Home »
» Usafiri wa treni: Serikali yaomba mabehewa, injini za treni Uingereza
SERIKALI
ya Uingereza imesema inatafakari ombi la Tanzania la kuomba isaidiwe
mabehewa na injini za treni ambayo nchi hiyo haizitumii tena, lakini
bado ni nzima kwa ajili ya kusaidia kuimarisha usafiri wa reli nchini
hasa wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ahadi hiyo ya Uingereza
ilitolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza, Nicholas William Peter,
wakati akizungumza na Rais Jakaya Kikwete, nchini Uswisi, ambako
viongozi hao wawili walikuwa wanahudhuria Mkutano wa Taasisi ya Uchumi
Duniani (WE F) mwaka huu.
Rais Kikwete alizungumzia hatua za Serikali
ya Tanzania za kuimarisha usafiri hasa ule wa reli mjini Dar es Salaam
na ile ya kwenda Bara.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa
pia na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na
Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, Rais alimwomba, Clegg kuangalia
uwezekano wa nchi hiyo kutoa mabehewa na injini ambazo hazitumiki tena
Uingereza ambazo Rais alisema kuwa bila shaka bado zinafaa kwa Tanzania.
Akielezea
hali ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli nchini, Rais Kikwete,
alisema kutoka na na uchakavu wa reli na ukosefu wa injini na mabehewa
ya kutosha ni kiasi cha tani 300,000 tu za mizigo zinazosafirishwa kwa
reli kati ya mizigo tani milioni 13.7 ambayo inasafirishwa nchini kila
mwaka.
Alisema kuwa kiasi kilichobakia kinasafirishwa kwa barabara.
“Mheshimiwa unaweza kuona uzito wa ninayoyasema kwa sababu tunajenga
barabara nyingi nchini, kila kona, lakini usafirishaji wa namna hii wa
mizigo kwa barabara utaharibu kabisa barabara hizo katika muda mfupi,”
alisema Rais Kikwete.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete
aliishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo
ya Tanzania kwa kusaidia nyanja za elimu, afya na maji na pia kuendelea
kuwa nchi inayoongoza duniani kwa makampuni yake kuwekeza katika uchumi
wa Tanzania. Rais alimwomba Clegg kusaidia kuvutia uwekezaji zaidi
kutoka Uingereza kuja Tanzania kwa kuisemea vizuri Tanzania.
“Neno lako moja la kusifia Tanzania lina nguvu zaidi kuliko hotuba zangu kwa makampuni na wenye makampuni Uingereza,” alisema.
Viongozi
hao pia walizungumzia umuhimu wa kukamilisha mikataba ya Ushirikiano wa
Uchumi ya EPA kati ya nchi za Afrika na nchi za Ulaya. Walikubaliana
kuwa mjadala wa jambo hilo umechukua muda mrefu kupita kiasi na sasa ni
wakati wa kufika mwisho wa jambo hilo.
Rais Kikwete alisema moja ya
sharti linaloikwaza Afrika kufikia makubaliano ya mikataba hiyo ni lile
la kuzilazimisha nchi za Afrika kufungua masoko yao kwa namna ile ile
yatakavyofunguliwa masoko ya nchi za Ulaya.
“Hofu yetu hasa ni
kuhusu jambo hilo. Ni vigumu, kwa mfano, kwa makampuni ya ujenzi ya
Tanzania kushindania tenda moja na kwa masharti yale yale na makampuni
ya Uingereza kwa sababu wakati mwingine unaweza kufungua uwanja ukawa
sawa, lakini wachezaji wasiwe na uwezo unaofanana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment