LATEST POSTS

Monday, January 13, 2014

Mvua yaleta maafa, yaezua nyumba 83 Meatu

Meatu. Kaya 83 zimeezuliwa kutokana na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali, huku  takriban ekari 15 za mazao mbalimbali zikiharibiwa.

Pia, mtu mmoja amesombwa na maji kwenye  mto wilayani Meatu, mkoani Simiyu.
Tukio hilo lilitokea Januari 8  saa 1:00 jioni kijiji na Kata ya Mwandoya, wilayani Meatu, hali iliyosababisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti kutembelea waathirika.
Akisoma taarifa ya awali iliyoandaliwa na Kitengo cha Maafa cha Wilaya, Naibu Katibu Tawala Wilaya ya Meatu, Mossa Lutani alisema baada ya kupata taarifa ya maafa hayo timu ya wataalamu ilitumwa kufanya tathmini. Lutani alisema timu hiyo ilishirikiana na uongozi wa kata, vijiji na viongoji vyote vilivyokumbwa na maafa kuzungukia maeneo yaliyoathiriwa kubaini jinsi waathirika wanavyoweza kusaidiwa. 
Alisema vitongoji vya kijiji vilivyokumbwa na maafa ni sita, kati ya vinane navyo ni  Madukani, Mabondeni, Itugutu,  Manasubi, Kanisani na Kisimani na kwamba, waathirika wakubwa ni kaya tano  ambazo nyumba zimebomolewa na kuezuliwa paa kabisa.
Lutani alisema Tabu Mazingo ameripotiwa kufa maji akijaribu kuvuka mto kutoka Kijiji cha Mwandoya kwenda  Mwandaya, huku wengine watatu wakijeruhi wa kwa kuangukiwa na kuta.
Akizungumza na waathirika,  Mabiti alisema Serikali inafanya jitihada kuhakikisha huduma zote za jamii kama miundombinu ya barabara zinatengenezwa na visima vilivyoharibiwa kusafishwa vizuri ili kupata maji salama.
Pia, Mabiti aliwataka wananchi kupanda miti ya kutosha, kwani  Meatu haina miti ya kutosha.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: