WATU wawili
wanaosadikiwa kuwa majambazi, wamefariki dunia wakiwa njiani kupelekwa
Hospitali ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara ili kupatiwa matibabu baada
ya kujeruhiwa na risasi walizopigwa na wenzao.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Justus
Kamugisha, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 2:40 asubuhi, katika
Kitongoji cha Kokemange, Kijiji cha Nyamwaga, wilayani Tarime.
Alisema
watu hao walipigwa risasi na majambazi wenzao wakiwa njiani kuwapeleka
polisi eneo wenzao walijificha na silaha walizokuwa wakizitumia kufanya
uhalifu.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Wambura Sagare Orondo (26),
mkazi wa Kitongoji cha Nyaichirichiri, Kijiji cha Kitawasi ambaye
alijeruhiwa vibaya tumboni na Shabani Nyang'era 45, mkazi wa Kijiji cha
Borenga, Wilaya ya Serengeti, aliyejeruhiwa kifuani.
"Katika tukio
hili, polisi walijibu shambulio la risasi hivyo majambazi waliojificha
walifanikiwa kutoroka na kutelekeza bunduki moja aina ya G3 ambayo namba
zake zimefutwa na imekatwa kitako pamoja na risasi tano katika
magazini.
"Hawa majambazi waliofariki, walikuwa wakitafutwa muda
mrefu kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha, mauaji na wizi wa
mifugo," alisema Kamanda Kamugisha.
Aliongeza kuwa, chanzo cha tukio
hilo ni baada ya majambazi kutoka nchi jirani ya Kenya, kubaini
wanafuatiliwa na kuamua kujihami kwa kufyatua risasi.
Aliwaomba
wananchi waendelee kutoa taarifa kwa jeshi hilo ili watuhumiwa wa
unyang'anyi na mauaji waweze kukamatwana kufikishwa katika vyombo vya
sheria.
0 comments:
Post a Comment