Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Prof Ibrahimu Lipumba akizungumza
katika kikao cha bunge jana ambapo alitangaza kujitoa kwa baadhi ya
wajumbe kuendea na mchakato wa kupitisha Rasimu ya Katiba, mjini Dodoma
jana.
Mambo yamebadilika. Ukimya ulitawala jana katika Ukumbi wa Bunge
mjini Dodoma, baada ya wabunge zaidi ya 200 ambao ni wanachama wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vya Bunge hilo.
Ilikuwa ni saa 10:31 jioni baada ya Mjumbe wa
Bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alipohitimisha uchangiaji wake akisema: “Ukawa hatuwezi kuendelea
kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni
kinyume cha matakwa yao.”
Baada ya kauli hiyo aliondoka akifuatiwa na
Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na wajumbe wao kutoka nje ya
Bunge.
Ukimya ulitawala takriban dakika mbili hivi na
baada ya wajumbe hao kutoka, Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samia
Suluhu Hassan aliwaelekeza makatibu kuhesabu wajumbe ili kuona kama
akidi imetimia ili waendelee na kikao.
Baadaye aliliambia Bunge kuwa makatibu wamemweleza
hawahitaji akidi kwa kuwa kikao kilikuwa kinaendelea wakati Ukawa
walipotoka nje ya ukumbi.
Hotuba ya Lipumba
Profesa Lipumba alianza kwa kunukuu Gazeti la
Mwananchi la Aprili 14, mwaka huu katika sehemu inayosema; “Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) ameanza kampeni
kanisani kwa kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa
kuwa serikali ya muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.”
Alisema yeye ni muumini wa dini ya Mwenyezi Mungu
lakini anaafiki mapendekezo yaliyoletwa bungeni hapo na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais.
“Hii ni kauli ya Waziri Lukuvi ndani ya Kanisa la
Methodist wakati wa sherehe ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa
Askofu na Waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu.”
Alisema inasikitisha kwa sababu kauli hiyo inafanana na ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akihutubia Bunge Maalumu.
Alisema kauli za Lukuvi zinatisha baada ya kusema
Wazanzibari ambao wanataka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali
wanataka wapate nafasi ya kujitangazia kuwa ni nchi ya Kiislamu.
“Waziri anaweza kusema hivyo ndani ya kanisa?
Kawahamasisha mpaka yule kiongozi wa kanisa akasema ili kudumisha
Muungano bora Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja
ambayo inadumisha Muungano,” alisema.
Alisema Lukuvi alikuwa akiwaaminisha kuwa mfumo wa serikali tatu
ukipita kutakuwa na mapinduzi na nchi haitatawalika na hivyo watu
watashindwa kwenda kusali makanisani.
“Kama ndugu zetu wa Zanzibar wangekuwa wanahitaji
serikali moja tungekuwa na utaratibu mzuri tu, lakini siyo wanachama wa
CUF, siyo wa CCM, Wazanzibari wote hawataki muungano wa serikali moja,”
alisema.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa
mapendekezo ya serikali tatu kutokana na ukweli huo. “Hoja zilizoletwa
hapa ni hoja za serikali moja, si hoja za serikali mbili lakini wenzetu
moja hawataki, kwa hiyo tunahitaji Muungano ambao tutakuwa na maridhiano
ya pande zote mbili,”
“Wengi wamenukuu makala niliyoitoa katika kituo
cha TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania), ambayo iliunda Baraza la Katiba
na mimi nilichambua mapendekezo ya Tume nikasema kwa mapendekezo
yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba hayatakidhi mapato ya shirikisho.”
Alisema wajumbe wanaomnukuu wanaishia hapo bila kwenda katika mapendekezo aliyoyatoa.
“Wamenisifu sana ni mchumi mahiri, basi waendeleze
sifa hizo kwa mapendekezo niliyoyatoa ya mapato ya kukidhi uendeshaji
wa serikali ya shirikisho.
“Nimeeleza katika hali halisi kuwa utaratibu mzuri
ni mapato ya kila serikali kuchangia katika shirikisho na mambo haya
yaandikwe katika Katiba. Katiba inaweza ikasema wazi asilimia 20 ya
mapato yote yanayokusanywa Zanzibar au Tanganyika yataenda kwenye
shirikisho.”
Alitaka pia kuwekwa kwa misingi mizuri ya
kukusanya kodi na kutumia fedha za wananchi ndani ya katiba ya muungano
ambayo ndiyo katiba mama.
“Lakini ndugu zangu mjadala wetu unavyokwenda
utadhani kuwa Rasimu ya Katiba iliyoletwa imeletwa na CUF au na Chadema
au na NCCR-Mageuzi, au Wapemba,” alisema.
Alisema ukurasa wa kwanza wa Rasimu ya Katiba
unaeleza kuwa toleo hili la Rasimu ya Katiba lilichapishwa katika Gazeti
la Serikali kwa mujibu wa Kifungu cha 20(2) ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba Sura ya 83.
Alisema hiyo ni rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba.
Hata hivyo, alisema mjadala unaoendelea bungeni
umekuwa na utaratibu wa ubaguzi... “Watu wamebaguliwa humu na viongozi
wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la Intarahamwe.
Hii ni hatari kwa nchi yetu. Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo,”
alisema.
“Hii hatuhitaji, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila
mwananchi anapata haki yake wote tuwe sawa bila kujali rangi zetu,
jinsia zetu, makabila yetu, huu ndiyo msingi aliotuachia Mwalimu Nyerere
tuenzi msingi huo.”
Alilalamikia kile alichokiita kuwa ni ubaguzi
ndani ya Bunge na kwamba kama Serikali haikutaka Katiba Mpya kwa nini
imepeleka wabunge Dodoma? Pia alihoji ni kwa nini ilitumia Sh70 bilioni
katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa nini mmetufikisha hapa? Jengo hili nimeambiwa
limekarabatiwa kwa Sh8.2 bilioni hali hamuamini Rasimu ya Katiba ama
ilikuwa ni utaratibu wa kupata hizo asilimia 10, ndiyo maana mmekarabati
kwa gharama kubwa?” alisema.
“Tunataka CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali), akague matumizi ya fedha zilizotumika. Utatumiaje fedha
nyingi wakati hiyo katiba iliyowasilishwa kumbe huitaki kabisa.
“Hakuna utaratibu wowote wa kupiga kura na kufanya
maamuzi kuhusu sura hizi mbili. Tumechoka kusikiliza matusi. Tumechoka
kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya
kundi linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatukubali,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment