LATEST POSTS

Friday, February 28, 2014

Mtikila, Makaidi, Kingunge ‘waliteka’ Bunge la Katiba

Mchungaji Mtikila, ambaye jana alizungumza kwa utulivu wakati akitoa hoja zake za kuunga mkono kanuni inayotaka kufanya maamuzi kwa kupiga kura kwa siri.            

Wajumbe watatu wa Bunge Maalumu la Katiba wamekuwa kivutio katika ndani na nje ya Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru.
Mchungaji Mtikila, ambaye jana alizungumza kwa utulivu wakati akitoa hoja zake za kuunga mkono kanuni inayotaka kufanya maamuzi kwa kupiga kura kwa siri, mara nyingi huzungukwa na waandishi wa habari na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wakimsikiliza kwa makini hoja zake. Kikubwa kinachomfanya Mtikila kuwa maarufu ni ile hoja yake ya kutaka kurejea kwa Tanganyika na kuvunjwa kwa Muungano.
Kila anaposimama, Mchungaji Mtikila lazima azungumzie suala la Tanganyika na hata jana aliposimama kuchangia mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo, idadi kubwa ya wajumbe walikuwa makini wakimsikiliza.
Wengine walidiriki hata kupiga meza kuashiria kuwa kitakachozungumzwa na mjumbe huyo, kitakuwa na utata.
Dk. Makaidi amejipatia umaarufu mjini hapa kutokana na kumteua mkewe, Modesta Ponera kuwa mmoja wajumbe wawili wa Bunge hilo.
Uteuzi wake na mkewe  uliibua sintofahamu baada ya Naibu Katibu wa NLD-Zanzibar, Khamis Haji Mussa, kudai kuwa Makaidi aliwasilisha majina mwili, la kwake na mkewe kwa ajili ya uteuzi. Hata hivyo, Dk Makaidi kila anapoulizwa kuhusu tuhuma hizo anasema licha ya kuwa Ponera ni mke wake, pia ni mwanachama wa NLD na kwamba ana haki ya kuteuliwa.
Anasema majina ya chama hicho yaliyopelekwa kwa ajili ya uteuzi, yalifuata taratibu zote.
Wa mwisho ni Mzee Kingunge ambaye uteuzi wake ulizua mjadala mkali kutokana na kuteuliwa kupitia kundi la taasisi zisizokuwa za Serikali.
Baada ya kutakiwa kueleza taasisi aliyotokea, alisema amepitia Kundi la Waganga wa Tiba ya Jadi.
Karibu kila mjumbe anayekutana na Kingunge hupenda kumsalimia kwani tangu aachane na masuala ya siasa, amekuwa haonekani katika maeneo ya mikusanyiko ya watu mara kwa mara.

0 comments: