LATEST POSTS

Tuesday, January 28, 2014

matunda ya gesi: Kusini kuunganishiwa umeme kwa 27,000/-

SERIKALI imepunguza kwa kiasi kikubwa bei ya kuunganisha umeme majumbani na kufikia sh. 27,000 kwa wanavijiji wanaoishi kwenye maeneo ambayo bomba la gesi linapita.
 Hatua hiyo imetangazwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wakati akizungumza na wanakijiji wa Mangaka wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili azindue mradi wa umeme kwenye wilaya hiyo.
“Jana Waziri Mkuu aliagiza tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wanaoishi jirani na njia ya bomba la gesi. Nami nilikaa na wasaidizi wangu jana usiku na kufanya hesabu na tukaamua tuweke kiwango hicho kwa ajili ya wakazi hao,” alisema.
Alisema katika mikoa mingine gharama za kuunganisha umeme ni sh.177,000, lakini kwa mikoa ya Lindi na Mtwara gharama hizo zilishushwa na kufikia sh.99,000.
“Lakini sasa hawa wenzetu tumewapa upendeleo zaidi na tumewapunguzia gharama hizo hadi sh.27,000,” alisema huku akishangiliwa na wananchi na kuongeza: “ Gharama hizo ni maalum kwa ajili ya wakazi waishio jirani na bomba hilo linaloanzia Mtwara hadi Dar es Salaam kupitia mikoa ya Lindi na Pwani.”
Akizungumza na mamia ya wakazi wa Mangaka waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Waziri Mkuu,Mizengo Pinda, alisema uzinduzi wa mradi huo wa umeme ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kila wilaya inapata umeme.
“Mpango wa kupeleka umeme nchi nzima ni wa miaka mitatu na katika sekta ya Nishati chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN), tumeazimia kwenda kwa awamu ili tuwafikie wananchi wengi zaidi kutoka asilimia 24 ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ya watumiaji wa umeme,” alisema Waziri Mkuu.
Akitoa taarifa juu ya mradi huo wa umeme wilayani Nanyumbu, Meneja Mwandamizi wa TANESCO, Kanda ya Dar es Salaam na Pwani inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara, Mahende Mugaya alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni 5.6 na unatarajiwa kukamilika Aprili, mwaka huu.
Alisema kuzinduliwa kwa mradi huo kunafanya wilaya zote za Mkoa wa Mtwara ziwe zimepata umeme wa kuanzia na kwamba kazi itaendelea kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ili kuongeza idadi ya watumiaji wa umeme kwenye mkoa huo.
“Chini ya mfuko wa REA tumetenga sh. bilioni 7.6 ili zitumike kusambaza umeme katika wilaya zote za Mkoa wa Mtwara ambao sasa hivi watumiaji wa umeme wamefikia 15,675 sawa na asilimia nne ya wakazi wote wa mkoa huu.”
Alisema katika mwaka 2012/13 walipata wateja 2,609 tofauti na idadi ya zamani ya wateja 1,300 ambayo ilikuwa imezoeleka. Alisema hivi sasa wamepokea maombi kutoka kwa wateja 2,588 ambao tayari wamekwishalipia gharama za kuunganishiwa umeme.
Chini ya mradi wa umeme kupitia REA, jumla ya vijiji 54 katika wilaya za Tandahimba, Masasi na Newala vitanufaika na mradi huo ulioanza kutekelezwa Desemba 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2015.

0 comments: