Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe anapanga kumchukulia hatua za kisheria Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe kutokana na kile alichodai kuwa ni kuzusha tuhuma zenye
lengo la kumchafua yeye binafsi na chama hicho.
Tuhuma hizo ni zile zilizowekwa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii na kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari
kuanzia Januari 6 mwaka huu, zikimnukuu Zitto akieleza kuwa Mbowe
amewahi kuhongwa mamilioni ya fedha na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM),
Nimrod Mkono.
Tuhuma dhidi ya Mbowe ziliibuka baada ya
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu Zitto kuwa amehongwa
magari mawili na Mkono.
Hata hivyo, Mkono katika taarifa yake alikanusha
madai ya Zitto kuhusu kuwapa fedha Chadema, pia alitoa ufafanuzi kwamba
hakuwahi kumhonga mbunge huyo magari kama ilivyodaiwa na Lissu bali
alimuuzia gari moja na kumkodisha gari la pili.
Taarifa ya kusudio la Mbowe kumburuza Zitto
mahakamani ilitolewa jana na Ofisa Mwandamizi wa Habari wa Chadema,
Tumaini Makene, huku ikikanusha tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya Mbowe.
“Mbowe ameshawasiliana na mawakili walifanyie kazi
suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria. Mwenyekiti wa chama
hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo
yaliyosemwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo hata hivyo
haikumtaja Zitto moja kwa moja.
Jana gazeti hili lilimtafuta Zitto ili aweze kuzungumzia suala hilo lakini hakupatikana.
Msingi wa taarifa
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tuhuma hizo
zinasambazwa na watu wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa
yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama hicho.
Kauli hiyo ni dhahiri inamlenga Zitto, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe
wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, kwani walivuliwa nyadhifa zao kutokana
na kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, uliolenga kufanya
mapinduzi ya uongozi ndani ya Chadema.
Taarifa hiyo imesema tuhuma zinazoshughulikiwa ni
zile zinazodai kwamba Mbowe alichukua Sh40 milioni mwaka 2005 kutoka
kwa Mkono ili asifanye kampeni katika Jimbo la Musoma Vijijini.
Tuhuma nyingine ni kuwa 2008 Mkono alimpatia Mbowe
Sh20 milioni kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime, kwamba
Mbowe alizitoa fedha hizo kwenye chama kama mkopo na akalipwa.
“Wanasema mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu eti Mkono
alimpatia Mbowe Sh200 milioni kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.
Mwaka huo huo eti Mbowe alipokea Sh100 milioni kutoka kwa Rostam Aziz
kwa ajili ya kampeni,” inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa hakuna ukweli wowote
katika tuhuma hizo, kwamba ni uzushi uliopangiliwa kama moja ya
mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi
wa Chadema hawana tofauti na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Wanataka kuwafanya Watanzania waamini kuwa
viongozi wa Chadema hawana tofauti na wale wa CCM, waamini kuwa chama
hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya Watanzania kionekane
hakina tofauti na chama kilichoko madarakani,” inaeleza.
Inaeleza kuwa lengo la watu hao ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala husika dhidi yao.
“Waliozusha tuhuma hizo, ni vyema wakatunza
heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo
wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya Chadema,” inaeleza na
kuongeza;
“Wajibu masuala ya msingi yanayowaandama kuhusu
mikakati yao ya kuhujumu Chadema na viongozi wake, ambayo iwapo chama
kisingebaini na kuchukua hatua za kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto na
matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa
kuiondoa CCM madarakani.”
Ufafanuzi wa Mkono
Januari 6 mwaka huu Mkono alitoa taarifa kuhusu
tuhuma zilizorushwa dhidi yake na kufafanua kuwa magari mawili aina ya
Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol yanayodaiwa kuwa alimpa Zitto, moja
alimuuzia na jingine amemkodisha.
Kuhusu tuhuma kwamba anawahonga wapinzani wake
wajitoe katika uchaguzi ili apite bila kupingwa alisema katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 alipita bila kupingwa kutokana na
uchapakazi wake wa kiwango kikubwa.
Mkono pia alijibu tuhuma zilizotolewa na Zitto
kwamba Mbowe alipewa mamilioni ya fedha na Mkono kwa nyakati tofauti na
kusema hajawahi kutoa fedha zozote kusaidia Chadema.
Mvutano kati ya Zitto na Chadema ulishika kasi
baada ya Mbunge huyo kufungua kesi Mahakama Kuu kuomba mahakama hiyo
kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua uamuzi wowote
kuhusu uanachama wake hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na
kutolewa uamuzi.
Zitto alishinda katika shauri hilo.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment