Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho
amekiri kuwasilisha waraka kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa
chini ya Jaji Joseph Warioba na kupendekeza Zanzibar na Tanganyika kuwa
na mamlaka huru, hatua ambayo imezua malalamiko miongoni mwa makada wa
chama hicho ambao wamesema huo ni usaliti.
Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma, Kificho ambaye
pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), alisema kimsingi
waraka huo ulilenga kuipa nguvu Zanzibar kushughulikia mambo yasiyo ya
Muungano ili kujiimarisha kiuchumi.
Kauli ya Kificho inakuja wakati baadhi ya wajumbe
wa CCM kutoka Zanzibar wakiitisha mkutano na kutoa tamko la kumshutumu
kwa kutoa mapendekezo hayo, wakisema ni kinyume na msimamo wa chama
hicho.
Kificho alionyesha kushangazwa na madai kuwa mapendekezo hayo yaliyoandaliwa na watu wanne ambayo ameyasaini si msimamo wa BLW.
“Tatizo lililopo ni tafsiri ya kila mmoja
anapousoma waraka huo, hakuna sehemu tuliyoandika tunataka Serikali
tatu, mamlaka huru maana yake kila upande uwe na uwezo wa kushughulikia
mambo yake yasiyo ya Muungano na kujijenga kiuchumi, ikiwa ni pamoja
Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya Kimataifa (OIC) na siyo
kuunda dola,” alifafanua Spika Kificho.
Alisisitiza kuwa angependa mambo ambayo hayamo
katika orodha ya Muungano yaendeshwe na Zanzibar bila ya kuwekewa
vikwazo mahali popote.
Madai hayo ni dalili za wazi za mgawanyiko baina
ya wajumbe wa CCM ambao wameanza kuonyesha makundi mawili yenye misimamo
tofauti.
Kundi linalomshutumu Kificho, linawajumuisha
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Juma Ali Shamhuna, Waziri Kiongozi
mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Spika wa BWZ, Ali Abdallah Ali.
Jana, kundi hilo lilimtuhumu Kificho kuwa
hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo Serikali tatu
aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema Baraza la
Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Hata hivyo, mtazamo huo wa BLW unatofautiana na
ule wa Kificho uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Zanzibar, Othman Masoud Othman, ukipendekeza Serikali tatu.
“Kwa vile mfumo wa Serikali mbili uliopo sasa
hauwezi kujenga Muungano utakaohimili mabadiliko ya kisiasa na kwa vile
umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa umeshindwa kujenga Muungano imara,
uachwe katika kuendesha Muungano wa Tanzania,” inasomeka sehemu ya
taarifa hiyo ya Othman.
Jana asubuhi, zaidi ya wajumbe 10 wa Baraza la
Wawakilishi akiwamo Shamhuna, Nahodha na Ali waliitisha mkutano wa
waandishi wa habari mjini Dodoma na kumtupia lawama Kificho wakisema;
“Amewasaliti katika mchakato huo wa Katiba.”
Akizungumza katika mkutano huo, Mnadhimu wa BWZ ambaye pia ni
Katibu wa Wawakilishi wa CCM, Salmin Awadh Salmin alisema katika
uwasilishaji wa maoni ya taasisi hiyo katika Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Baraza la Wawakilishi halikutumia fursa hiyo ipasavyo.
“Ni viongozi wachache tu waliobeba jukumu hili
kubwa na zito bila kuwashirikisha wajumbe walio wengi. Sisi wawakilishi
tunashukuru kwa taasisi yetu hii kupatiwa heshima kubwa ya kutoa maoni
yetu ingawa utekelezaji wake haukuendana na malengo tuliyokusudia.
“…Ieleweke kwamba sisi Wawakilishi wa CCM hatukuwa
sehemu ya maoni yaliyowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kwa vile jambo hilo lilifanyika kwa siri bila kutolewa taarifa kwa
viongozi wakiwamo viongozi wa Kamati ya Uongozi.”
Alisema ni jambo la ajabu na kushangaza kuona taasisi kubwa kama Baraza la Wawakilishi, kuteleza kwa kiasi hicho.
“Tulitarajia baada ya kuteleza huko tungepatiwa
taarifa ili kutambua kilichotendeka. Taarifa na maoni hayo yaliyotolewa
kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi hayakuwa na baraka wala kuvihusisha
vikao husika,hivyo kubeba zaidi maoni binafsi ya viongozi waliohusika,”
alisema na kuongeza:
“Tunaendelea kusisitiza kwamba hatukuwahi kukutana
wala kuamua kuwasilisha maoni hayo, tunatambua pengine wenzetu hao
walikuwa na dhamira njema na pana zaidi hadi kusababisha utaratibu
kusahaulika.”
“Tunapenda kutumia nafasi hii kuwatoa hofu
viongozi na wanachama wetu kwamba Wawakilishi wa CCM katu hatutakisaliti
chama chetu na wanachama wake.
Tutasimamia maelekezo na miongozo ya CCM kwa
gharama yoyote huku tukiamini kwamba Muungano imara na endelevu ni wa
Serikali mbili.”
“Document (waraka), iliyotolewa ameisaini mwenyewe
na jana (juzi) tulivyozungumza (Kificho) alikubali kuwa ni document
sahihi na ni document aliyoisoma wakati akiwasilisha hiyo taarifa. Kwa
hiyo mmoja ni yeye (Kificho), ambaye aliwasilisha mwenyewe, wengine
pengine anawafahamu mwenyewe, lakini sisi hatuwafahamu.”
Alipoulizwa walikuwa wapi tangu Jaji Warioba
alipotoa msimamo wa Baraza la Wawakilishi, Salmin alijibu: “Ni muda
mrefu na wakati Jaji Warioba alipowasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa
msimamo wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni Serikali tatu, sisi
tulishangazwa sana kauli hiyo.
“Mimi mwenyewe nikiwa Mnadhimu niliwasiliana na
kiongozi wa taasisi ile (Kificho), nikamuuliza kuhusu taarifa
iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
akanihakikishia kuwa taarifa hiyo siyo sahihi na sivyo ilivyokuwa.”
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment