Dodoma/Dar. Wajumbe watatu wa Bunge la Katiba ambao ni wabunge wa CCM wametofautiana na msimamo wa chama chao kwa kuunga mkono kura ya siri itumike kuamua ibara za Rasimu ya Katiba.
Hilo lilitokea jana katika mjadala mkali baina ya wajumbe kuhusu ama matumizi ya kura za siri yatumike au kura za wazi.
Katika mjadala huo ulioonyesha mgawanyiko wa wazi, wajumbe wengi wanaotokana CCM na ambao wamekuwa wakipigania kura za wazi, walionekana kuwazidi kwa wingi wale wanaotaka kura za siri.
Wajumbe wa CCM ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muunganom– Esther Bulaya na Profesa Juma Kapuya walijitoa mhanga na kueleza bayana kuwa hawako tayari kuona demokrasia ikikandamizwa kwa kulazimishwa kupiga kura za wazi. Akishangiliwa kwa nguvu, Bulaya alisisitiza kuwa hayuko tayari kulazimishwa kupiga kura ya wazi huku akijua kuwa utaratibu huo unamnyima uhuru wake.
“Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Ni lini na wapi maamuzi magumu kama haya yalifanyika?” Alihoji mbunge huyo wa Viti Maalumu.
Bulaya alisema hakuna sheria inayomtaka mtu kushurutishwa kufanya uamuzi na kwamba kumtaka atoe sauti ya juu katika kura za wazi, ni kumlazimisha kufanya kinyume na matakwa yake.
Alisema kamwe hawezi kuuza uzalendo wake kwa kupiga kura za wazi na kwamba atapimwa kwa utashi wake kuhusu kile anachokiamini. Kwa upande wake, Profesa Kapuya alisema namna nzuri ya kumpa uhuru mpiga kura, ni kutomshurutisha ili afuate matakwa ya wengine.
Alisema kura za siri ndizo zitakazowaimarisha wajumbe na kwamba kinyume chake, kura za wazi zitawagawa na hatimaye kutoka bungeni wakiwa vipande vipande.
Kwa upande wake, Anna Kilango Malecela aliunga mkono ‘kiaina’ kura ya siri akisema alimsikiliza Profesa Ibrahim Lipumba kwa karibu saa nzima kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), akamshawishi kutokana na hoja alizozitoa.
Alisema kwa kuwa suala hilo limezua mvutano mkubwa katika bunge hilo, ni bora likaamuliwa kwa kupigiwa kura ya siri.
Wajumbe wengine
Mjumbe wa Bunge hilo, Sheikh Mussa Kundecha aliunga mkono utaratibu wa kura ya siri akisema ndiyo pekee unaoweza kuwaunganisha wajumbe.
Mchungaji Christopher Mtikila alitumia dakika tano kutoa somo kwa wajumbe wa Bunge hilo, kuhusu umuhimu wa kupiga kura ya siri badala ya kura ya wazi.
“Mwenyekiti, wewe tumekuchagua kwa kura ya siri siyo kwamba tulikuwa wajinga kuliko wenzetu, hapana! Ni democratic civility (ustaarabu wa kidemokrasia),” alisema.
Mjumbe mwingine, Philemon Ndesamburo aliwataka wajumbe kuacha ushabiki wa kisiasa na kwamba lazima wazingatie kwamba wanatengeneza Katiba itakayodumu kwa miaka 50 au miaka 100 ijayo. Hata hivyo, wajumbe, Sixtus Mapunda na Stephen Wassira wote wa CCM, walisema kura za wazi ndiyo suluhisho la kutoa uamuzi juu ya nani anasema nini na kwa wakati gani.
Dk. Zainabu Gama alisema baadhi ya watu wanaotaka kura za siri wametumwa au wamekula rushwa ndiyo maana hawataki kura za wazi.
Wassira alikiri kuwa CCM imeingia na msimamo ndani ya Bunge, lakini alisema hata wajumbe wengine pia wana misimamo yao.
Waunda umoja kuikabili CCM
Katika hali inayoonyesha dhahiri kwamba wajumbe wa Bunge hilo wamegawanyika, vyama vya upinzani na wajumbe wa makundi mengine wameunda umoja wenye lengo la kuhakikisha kuwa Rasimu ya Katiba inapita.
Rasimu hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote kuanzia sasa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Umoja huo umepewa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao sasa unajipanga, kuhakikisha unadhoofisha misimamo ya CCM ya kutaka kuikwamisha.
“Umoja huu pia unawashirikisha baadhi ya wajumbe kutoka CCM wenye msimamo wa kutaka mawazo ya wananchi yapewe nafasi katika Katiba tunayoiandaa,” alisema mmoja wa wajumbe.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari taratibu zimefanyika kwa wajumbe wa Ukawa kukutana na kuweka mikakati.
“Ukawa inaundwa na wajumbe kutoka makundi yote ya uwakilishi katika Bunge la Katiba ambao lengo lao ni kuhakikisha kuwa Katiba inayopatikana ni ile inayozingatia maoni ya wananchi,” alisema Profesa Lipumba.
Mjumbe mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema wameamua kuunda umoja huo ili kupata nguvu ya pamoja na kwamba hatua hiyo imekuja baada ya kugundua kuwa CCM imeandaa waraka wake unaopingana na maoni ya wananchi.
Wajumbe 43 ‘wachomoa’
Wajumbe 43 kati ya 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushiriki katika Bunge Maalumu la Katiba hawajaripoti bungeni hadi kufikia jana.
Hadi jana ikiwa ni siku ya kumi na moja, wajumbe hao walikuwa hawajasajiliwa na kati ya hao ni sita tu waliotoa udhuru katika Ofisi ya Katibu wa Bunge.
Taarifa zilisema wajumbe wengi ambao hawajafika waliteuliwa kupitia makundi ya wakulima, wafugaji na yenye malengo yanayofanana.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema: “Ni kweli kabisa kuhusu hizo taarifa, unajua tangu Bunge limeanza mpaka hii leo (jana) wajumbe 43 hawajaripoti na maana yake ni kwamba hawajasajiliwa. Hao sita wameeleza wazi kuwa wanauguliwa na ndiyo ambao taarifa zao zipo ofisini, ila hao wengine sijui wako wapi kwa sasa.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Tunajua kuna wengine hawajapata ruhusa kazini, wengine wana shughuli maalumuna wengine wameamua kutokuja tu.”
Habari hii imeandikwa na Sharon Sauwa, Daniel Mjema, Fidelis Butahe na Habel Chidawali (Dodoma) na Leon Bahati (Dar).
0 comments:
Post a Comment