WATUMISHI kutoka Wizara ya Ardhi na wale wa Halmashauri ya Bagamoyo
wamejikuta katika wakati mgumu baada ya kutimuliwa katika kikao
kilichoandaliwa na wakazi wa Kijiji cha Makaani Gama, Kata ya Magomeni,
wilayani humo kwa lengo la kujua hatima ya ukazi wao katika eneo hilo.
Hali hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki, saa 7 mchana baada ya
watumishi hao kufika ambako awali walisubiriwa kwa hamu na wakazi hao
ambao walijua wangeendelea na ufafanuzi mzuri kuhusu hatima yao na eneo
hilo linalotakiwa kupewa mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Ecoenergy.
Baada ya kufika kwa ugeni huo kikao kilianza vizuri, lakini hali ya
hewa ikaanza kuchafuka pale Mthamini kutoka Wizara ya Ardhi, Eveline
Mugasha, alipowasilisha mada ya ujazwaji wa fomu ya fidia inayojulikana
kama fomu namba 69, ambayo ilikataliwa awali na wakazi hao kwa madai
mpaka wapate ufafanuzi na kuwashirikisha wenzao waishio mjini.
“Jamani mlishakuja na fomu hiyo majumbani kwetu siku kadhaa
zilizopita tukawakatalia suala lenu hilo, moja ya sababu ikiwa ni
mkanganyiko wa kichwa cha habari kinachosomeka katika fomu hiyo kuwa ni
fomu kwa ajili ya fidia, huyo aliyewaambia tunataka fidia nani wakati
kesi yetu bado ipo mahakamani? Tuna imani tutashinda kwa kuwa mahakama
ndio muamuzi wa mwisho.
“Kama hamjaja na jambo jipya la kutuambia ni vema mkaondoka na
mkatuachia kikao chetu, ili tuendelee kuweka mikakati ya kuendelea
kubaki na eneo letu ambalo tunajua ni haki yetu na mwekezaji
analinga’ang’ania kwa masilahi yake binafsi,” alisema Mwenyekiti wa
Kamati maalumu iliyoundwa na wananchi hao, Ally Mbawe.
Kutokana na hali hiyo, Ofisa Ardhi, Utalii na Mazingira wa
Bagamoyo, Clement Nkusa, alitumia busara kuwapoza wananchi hao ili
kuweza kusikilizana na ugeni huo ambako walimpa dakika chache Kamishna
wa Ardhi, Gasper Luhanga, kutoa ufafanuzi kuhusu fomu hizo.
Katika maelezo yake, Luhanga aliuhakikishia umma huo kwamba ujazaji
wa fomu hizo hauingiliani na wala hautaathiri kesi iliyopo mahakamani,
kwani lengo lao ni kutaka kujua jumla ya wakazi na mali zinazopatikana
katika eneo hilo.
“Wananchi mnapaswa kuelewa ili kijiji kiwe kijiji kuthaminiwa ni
muhimu, na jambo hili msidhani tunalifanya kwa ajili ya kuwaondoa,
badala yake tunataka tujue nani yuko wapi na anamiliki nini, sasa
msichanganye na kutathminiwa kwa ajili ya kulipwa fidia na wala kichwa
cha habari cha fomu kisiwachanganye kwa kuwa ndivyo ilivyotengenezwa na
watunga sheria wetu,” alisisitiza kamishna huyo.
Pamoja na ufafanuzi huo bado baadhi ya wakazi walikuwa wagumu
kuelewa huku wakishauriana kuwa mtu asikubali kujaza fomu hizo mpaka
pale watakapowasiliana na mwanasheria wao.
Wananchi hao waliwataka watumishi hao kuondoka na kuwaacha wenyewe
katika kikao hicho mpaka pale watakapojadiliana na kuja na jibu moja
ambako ilipendekezwa pia kuunda kamati ya ufuatiliaji itakayokuwa
inawasiliana kwa karibu na halmashauri.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment