Utengenezaji wa kucha na uoshaji miguu ni
biashara inayokuwa kwa kasi hasa maeneo ya mijini ambapo wanawake wengi
wanahusudu na kujihusisha na masuala ya urembo.
Biashara hii inazidi kukua huku pia huduma
zinazotolewa zikizidi kuongezeka kila kukicha, ambapo mara nyingi
wanaotengeneza kucha, hujihusisha na usuguaji wa miguu, uchoraji wa
tattoo ukandaji wa mwili (massage)na nyingine zinazofana na hizo.
Kazi hii imetokea kuwa chanzo kimojawapo cha
mapato na ajira mpya kwa vijana wengi hasa wa kiume, wenye umri wa miaka
17 hadi 35.
Hata hivyo, uchuguzi uliofanywa na gazeti hili
hasa jijini Dar es Salaam, umegundua kuwa vijana wengi wanaofanya
biashara hii huishia kufanya ngono na wateja wao hasa wanawake wenye
umri mkubwa na wa kati (Mijimama), ambao wamewahi kuwahudumia zaidi ya
mara moja, hivyo kutumbukia katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya
zinaa na Virusi Vya Ukimwi(VVU).
Kwa mujibu wa takwimu za Ukimwi nchini, vijana
wengi walio kwenye umri kati ya miaka 17 hadi 35 ndilo kundi
linalotajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU.
Hatari hiyo inatokana na mazingira hatarishi
wanayokutana nayo vijana hao wanapofanya shughuli zao na kufanya vitendo
hivyo kwa makusudi, wakati mwingine kwa kushawishiwa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wakati wa ufanyaji wa
shughuli hiyo, hutokea baadhi ya wanawake wakaoshwa au kusuguliwa sehemu
za miguu zinazokaribia maeneo ya mapaja, hivyo kuamsha hisia kati ya
mtoa huduma na mpokea huduma.
Hatua hiyo inatajwa kuwasababashia baadhi yao
kufanya ngono ambayo mara nyingi siyo salama, wanapotoa huduma katika
maeneo tulivu ikiwamo saluni maalumu na nyumbani kwa wateja.
Mmoja wa wafanyabiashara hiyo katika Soko la
Mwenge Hamis Shaban(19) (siyo jina halisi) anasema kuwa kuna wakati
wamekuwa wakiingizwa katika mtego na wateja wao, ambayo huwasababishia
kufanya ngono.
Anasema kuwa hali hiyo hutokea mara nyingi hasa
mteja anapotaka kwenda kuhudumiwa nyumbani kwake, ambapo hukuta tayari
wameandaa mazingira, ambayo mwisho wake huishia katika hatua hiyo
.
.
“Mimi mwenyewe imenitokea siku chache zilizopita;
kuna binti fulani amekuwa mteja wangu kwa muda mrefu, amekuwa
akinifanyia vituko vya hapa na pale. Nilikuwa sijali, ila majuzi
akaniambia niende kwake nikamchore tattoo,” anasema Shaban na kuongeza:
“Eneo alilotaka nimchore ndilo lilianza kunipa
wasiwasi, lakini kwa sababu ya pesa nikapiga moyo konde. Akavua blauzi
yake na kutaka nimchore kwenye titi; nilijaribu kutimiza wajibu wangu,
lakini mambo ambayo alikuwa akifanya, yalinisababishia uzalendo
kunishinda, hatimaye tukajikuta tukifanya ngono.”
Shaban anakiri alifanya tendo hilo bila kutumia kinga akiamini kuwa msichana huyo ni mbichi na hana uwezekano wa kuwa na VVU.
Anafafanua kuwa sababu nyingine iliyosababisha
kufanya ngono ilikuwa kutaka kujenga heshima kwa mteja wake huyo, ili
amwone kuwa ni mwanaume aliyekamilika.
“Yule sista amenifanyia vituko muda mrefu, nikaona
asije kunitangazia vibaya bure kwamba mimi siyo mwanaume kamili; hivyo
kumwonyesha kuwa nimekamilika, nikalazimika kufanya, ingawa sasa hivi
unavyoniuliza naanza kupata wasiwasi.”
