Vurugu za aina yake zimezuka katika Mahakama Kuu jijini Dar es
Salaam, baada ya watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wa Chadema kumzomea
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe.
Vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa chama hicho
wanaomuunga mkono Zitto na wale wanaompinga, ambao walikuwa wamebeba
mabango ya kumsifia na wengine wakiwa wamebeba ya kumkashifu.
Katika vurugu hizo, baadhi ya wanachama hao
waliamua kufanya doria isiyo rasmi ndani ya mahakama hiyo ya kuwasaka
watu waliodai kuwa ni mamluki, huku wakimkamata askari kanzu, kabla ya
kumpiga ngumi na kumchania shati mtu mmoja wakidai kuwa alikuwa
akiwarekodi kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana asubuhi
ambapo kundi la wanachama hao, huku baadhi wakiwa wamevaa nguo za kaki
zinazotumiwa na chama hicho kufika katika mahakama hiyo kwa lengo la
kusikiliza kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Zitto.
Mara baada ya kuwasili kwa Mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini, huku akiwa ameongozana watu kadhaa wakiwamo wanasheria wake
na mabaunsa, wanachama hao walianza kumzomea huku baadhi wakimwita
fisadi.
Hali hiyo iliibua zogo katika eneo la mahakama
hiyo, hali iliyowalazimu maofisa kadhaa wa polisi kuingilia kati kwa
kuamua kumchukua Zitto na kumhifadhi kwenye chumba maalumu na kumtoa saa
6 mchana kesi yake ilipoanza kusikilizwa. Baadhi ya mabango ya
kumkashifu yalisomeka; Zitto tulimpenda, CCM imempenda zaidi, Zitto
rudisha fedha za CCM.
Yale yaliyomsifia yalisomeka; Zitto kama Mandela
na Zitto ni Mkombozi.Baada ya kumalizika kusikilizwa kwa kesi hiyo, saa
12 jioni wanachama hao walianza kurushiana ngumi, hasa baada ya
kuibuliwa kwa mabango yaliyosomeka ‘Zitto kwanza Chadema baadaye’.
Awali hali hiyo ilimfanya Zitto kutaharuki, huku mabaunsa wake wakijihami na kuanza kumlinda.
Baada ya Zitto kuhifadhiwa baadhi ya wanachama hao
ambao waliingia kwa kuandikishwa majina yao getini, walianza kuwasaka
watu waliowahisi kuwa mamluki, ambapo walimnasa askari kanzu na kuanza
kumzonga wakimuhoji anapeleleza nini katika eneo hilo.
“Hapa tunataka kujua wewe ni nani na unataka nini
hapa, maana hatukuelewi kabisa kwa nini unakuja kusikiliza mazungumzo
yetu, jitambulishe,” alisisika mmoja wa wanachama hao akimhoji askari
huyo huku akiwa amemkandamiza ukutani,
“Tunajua wewe ni askari kwa nini hujavaa sare leo? Kisha unajichanganya kwenye kundi letu.”
Kesi hiyo ilimalizika saa 12 jioni ambapo Zitto
alitolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi kwa kupitia mlango wa nyuma wa
mahakama hiyo na kuwaacha wafuasi hao wakionyeshana ubabe kwa mabango
na kauli za kejeli.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment