Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) Ludovick Utouh
Bukoba. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amemtaka Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Amani kuachia ngazi baada ya Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kubaini ubadhilifu katika miradi ya halmashauri hiyo na ukiukwaji wa taratibu za kusaini mikataba.
Akisoma maelezo ya Serikali kutoka kwa waziri mkuu
baada ya mkaguzi mkuu kuwasilisha taarifa yake,Naibu Waziri wa Tamisemi
Agrey Mwanri alisema jana kuwa, maelekezo ya Serikali kutoka kwa Waziri
Mkuu yanawataka madiwani kumuwajibisha ikiwa atakataa kujiuzulu.
Kwa mujibu wa maleezo hayo yaliyosomwa kwa niaba
ya waziri mkuu, ameagiza aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Hamis
Kaputa ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba,
mkoani Mbeya kuvuliwa madaraka, akiwamo Mhandisi wa Manispaa,Stephen
Mzihirwa na wakuu wengine wa vitengo na idara. Ripoti hiyo ilipelekwa
kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya taarifa ya
CAG kugundua kuwapo kwa makosa mbalimbali ya jinai na ukiukwaji mkubwa
wa taratibu za manunuzi na uingiaji wa mikataba.
Baada ya taarifa hiyo, Meya Dk Anatory Amani
alisema, anakubaliana na maagizo ya Serikali na Naibu Meya, Alexander
Ngalinda alikabidhiwa maelekezo hayo na kuahidi vikao vya madiwani
vitaanza mara moja baada ya kususiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Akisoma matokeo ya ukaguzi huo maalumu, Mkaguzi
Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh pamoja na
kubainisha upungufu na harufu ya rushwa katika miradi mbalimbali pia
amebatilisha uteuzi uliofanywa na Waziri wa Maji kwa kumteua Mulungi
Kichwabuta ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu (CCM) kuingia katika Bodi ya
Maji bila taratibu za kisheria.
Kwa mujibu wa Utouh, waziri huyo wa maji ambaye
hakumtaja jina alikiuka sheria kwa kupendekeza jina ambalo halikupitia
katika mapendekezo ya vikao vya mkoa ambapo mkoa ulikuwa umependekeza
jina la Ashura Hassan viti maalumu CCM.
Katika ripoti hiyo iliyosomwa mbele ya madiwani na
viongozi mbalimbali wa mkoa,CAG alisema Meya wa Manispaa hiyo, Dk
Anatory Amani aliingia makubaliano ya ujenzi wa soko bila madiwani
kushirikishwa huku ripoti ikibaini ukiukwaji wa taratibu katika
uwekezaji wa kituo cha kuosha magari.
Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo kuna uwekezaji
wenye utata kati ya Manispaa ya Bukoba na Benki ya Uwekezaji( UTT)katika
upimaji wa viwanja 5,000 na kuwa baadhi ya kampuni zilizopewa mikataba
hazikuwa na usajili na hazina utambulisho wa mlipa kodi.
Pia CAG amemtaka Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi
Hamisi Kagasheki kukabidhi gari lililosajiliwa kwa namba za Serikali za
mitaa kwa manispaa alilodai alilinunua kusaidia wananchi au alisajili
kwa namba binafsi na kulipa kodi.
Ripoti hiyo ilisema madai ya Meya Dk Anatory Amani
kuhamisha mradi wa maji kutoka Kata ya Nyanga kwenda kwenye Kata yake
ya Kagondo hayakuwa na ukweli kwa kuwa taratibu zilifuatwa ikiwa ni
pamoja na mchango wa wananchi.
Baada ya ripoti hiyo askari polisi walilazimika
kuimarisha ulinzi kufuatia taarifa kuwa wananchi wanaodaiwa kuunga mkono
makundi yaliyokuwa yanavutana kuzingira maeneo ya ofisi za mkuu wa mkoa
wa Kagera na wengine kulipuka kwa shangwe.
Tuhuma za ubadhilifu katika utekelezaji wa miradi
ya Manispaa ya Bukoba ziliibuliwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Balozi Hamisi
Kagasheki katika mkutano wa hadhara kauli iliyoleta mvutano na hata
kuibuka mgogoro uliokosa usuluhishi katika vikao vya chama katika ngazi
tofauti.
Tangu wakati huo mvutano kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani ulisababisha makundi ya uhasama wa kisiasa na hata Serikali kumuomba CAG kufanya kufanya ukaguzi maalumu katika manispaa hiyo.
Tangu wakati huo mvutano kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani ulisababisha makundi ya uhasama wa kisiasa na hata Serikali kumuomba CAG kufanya kufanya ukaguzi maalumu katika manispaa hiyo.
0 comments:
Post a Comment