Licha ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ahadi ya kuteketeza maelfu ya
meno ya tembo yaliyo kwenye ghala la Serikali, imeelezwa kuwa uwezekano
huo ni mdogo.
Mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza,
Martin Fletcher ameeleza kushtushwa na hali ya ulinzi kwenye ghala hilo
lililosheheni meno 34,000 ya tembo ambayo kwa biashara ya magendo nchini
China yanagharimu Pauni 150 milioni za Kiingereza (Sh403.5 bilioni)
Fletcher, ambaye aliandika habari ya kuhusika kwa
wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania katika biashara haramu
ya meno hayo kiasi cha kuifanya nchi kuwa muuzaji mkuu wa nyara hizo,
aliandika hayo kwenye taarifa kuhusu ziara yake nchini iliyochapishwa na
gazeti hilo jana.
Habari ya awali ilitikisa ulimwengu ambao
unapambana kulinda viumbe walio hatarini kutoweka ikiwatuhumu wanasiasa
na wafanyabiashara wakubwa nchini kuhusika, huku Serikali ikishindwa
kuwadhibiti.
Habari hiyo iliifanya Serikali ya Tanzania
kufungua milango kwa vyombo vya habari vya nje kuja nchini kupata habari
sahihi kuhusu tatizo hilo, akiwamo Fletcher wa Daily Mail.
Katika ziara yake, Fletcher alipata nafasi ya
kutembelea ghala la nyara hizo, kuzungumza na maofisa wanyama pori
pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
“Nyalandu pia aliweka bayana kuwa uteketezaji wa
shehena ya Tanzania ni kitu ambacho kiko mbali na uhalisia, licha ya
ahadi ya Kikwete jijini London,” Fletcher alimkariri Nyalandu kwenye
habari hiyo ambayo imeambatana na picha alizozielezea kuwa za kushtua za
ghala hilo, lenye idadi kubwa ya meno ya tembo kuliko maghala yote
duniani.
“Alisema Rais alikuwa na nia ya kuteketeza
(shehena hiyo), lakini Tanzania ilitaka ilipwe takriban Pauni 30 milioni
za Uingereza kutoka Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi
ya Tembo.”
Hata hivyo mwandishi huyo anaripoti kuwa;
“Wahisani ambao wangeweza kutoa fedha hizo, walikejeli kiwango hicho
wakisema hakina uhalisia.”
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo jana, Nyalandu
alisema baadhi ya mambo kwenye habari ya mwandishi huyo yamekuzwa,
lakini alisema uamuzi wa kuteketeza nyara hizo haujafikiwa.
Alisema Serikali ilichofanya hadi sasa ni kupiga
marufuku biashara zote za meno ya tembo, hivyo haitauza yaliyopo na
haitaomba kibali tena cha kufanya biashara hiyo na kwamba kinachoendelea
sasa ni mazungumzo ya namna ya kushughulika na shehena iliyopo.
“Meno mengine yaliyopo ni ya kihistoria. Ni marefu
kuliko mengine na tembo wa aina hii hawapo tena, hivyo kuwa nayo pia ni
kitu kizuri. Haya meno ni mali ya Watanzania wote, uamuzi wa
kuyateketeza lazima uchukuliwe kwa busara,” alisema.
Kwa mujibu wa Fletcher meno mengine yana urefu wa futi 7, uzito
wa tani 125 na moja linaweza kubebwa na watu kuanzia watatu, huku jino
fupi likiwa na uzito wa kilo 0.4500 na kwa mujibu wa jangili aliyekiri
kuua tembo 30 kwa siku, jino hilo dogo liling’olewa kutoka kwa tembo
mtoto.
Mara tatu katika kipindi cha miaka minane,
Tanzania imeomba bila mafanikio kibali cha kuuza shehena yake kutoka
katika nchi 180 zilizosaini makubaliano ya kudhibiti biashara ya
kimataifa ya viumbe walio hatarini kutoweka, Cites, licha ya ushahidi
mkubwa kuwa kitendo cha kuuza mara moja tu, kitazidisha tamaa ya China
kupata meno hayo.
Akizungumzia ziara yake nchini, mwandishi huyo
anaelezea udhaifu katika ulinzi wa ghala hilo lililo nyuma ya jengo la
Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.
“Ghala hilo niligundua siyo kama ngome (yenye
ulinzi mkali). Lina milango ya chuma ya kusukuma ikiwa na kufuli nzito
tano ambazo funguo zake zimegawanywa kwa maboharia wawili, lakini
milango ilifunguliwa yote nilipofika,” makala hiyo inaeleza. “Kila jino
limewekwa alama na namba na ghala ina kamera za ulinzi wa ndani, lakini
sikuona mlinzi mwenye silaha nje.”
Mwandishi huyo anaeleza kuwa habari yake ya kwanza
iliyohoji kama mtoto wa Mfalme wa Wales na Waziri Mkuu wanaweza
kushikana mkono na Rais Kikwete wakati alipotembelea Uingereza, ilizua
kizaazaaa kiasi cha Rais Kikwete kuitisha kikao na maofisa waandamizi wa
Maliasili na kutoa maelekezo kuwa wafanye kazi.
Mwandishi huyo alitembelea maghala ya meno ya
tembo, Hifadhi ya Selous ambayo mwaka 2006 ilikuwa na tembo 70,000
lakini hadi sasa wamesalia 13,000 tu. Baadhi ya meno yalichukuliwa
kutoka tembo waliokufa na mengi kukamatwa kutoka kwa majangili na
hayawezi kuuzwa kwa sababu ya biashara hiyo kuzuiwa duniani.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment