Mahakama ya Wilaya ya Geita jana ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka mitano jela Musa Lutobeka (30) baada ya kupatikana na hatia ya kumkata mkewe kiganja cha mkono wa kushoto na kumsababishia ulemavu wa kudumu.
Mahakama hiyo, chini ya Hakimu Zabroni Kesase, ilimhukumu mshtakiwa huyo mkazi wa Bugarama wilayani Geita na imemtia hatiani kwa kosa la kumkata mkono mkewe Leaha Clement (26) mkazi wa Nyamikoma wilayani hapa kutokana na mgogoro wa kifamilia.
Hakimu Kesase alisema mshtakiwa huyo atatumikia kufungo cha miaka mitano jela na kumlipa fidia mwathirika wa tukio hilo, Leah kiasi cha Sh500,000 kutokana na kwenda kinyume cha kifungu cha 225 sura ya 16 ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Awali wakili wa Serikali, Jairo Nyaukumbwa aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda unyama huo dhidi ya mkewe Leah Clement (26), Oktoba 9,2013 katika Kijiji cha Kifufu, Kata ya Bugarama saa 2:00 usiku.
Alisema mshtakiwa alikuwa amehitilafiana na mkewe na kulazimika kwenda kwao ndipo siku ya tukio alipomfuata kwenye Kijiji cha Nyamikoma na kumkata kiganja cha mkono wa kushoto.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Fred aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa kuwa kitendo alichokifanya mshtakiwa ni cha kinyama na kikatili na kwamba hakina utu kwa mtu anayempenda, kumtenda hivyo.
Akisoma hukumu, Hakimu Kesase alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo umedhihirisha bila kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo na hivyo kumhukumu kwenda jela miaka mitanop na kumlipa mlalamikaji Sh.500,000.
0 comments:
Post a Comment