama Dodoma

Wasafiri wa treni wakwama Dodoma

ZAIDI ya abiria 1,600 waliokuwa wakisafiri kwa treni kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam na kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma wameandamana hadi ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, wakipinga kusitishwa kwa safari zao.

Katika maandamano yao, abiria hao walipinga  uamuzi wa uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) kuahirisha safari yao hadi saa 11 jioni kutokana na kuharibika kwa reli eneo la Gulwe na Godegode wilayani Mpwapwa.

Abiria hao walioanza safari Januari 2, mwaka huu walifika stesheni ya Dodoma jana asubuhi lakini walishindwa kuendelea na safari kutokana na kuharibika kwa kipande hicho cha reli kilichosombwa na mafuriko.

Akizungumza kwenye kikao cha dharura kilichoitishwa na Dk. Rehema, mmoja wa abiria hao, Alphonce Evarist, alisema tangu walipoanza safari imekuwa na matatizo kwa kuwa wamekaa njiani siku nane.

Alisema wakiwa Kigoma waliambiwa hawawezi kusafiri kwa kuwa reli imezolewa na mafuriko Dodoma na baada ya kufika mjini hapa bado waliambiwa hawawezi kusafiri kwa kuwa reli imeharibika.

“Tuna watoto na mizigo ya kuharibika njiani, tumeuza kila kitu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wasife njaa, lakini tena tumefika hapa tunaambiwa hakuna safari, kwa kweli mnatukatisha tamaa na huu usafiri,” alisema Evarist.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo aliwasihi abiria hao kuwa wavumilivu kwa kuwa ni kweli eneo la Gulwe na Godegode reli imeharibika.

Aliuagiza uongozi wa TRL kuhakikisha abiria wote wanapata huduma zote bila malipo ikiwemo chakula hadi watakapoanza safari.

Kwa upande wake Mhandisi wa Mitambo kutoka TRL Mkoa wa Dodoma, John Mandalu, aliahidi kuwa abiria wote watapata chakula na huduma nyingine hadi safari yao itakapoanza.
 
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: