Dodoma. Wakati mapendekezo ya Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba haijapitishwa, maofisa usalama jana walianza kuzitumia kanuni hizo kuwazuia wanawake waliovaa nguo fupi.
Kanuni hizo ambazo zilitarajiwa kukubaliwa na wajumbe jana jioni, zinazuia wanawake kuingia bungeni wakiwa wamevaa nguo fupi maarufu kama vimini au nguo zinazowabana na kuonyesha maumbile yao.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa baadhi ya wageni waliofika katika Viwanja vya Bunge wakiwa wamevalia nguo fupi walikataliwa kuingia na kutakiwa kwenda kuvaa mavazi ya staha.
Mbali na wageni waliokumbwa na kanuni hiyo, ni waandishi wa habari wawili (majina tunayo), ambao kwa mtazamo wa maofisa usalama, waliamini kuwa wamevaa sketi fupi.
Kanuni ya 82 (9 imeainisha vazi rasmi linaloruhusiwa kuwa ni vazi lolote la heshima ambalo si la kubana mwili, lisiloonyesha maungo na ambalo kwa mila na desturi za Kitanzania, hayapaswi kuonyeshwa.
“Vazi lolote la heshima ambalo si la kubana mwili, lisiloonyesha maungo kwa mila na desturi za Kitanzania na pia liwe refu kuvuka magotini,”imesema sehemu ya mapendekezo ya kanuni hiyo.
Pia imeainisha mavazi mengine ni gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote, suti ya kike, vazi linalovaliwa wakati wa eda na kilemba cha kadri au mtandio.
Mavazi rasmi kwa wanaume ni suti ya kiafrika au ile ya safari ikiwa na mikono mirefu au mifupi na yenye ukosi au shingo ya mviringo.
Wanaume pia wametakiwa kuvaa suti ya nchi za magharibi, shati na tai, suruali ya aina yoyote isipokuwa suruali aina ya `jeans’.
Sehemu ya 6 ya kanuni hiyo, imeweka wazi kuwa mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu, anaweza kutoa taarifa kwenye Bunge au kwenye kamati iwapo mjumbe mwingine ataingia akiwa amevaa vazi linalovunja au kukiuka masharti ya kanuni.
Suala la mavazi lilizua utata wakati vikao vya mwanzo vya Bunge la Katiba limezua utata kutokana na kukosekana kanuni za kuelekeza mavazi.
0 comments:
Post a Comment