KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL), imesitisha kwa muda huduma ya usafiri wa treni kwenda mikoani.
Kusitishwa kwa usafiri huo unaotegemewa na Watanzania wengi nchini,
kumetokana na kujaa maji katika stesheni za Godegode na Gulwe mkoani
Dodoma na kuharibu tuta la reli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi wa TRL, Paschal Mafikiri, alisema: “Uongozi
wa Kampuni ya TRL unawaomba radhi abiria wote na wananchi kuwa usafiri
wa treni unasitishwa kwa muda kutokana na kujaa maji katika stesheni za
Godegode na Gulwe mkoani Dodoma na kuharibu tuta la reli.
“Kutokana na uharibifu huo, tunaomba radhi kwa usumbufu
unaojitokeza, tunasitisha kwa muda huduma ya usafiri wa abiria
kuanzia Ijumaa Januari 10, 2014 hadi itakapotangazwa tena, kwa wasafiri
waliokuwa Dodoma tumeshawatafutia usafiri wa mabasi na abiria waliokuwa
Dar es Salaam tumeamua kuwarudishia nauli zao,” alisema.
Mafikiri aliwataka wasafiri wote wenye tiketi halali wafike katika stesheni walizokatia kwa ajili ya kurejeshewa fedha zao.
Alisema kampuni hiyo tayari imetuma mainjinia wake kwa ajili ya kufanya tathmini ili wajue ukubwa wa tatizo na kulishughulikia.
Mafikiri alisema tatizo la kuharibika reli linatokana na mvua
zinazoendelea kunyesha kwenye mikoa ya Dodoma, Morogoro na Iringa ambazo
zinasababisha kuharibika kwa miundombinu ya reli.
Aliwaomba wateja wa usafiri wa treni wawe na subira wakati kampuni ikijitahidi kumaliza tatizo hilo ndani ya muda mfupi.
Abiria zaidi ya 1,600 waliokuwa wakitoka Kigoma kuelekea Dar es
Salaam walishindwa kuendelea na safari baada ya reli eneo la Gulwe na
Godegode wilayani Mpwapwa kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mkuu wa
Stesheni ya Reli Dodoma, Zacharia Kilombele, alisema kulingana na
tathimini iliyofanyika, eneo hilo wameamua kusitisha usafiri wa reli kwa
njia hiyo.
Mkuu huyo alisema kwa kushirikiana na serikali ya mkoa walikubaliana
kuwasafirisha abiria hao kwa mabasi ambapo hadi mchana zaidi ya mabasi
17 yalipakia abiria kuwapeleka jijini Dar es Salaam huku mabasi mengine
10 yakisubiriwa kusafirisha abiria waliobaki.
Kilombele alieleza kuwa changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya abiria
kuwa na mizigo mingi na mikubwa hali inayowapa ugumu katika
kuwasafirisha.
“Usafiri wa treni ya abiria kwenda bara umesitishwa mpaka hapo itakapotangazwa tena,” alisema.
Alisema kinachofanyika sasa ni abiria kurudishiwa nauli zao ili wakatafute usafiri mwingine.
Baadhi ya abiria hao waliiomba serikali kuboresha miundombinu ya reli
kwa kuwa usafiri wa treni utegemewa na wananchi wengi wa kipato cha
chini.
0 comments:
Post a Comment