Mahamod Abdalah anayefanya biashara hiyo eneo la
Makumbusho, naye anakiri kuwepo na changamoto mbalimbali, ambazo
huwafanya wengi wao kuingia kwenye mitego na kufanya kazi ya
kuwafurahisha wake za watu.
“Hiyo changamoto kweli ipo, inahitaji moyo wa
ziada kukabiliana nayo. Wanakuja wanawake wa haja, utakuta anakufunilia
maungo, anataka umsugue; yaani hatari tupu, sasa kama huna ujasiri,
lazima utaingia kwenye mtego.”
Pamoja na kuingizwa kwenye vishawishi hivyo kuna
muda vijana hao hujikuta katika wakati mgumu, hasa wanapofanya shughuli
hiyo nyumbani na kukutwa na waume wa wateja wao.
“Si wanaume wote wanaelewa kama hii ni kazi,
mwingine akikukuta nyumbani kwake unamsugua mkewe, unaweza kuambulia
kichapo na mambo kama hayo. Hizo ni miongoni mwa changamoto tunazokutana
nazo,”anasema Abdalah.
Kauli ya TACAIDS
Mkurugenzi wa Uraghabishi na Habari wa Tume ya
Taifa ya Kuthibiti Maambukizi ya Ukimwi (TACAIDS), Jummane Issango
anakiri kuwa hali hiyo ni changamoto dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo
unaogharimu maisha ya vijana wengi nchini.
Anasema kuwa kutokana na hali hiyo kwa mwaka huu
wa fedha, TACAIDS imejiwekea mkakati wa kutoa elimu kwa makundi ya
vijana, ambao shughuli zao zinawaweka katika hatari ya kupata maambukizi
ya Ukimwi.
“Kuna fursa nyingi za ajira kwa vijana, ambazo
zimekuwa zikiibuka kila kukicha, lakini kwa bahati mbaya na kasi ya
maambukizi ya Ukimwi inanyemelea katika fursa hizo, ndiyo maana mwaka
huu tunakuja na mkakati wa elimu kwa vijana,”alisema.
Issango aliongeza: “Mpango huu utahusisha vijana
walio shuleni na walio nje ya shule kama vile wasichana wanaojiuza,
wahudumu wa bar na vijana wanaojihusisha na masuala ya urembo kama hayo
kutengeneza kucha, kukanda mwili na mengineyo.”
Anasema kuwa mkakati huo utalenga kutoa
hamasa kwa vijana wapende kujua hali zao kiafya na kujitoa katika hatari
ya kupata maambukizi na kupima VVU kwa hiari.
Mtaalamu wa Afya, Samuel Shitta anasema kuwa hali
hiyo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na masuala ya kisaikolojia, pamoja
na hisia za kimapenzi ambazo huwashika kwa haraka zaidi wanaume.
Anasema kuwa kisaikolojia, wanaume hushikwa na
hisia za mapenzi kwa haraka zaidi kuliko wanawake, hivyo kitendo cha
kuchezea au kusugua mwili wa mwanamke kinaweza kumsababishia akajikuta
akifanya ngono bila kutarajia.
“Wapo ambao inawatokea kisaikolojia, lakini
vilevile kuna kundi lingine ambalo hufanya kwa makusudi kwa lengo la
kujiingizia kipato, wakiamini kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwasaidia
kupata kipato zaidi,”anasema Shitta.
Madhara mengine
Pamoja na madhara hayo, Shitta anafafanua kuwa
kazi hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa pia kuwaweka vijana katika hatari
ya kupata maradhi ya ngozi hasa fangasi kutokana na wengi wao kutotumia
vifaa vya kujikinga.
Anataja pia hatari ya kupata maradhi ya uti wa mgongo, kutokana na kundi hilo kuinama kwa muda mrefu linapokuwa kazini.
“Kufanya shughuli hiyo kwa muda mrefu kunaweza
kumfanya mtu akavunja pingili za mgongo hivyo kupata maradhi ya mgongo,
hususani wakiwa uzeeni,”anasema Dk Shitta.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment