LATEST POSTS

Wednesday, February 19, 2014

Mabasi ya majini kumaliza msongamano wa magari?


Serikali, mashirika binafsi na wadau wa usafiri ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

Msongamano huo ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uduni wa miundombinu ikiwemo barabara, umekuwa ni kero kwa wananchi na Serikali kwa jumla.
Serikali imewekeza katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (BRT) na usafiri wa treni ndani ya Jiji la Dar es Salaam kama njia mojawapo ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari na foleni.
Msingi wa tatizo
Chanzo kikubwa cha foleni jijini Dar es Salaam si wingi wa abiri
a bali ni wingi wa magari binafsi na njia finyu zisizokidhi mahitaji ya watu walioko katika jiji hilo.
Njia muhimu ya kupunguza foleni na msongamano wa magari ni kupunguza wingi wa magari barabarani na kuweza kuzipanua barabara ili kuwe na uwezekano wa kupita kwa urahisi.
Kutokana na foleni na uduni wa huduma za usafiri wa umma watu wa kundi la kati, wamekuwa wakikimbilia kununua magari binafsi kwa ajili ya kwenda nayo kwenye shughuli zao kwa urahisi.
Aidha, katika kuendeleza harakati za kupambana na tatizo la usafiri, Kampuni ya Transevents Marketing ya Tanzania kwa kushirikana na Kampuni ya Dutch Amphibious Transport Vehicles (DATV) ya Uholanzi inaendelea na mchakato wa kuleta usafiri wa mabasi ya abiria yenye uwezo wa kusafiri nchi kavu na majini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Transevents, Peter Nzunda anasema teknolojia hiyo ya mabasi ya nchi kavu na majini (amphibious) ina lengo la kupunguza tatizo la foleni kwenye barabara za Dar es Salaam hususan katikati ya jiji kwa kuwa mabasi hayo huweza kupita nchi kavu na majini.
Hii ina maana kuwa hata katika maeneo yenye barabara zisizo nzuri au zenye tope, magari hayo huweza kupita hivyo kutosababisha foleni kama ambavyo hutokea sasa katika baadhi ya maeneo hasa mvua zinaponyesha na kuharibu barabara.
Anasema mbali na lengo hilo, mabasi hayo yatatumika kama vivutio vya utalii kwa kufanya utalii wa baharini ambao kwa Tanzania haujashika kasi, licha ya sehemu kubwa ya nchi kuzungukwa na maji.
“Mpango huo wa mabasi ya nchi kavu na majini unalenga kutoa ushawishi kwa watu wa kundi la kati ambao wanatumia magari binafsi waegeshe magari yao na kutumia usafiri huu ambao utakuwa wa hadhi yao na unaokidhi haja kwa ubora wake,” anasema Nzunda na kuongeza:

“Lengo ni kujenga maegesho ya magari maeneo mbalimbali kandokando ya bahari, watu wataegesha magari yao na kupanda mabasi yatakayopita majini kwenda Posta na baadaye kurejea kwa utaratibu huohuo na kuyachukua magari yao tena kwenye maegesho walipoacha magari yao”.
Shughuli za utalii
Nzunda anasema mbali na teknolojia hiyo kutumika kama usafiri wa umma Jiji la Dar es Salaam, mabasi hayo yatatumika kupeleka watalii kwenye hifadhi za taifa zinazozungukwa na maji kama vile Bagamoyo, Mbudia, Mafia na visiwa vingine ili kujionea mambo mengi zaidi ya kiutalii.
“Tunataka pia watu wanaokwenda kwenye fukwe wasiishie kulala na kucheza mchangani, bali wawe wanapanda mabasi haya na kutembelea sehemu  mbalimbali zenye vivutio baharini; hiyo itakuwa ni fursa ya watu kuzunguka baharini wakiwa ndani ya mabasi hayo yatakayokuwa katika miundo tofauti,” alisema Nzunda.
Mahitaji ya mradi
Nje ya Kampuni ya Dutch Amphibious Transport Vehicles (DATV) kutaka kuingiza teknolojia hiyo nchini, Serikali ya Uholanzi pia ipo tayari kuchangia  kwa asilimia 50 ya gharama za mradi wote ambao gharama zake zitajulikana mara baada ya kufanyika tathmini wa mradi.
Aidha, Serikali ya Tanzania, wawekezaji katika sekta ya usafirishaji wa abiria nchi kavu na majini na wadau wengine watatakiwa kuchangia asilimia 50 zilizobaki katika kufanikisha kuanza kwa mradi huo ambao mchakato wa kupata kibali umeshaanza.
Meneja Mwendeshaji wa Transevents Marketing, Mahamud Omari anaiomba Serikali kusaidia uharakishaji wa utoaji wa leseni ya uingizwaji wa teknolojia hiyo mpya ya mabasi.
“Mchakato wa kupata kibali umeshaanza na matarajio yetu ni kufanikisha hatua hiyo baada ya miezi sita kuanzia sasa,” anasema Omari.
Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Edna Rebecca anasema mradi huo wa ‘Mabasi ya Majini na Nchi Kavu’ utatengeneza ajira nyingi kwa vijana wengi na kuongeza fursa za kibiashara kwenye hoteli.
Pia mabasi hayo yataongeza pato la taifa kupitia utalii na maendeleo ya teknolojia hiyo kwa jumla, kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho, ukizingatia takwimu za Shirika la Makazi Duniani, zinaonyesha miaka 50 ijayo, Jiji la Dar es Salaam litakuwa na wakazi wapatao milioni 18.
Mabasi hayo yatatumika kwa shughuli za harusi hasa kwa wanandoa ambao watapenda kufunga ndoa ndani ya maji.Pia yatatumika kwa safari za kitalii za wafanyakazi wa kampuni mbalimbali, wanafunzi, wanakwaya, wanavikundi na klabu za mipira.

“Usafiri huu utakuwa ni wa bei ya kati ambayo itaendana na huduma bora na utalenga kuziba changamoto zote ambazo zinapatikana sasa kwenye usafiri mwingine wa umma,” anasema Rebecca na kuongeza:
“Kuna watu wanapanda magari kwa kulipia Sh1,000 badala ya Sh400 kutoka Posta kwenda Mwenge ili kukwepa adha ya kubanana kwenye daladala zinazokaa muda mrefu kwenye foleni, kwahiyo unaweza kuona ni kwa namna gani watu wanahitaji huduma bora za usafiri wa umma.”
Katika mazingira ya kawaida familia nyingi jijini Dar es Salaam zinatumia magari matatu kwa wakati mmoja yaani baba, mama na mtoto, jambo linaloongeza masongamano barabarani.
Rebecca anasema usafiri huo utawafanya watu hao kuyaacha magari yao nyumbani au kwenye maegesho ya magari yatakayojengwa na hivyo kupunguza kabisa idadi ya magari barabarani.
Mabasi hayo pia yatapunguza gharama za maisha zinazotokana na matumizi ya mafuta kwani kama mtu anaweza kutumia lita 20- 50 kwa siku.
Serikali inasemaje
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), David Mziray anasema teknolojia hiyo ya usafiri wa mabasi ya nchi kavu na majini imekuwa na msaada mkubwa kwa nchi nyingi Ulaya, kuja kwake Tanzania itakuwa ni habari njema hususan wakati huu ambapo jiji linakua kwa kasi.
 “Kazi yetu ni kupokea maombi na kuangalia kama yanakwenda sambamba na sheria na kanuni zetu na kama unavyojua hii ni aina mpya ya usafiri kwa hiyo lazima kutakuwa na mambo ya msingi ya kuyajadili na kuyapatia ufumbuzi kabla ya kuanza,” Anasema Mziray.
Baadhi ya wananchi wanasema mradi huo unaweza kusaidia sana kuondoa kero ya usafiri Dar es Salaam

0 comments: