Baada ya uchunguzi wetu wa kina tumebaini kuwa habari hiyo ilipotosha ukweli na kutoa hisia potofu kwamba Waziri
Tibaijuka alibadili msimamo wake juu ya kuondoa
eneo la hekta 1,870 kutoka kwa eneo la mwekezaji na kurekebisha hati,
baada ya kuandamana na mwekezaji kwenye gari.
Tumejiridhisha pasipo shaka kuwa wananchi wa
Kapunga walimsikiliza Waziri kwa makini, pamoja na kuwa kulikuwa na
minong’ono ya hapa na pale katika baadhi ya wakati.
Kutokana na vyanzo mbalimbali, tumefahamishwa
kwamba awali, katika kikao cha ndani na viongozi wa Kijiji, Waziri
Tibaijuka aliwafafanulia msimamo wa Serikali wa kurejesha eneo lao
lililomilikishwa kimakosa kwa Nafco mwaka 1995 kabla ya shamba hilo
kuuzwa kwa mwekezaji mwaka 2006.
Waziri alisisitiza kwamba eneo litarejeshwa bila masharti, maana ni haki yao na pia ni suala la uhakika wa chakula kwao.
Waziri alikwenda Kapunga kukagua eneo hilo pamoja
na kushughulikia kwa upana wake mgogoro uliokuwapo kati ya wananchi wa
Kapunga na mwekezaji na ziara yake ililenga kutoa maelekezo kwa
wataalamu wa Wizara jinsi ambavyo ramani ya shamba hilo itarekebishwa
kulingana na jiografia ya kijiji, shamba na matumizi yake.
Baadaye waziri alifuatana na viongozi wa wilaya,
kijiji na waandishi wa habari kumtembelea mwekezaji na kufanya kikao cha
wazi, ambako pia alimweleza mwekezaji kwamba eneo la hekta 1,870
litapunguzwa kutoka kwenye eneo la shamba na kurejeshwa kwa wananchi
bila masharti yoyote.
Alimshauri mwekezaji kwa hiari yake arejeshe hati
ili irekebishwe na wizara la sivyo atamwandikia Rais akipendekeza hati
yote ifutwe na eneo kupimwa upya.
“Baada ya kauli hiyo, ndipo mwekezaji akasema,
tena kwa utani, ngoja kwanza nikutembeze uone eneo halafu nitakujibu
kwenye gari.” Kwa utani huo, watu waliangua kicheko, kwa hivyo
inawezekana wengine walitafsiri kuwa kitendo cha waziri kupanda gari la
mwekezaji pamoja na Mkuu wa Wilaya, Gulam Hussein Kifu, kungewafanya
washawishiwe isivyo halali ili kubadili msimamo zaidi wa kupata picha
halisi ya mgogoro kati ya mwekezaji kwa upande mmoja na wanakijiji kwa
upande mwingine. Pamoja na hayo yote, Waziri aliendelea kushikilia
msimamo wa kutatua mgogoro kwa manufaa ya pande zote mbili.
Tunakiri habari hiyo ilikuwa na upungufu na
ilileta taswira na hisia potofu kwa wasomaji wetu. Tunamwomba radhi
Waziri Tibaijuka na wananchi wa Kapunga kutokana na taarifa hizo.
Kauli ya Mhariri juu ya Usahihi na Haki.
Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd inaongozwa na sera
madhubuti ya uhariri, ambayo inaelekeza mambo mengi juu ya kutoa haki
kwa pande zote na makundi mbalimbali katika jamii. Kwa mfano,
inasisitizwa kwamba lengo la msingi la mwandishi wa habari ni kuripoti
kwa haki, usahihi na bila upendeleo masuala yote yanayohusu umma na
kwamba pande zote mbili za habari zinatakiwa kupewa nafasi sawa.
Kila wakati inapogundulika kuwa habari
iliyochapishwa si sahihi, inapotosha au imepotoshwa, ni lazima
isahihishwe na ni muhimu kupata maoni kutoka kwa mtu yeyote aliyetajwa
katika mazingira yasiyofaa. Masahihisho ni lazima yalenge katika
kusahihisha habari na wala siyo kurudia kosa ila tu pale uhakika
unapohitajika.
Ni kwa msingi huo sisi wa Mwananchi tumeamua
kuchukua hatua stahiki baada ya kujiridhisha kwamba taarifa ina
upungufu. Itambulike wazi kuwa hili lilikuwa kosa la kitaaluma na kamwe
si sera ya Mwananchi kulenga mtu, taasisi au kupotosha taarifa yoyote
kwa makusudi. Uungwana ni kukubali tatizo na kulitatua.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment