Katibu Mkuu, Nicholaus Mgaya, akifafanua jambo kwenye moja ya mikutano
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) jijini Dar es Salaam.
Uongozi
wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) umetakiwa kujiuzulu kwa
tuhuma za kushindwa kuliongoza kifaida shirikisho hilo, huku Katibu Mkuu
wake akiwekwa kikaangoni akidaiwa kuhusika na hali hiyo na
kung’ang’ania madaraka licha ya muda wake wa kustaafu kufika.
Kauli hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TUCTA waliokutana kujadili hatma ya
shirikisho baada ya kutolewa kwa ripoti ya mkaguzi wa hesabu za mapato
na matumizi iliyoonyesha kasoro kadhaa.
Wakizungumza kwa jazba nje wa ukumbi wa mkutano,
baadhi ya wajumbe walimlaumu Katibu Mkuu, Nicholaus Mgaya kuwa ndiye
aliyelifikisha shirikisho hilo hapo lilipo na kwamba umri wa kustaafu
umefika lakini anataka kuendelea kukaa madarakani.
Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, William Mboma alisema
ingawa TUCTA ina majengo mengi nchini, imekuwa ikikusanya mapato kidogo
kwa mwezi, wakati jengo moja lililopo Arusha lina uwezo wa kukusanya
zaidi ya Sh600 milioni.
“Ghorofa la Arusha tu endapo mapato yatasimamiwa
tungeweza kupata zaidi ya Sh600 milioni kwa mwezi lakini leo hii
tunaambiwa kuwa majengo yote Tanzania nzima tunakusanya Sh13 milioni,
inawezekana fedha zinaingia hazijulikani zinakokwenda,” alisema Mboma.
Alibainisha kuwa ripoti ya hesabu za mapato na
matumizi ya TUCTA iliyofanywa na kampuni ya Ernst & Young inaonyesha
kuwa shirikisho hilo limeshindwa kukusanya fedha kutoka katika vyanzo
vyake.
Pia alisema kuwa Tucta imekuwa ikishindwa
kutekeleza maagizo mbalimbali yanayoagizwa na Baraza Kuu, hivyo katika
kikao hicho walipendekeza Kamati Kuu itoke nje ili wajadili hatma ya
shirikisho, lakini walizuiwa kutekeleza uamuzi huo.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Idrisa Washington
alisema kikao hicho kimekuwa na msuguano baina ya wajumbe kwa kuwa hiyo
ni hali ya kawaida wakati watu wanapotaka kuleta mabadiliko yenye kuleta
maendeleo. “Katika dunia ya demokrasia kila mtu ana mawazo yake, haya
ni masuala mazito, kuna pande mbili, shirikisho na Serikali mwisho wa
siku lazima kuwa na mvutano,” alisema Washington.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la TUCTA, Musa
Mnyeti alisema mgogoro ndani ya shirikisho hilo ulianza mwaka jana baada
ya Katibu Mkuu, Nicholas Mgaya kutuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya.
“Alitumia madaraka vibaya kwenye Chuo cha
wafanyakazi Mbeya, alipendelea watu wa kwenda kusoma Afrika Kusini na
Italia, pia alifanya upendeleo kwa namna mkuu wa chuo aliyemaliza muda
alivyotakiwa kupata stahili zake,” alisema Mnyeti.
Mjumbe mwingine wa Baraza, Lameck Mahewa, alisema
kikao hicho kilipaswa kuwa wazi kwa waandishi kuingia, lakini katika
hali isiyofahamika, waliambiwa wakae nje wasubiri hadi kitakapomalizika.
“Msajili wa vyama na shirikisho anatakiwa kutazama
upya namna Tucta inavyoendeshwa, mikataba imefichwa haipo wazi, mibovu
inayowanufaisha wachache,”
Waandishi wa habari walipopata nafasi ya kuingia kwenye ukumbi
huo, walimwomba Katibu Mkuu, Mgaya kuzungumzia masuala yaliyojiri
kwenye kikao hicho, lakini alisema yeye siyo msemaji wa TUCTA na kwamba
hakumwita mwandishi yeyote.
Akizungumza nje ya ukumbi wa mkutano huo, Kaimu
Rais wa TUCTA, Nortimuga Masikini alisema hakuna maazimio yoyote
yaliyofikiwa na kwamba hakuna suala lolote lililooneka kuleta mvutano.
0 comments:
Post a Comment