Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wakimshangilia Juma Duni Haji
(aliyevaa kanzu) nje ya ukumbi wa bunge baada ya mjumbe huyo
kuwalisilisha bungeni maoni ya waliowachache ya Kamati namba11.
Shamrashamra za wajumbe wanaounga mkono serikali tatu na mbili,
nje ya Bunge jana, ziliendelea baada ya Mjumbe, Juma Duni Haji kutoa
ufafanuzi wa kutetea serikali tatu na kuwavutia wajumbe, ambao walitoka
ukumbi wa bunge wakimshangilia babu, babu, hawatuwezi hawatuwezi.
Tukio hilo ambalo ni mfululizo wa vijembe, baina
ya wajumbe wa CCM na upinzani, kuhusu hoja ya serikali tatu au mbili,
lilisababisha viwanja vyote vya bunge jana mchana, kutawaliwa na kelele
za kushangilia na kuzomeana.
Akitoa ufafanuzi wa kamati namba 11, Duni alisema
siyo serikali tatu ni ufumbuzi wa malalamiko ya Muungano, ambayo
yanaifanya Zanzibar kuendelea kubanwa na kushindwa kuwapatia maendeleo
wananchi wake.
Alisema serikali iliyopo madarani kwa miaka 50
sasa, imeshindwa kutumia rasilimali zilizopo Zanzibar na kuifanya iwe
kutovu cha utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati badala yake
inazuia kila jambo jema la maendeleo.
“Kama mngekuwa na dhamira ya dhati na Zanzibar,
leo Zanzibar ingekuwa kama Hong Kong ya Afrika lakini hakuna, Zanzibar
imefungwa mikono na miguu hata kutembea haiwezi,” alisema.
Alisema hoja kuwa katika muundo wa serikali tatu,
ukianza Zanzibar haiwezi kuchangia Muungano siyo ukweli kwani, uchumi wa
wananchi wa Zanzibar hauna tofauti na uchumi wa Watanganyika kwa mtu
mmoja moja. Akizungumzia takwimu za tume ya mabadiliko alisema zipo
sahihi kuwa waliotaka Muungano wa Serikali tatu ni wengi lakini
kinachofanywa na wanaotaka serikali mbili ni kupotosha ukweli.
Haji alitolea mfano katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2010, kuwa walioandikishwa kupiga kura walikuwa ni watu 20 milioni,
waliopiga kura ni watu milioni nane na ambao walimchagua Rais Jakaya
Kikwete ni watu milioni sita hivyo kwa hoja ya wanaCCM kuhusu Rasimu ina
maana watu 14 milioni hawamtaki Rais Kikwete.
Akizungumzia gharama za Muungano, alisema fedha
nyingi zaidi ya asilimia 70 za Muungano, zinatumika katika kuendesha
Serikali ya Tanganyika jambo ambalo siyo sahihi.
Huku akitoa takwimu mbalimbali, alisema kwa maana
hiyo uchangiaji wa Muungano kamwe hauwezi kuwa sawa kwa pande zote.
“Katika jambo moja tu la askari polisi, tafiti za kimataifa zinaonesha
kuwa askari mmoja anafaa kulinda watu 400, kwa Zanzibar yenye watu 1.3
milioni inahitaji askari 3,000 tu, lakini Tanganyika yenye watu zaidi ya
40 milioni inahitaji zaidi ya askari 120,000 hivyo uchangiaji wa
Muungano hauwezi kuwa sawa,” alisema.
Haji pia alieleza kuwa, hati za Muungano ambazo
waliowengi wanasema zinamsingi wa serikali mbili, siyo kweli bali hati
hizo zinatambua serikali tatu, ikiwapo ya Tanganyika.
Hata hivyo, alisema msingi wa serikali mbili ni
mkakati wa CCM ambao ulianza tangu enzi za TANU mwaka 1977, kutaka kuwa
na serikali moja na hivyo, kuifanya Zanzibar kuwa siyo nchi.
0 comments:
Post a Comment