Kwa neno moja unaweza kusema kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa ujumla wako “njiapanda”.
Hii ni baada ya hotuba ya ufunguzi wa Bunge hilo
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuibua mambo mazito ambayo kimsingi
yanatofautiana na mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa bungeni na mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba.
Huku wananchi wakijiuliza nini hatima ya Bunge
hilo baada ya hotuba hiyo, baadhi ya wajumbe ambao wiki hii ndiyo
wanaanza kujadili rasimu hiyo, watakuwa katika wakati mgumu wa kuamua
wafuate maoni ya nani, kati ya viongozi hao wawili.
Ingawa Rais Kikwete amesema mara kadhaa kuwa
wajumbe wa Bunge la Katiba ndiyo waamuzi. Mambo mengi aliyoibua
yanaonyesha kutokubaliana kwake na baadhi ya maoni ya wananchi yaliyomo
katika rasimu, ambayo Jaji Warioba amewahi kusema kuwa yanatakiwa
kuheshimiwa.
Wakizungumzia tofauti hizo, mjumbe wa Bunge la
Katiba, Ezekiah Oluoch alisema kauli za Rais Kikwete na Jaji Warioba
zimezidi kuwagawa wajumbe wa Bunge hilo kwa maelezo kuwa tangu awali
wajumbe hao walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili; ya wanaotaka
muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu na wale wanaotaka serikali
mbili.
Alisema kama suala la muundo wa Serikali
likishindikana kupatiwa mwafaka ni vyema likarudishwa kwa wananchi ili
wapige kura ya maoni kuchagua aina wanayoitaka, kisha suala hilo
lirejeshwe tena katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kuboreshwa.
“Rais alipoanza kuzungumza alikuwa kama mkuu wa
nchi lakini mwisho wa hotuba yake aligeuka kuwa mwenyekiti wa CCM.
Kifupi alichokizungumza kimekwenda tofauti na wadhifa wake,” alisema.
Naye Deo Filikunjombe alisema: “Nadhani kwa hotuba
hizi mbili, kazi ya wajumbe wa Bunge la Katiba itakuwa rahisi. Maana
sasa wameshajua uzuri na ubaya wa serikali tatu na mbili.
“Hata kama kutakuwa na tofauti, wananchi ndiyo
watakuwa wa mwisho kuamua kama Katiba hii ipite au isipite.
Tunachotakiwa wajumbe ni kuwa makini na uamuzi wetu.”
Naye Yusuf Manyanga alisema: “Bunge la Katiba
limejaa watu wenye busara. Sidhani kama tutashindwa kuelewana maana hata
katika biashara ya utumbo inzi ni wengi lakini utumbo unauzika.”
Katika hotuba yake aliyoitoa Ijumaa iliyopita Rais
Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika rasimu ya Katiba
na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani
kutekelezeka.
Muundo wa Serikali
Jambo kubwa pengine kuliko yote linaloliweka Bunge na wananchi
njiapanda ni kuhusu muundo wa Serikali na Rais Kikwete ameweka wazi
kuegemea katika muundo wa serikali mbili, wakati rasimu inayojadiliwa
imependekeza serikali tatu.
Rais Kikwete akisema iwapo mfumo wa serikali tatu
ukipita ni lazima serikali ya tatu ijengewe msingi imara kwa sababu
haitakuwa na chanzo cha uhakika cha mapato yake yatakayoiwezesha
kusimama yenyewe. Rasimu inasema Serikali ya Muungano itakuwa na mapato
yatokanayo na ushuru wa bidhaa, mapato yasiyo ya kodi, michango ya nchi
washirika na mikopo ya ndani na nje.
Kuhusu ulinzi, Rais Kikwete alisema: “Kama
tunataka serikali ya tatu lazima tuitengenezee misingi ya uhakika na
kuhoji nani atayeidhamini serikali ya tatu virungu, pingu, magari ya
kuwasha, majeshi au bunduki.”
Lakini Jaji Warioba, ambaye tayari alishasema
msimamo huo ni maoni binafsi ya Rais Kikwete na hawezi kuyazungumzia,
aliwatoa hofu wananchi na wajumbe akisema muundo wowote wa Serikali
utakuwa na changamoto zake, kwamba hata muundo wa serikali tatu utakuwa
na changamoto zake, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa gharama ingawa
hazitakuwa kubwa kama inavyofikiriwa.
Warioba alifafanua kuwa gharama kubwa kwa shughuli
za Muungano ni katika eneo la ulinzi na usalama, yaani Jeshi la
Wananchi, Polisi, Usalama wa Taifa na mambo ya nje na kwamba gharama
hizo hazibadiliki. Alisema zitabaki kama zilivyo bila kujali kama ni
muundo wa serikali mbili au serikali tatu.
Alisema tangu Muungano uundwe, Serikali ya
Muungano na Serikali ya Zanzibar zimekuwa zikiongeza wizara, mikoa,
wilaya na taasisi mbalimbali za kiutawala ili kuongeza ufanisi na hivyo
kuongeza matumizi ya Serikali, lakini gharama zinazoonekana ni hizo za
serikali ya tatu.
Mambo yasiyotekelezeka
Katika hotuba yake Rais Kikwete alisema baadhi ya
vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi ambayo
hayapaswi kuwemo katika Katiba, bali yangekuwa katika sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe. Kwa mfano, alisema ikiwa
kila jambo likiwekwa katika Katiba kuna hatari ya Serikali kujikuta
inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo
moja au jingine ambayo haina uwezo nayo.
Lakini Warioba alisema katika nchi yoyote, msingi
wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba ambayo ni sheria kuu au sheria
mama. Hivyo sheria nyingine zote zinategemea au zinatungwa kwa mujibu wa
Katiba. Aliongeza kuwa Katiba ni makubaliano ya wananchi kuhusu
utaratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao,
inaweka mfumo wa uendeshaji wa nchi kwa kuainisha misingi ya taifa,
mgawanyo wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi
wake, mgawanyo na ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola.
Mipaka ya nchi
Kuhusu mipaka ya nchi, Rais Kikwete alisema si
sahihi rasimu ya Katiba kusema tu “eneo la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari
na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Alisema maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande
wa Tanzania Bara, sehemu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa na ni lazima
mipaka hiyo ya maziwa na mito iwekwe katika Katiba ili kuzuia nchi
fulani kudai ziwa au mto fulani ni wao.
Kuhusu suala hilo, Rasimu ya Tume imependekeza eneo la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania lijumuishe eneo lote la iliyokuwa Jamhuri ya
Tanganyika ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la iliyokuwa
Jamhuri ya watu wa Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari, kama
ilivyoainishwa katika Katiba za Uhuru za nchi hizo mbili.
Kupoteza ubunge
Jambo jingine ambalo linaonekana halikumfurahisha
Rais Kikwete katika Rasimu ni suala la mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya
kuugua kwa miezi sita mfululizo.
“Kwa maoni ya watu wengi suala hilo ni ukatili ambao haustahili kufanywa na Katiba,” alisema Kikwete.
Alisema kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine mbunge anaweza kupata ajali wakati akiwatumikia wananchi wa jimbo lake.
Kauli hiyo ni tofauti na inavyoelezwa katika Ibara
ya 128(1)(d) ya Rasimu ya Katiba ambayo inasema: ‘Mbunge atakoma kuwa
mbunge ikiwa atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa muda wa miezi sita
mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza.
Vipindi vitatu vya ubunge
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema ni mapema
mno kuanzisha utaratibu wa ukomo wa vipindi vitatu vya mtu kugombea
ubunge na kusisitiza kuwa jambo hilo litawanyima watu wenye maarifa na
uzoefu mzuri wa uongozi katika nafasi ya ubunge.
Hata hivyo, Jaji Warioba alisema pendekezo hilo
linatokana na maoni ya wananchi waliotaka kuwapo ukomo wa ubunge ili
kuondoa dhana ya umiliki wa jimbo la uchaguzi, kutoa fursa kwa wananchi
wengine wenye uwezo kugombea nafasi ya ubunge na kuongeza uwajibikaji wa
wabunge katika majimbo.
Kumwondoa mbunge
Rais Kikwete alisema kitendo cha kumwondoa mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi kuna athari na kuwataka wajumbe wa
Bunge la Katiba kuzitafakari
Alisema jambo hilo linaweza kuanzisha misuguano
kwenye majimbo na kuwaacha wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali
wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa.
Kuhusu suala hilo, Jaji Warioba alisema wananchi wanaweza
kumwondoa mbunge madarakani iwapo atakwenda kinyume na masilahi ya
wapigakura, kushindwa kutetea kero zao na kuacha kuishi au kuhamisha
makazi katika jimbo husika.
Mawaziri kutokuwa wabunge
Katika maelezo yake Rais Kikwete alisema ni vigumu
kutenganisha uwaziri na ubunge kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa
kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali, lakini Jaji Warioba alisema
nia ya pendekezo hili ni kutenganisha mamlaka na madaraka ya mihimili na
kuliwezesha Bunge kufanya kazi yake ya kuisimamia Serikali.
Wakati huohuo, Bunge la Maalumu la Katiba leo
litafanya uchaguzi wa wenyeviti wa kamati ikiwamo Kamati ya Uongozi
itakayoshauri suala la upigaji kura ambalo liliwekwa kiporo kutokana na
mgawanyiko wa wajumbe wa ama iwe ya siri au ya wazi.
Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alisema leo Mwenyekiti wa Bunge Samuel Sitta atatangaza kamati 12.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment