Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam siku wakichimba udongo chini ya Daraja
la Mto Msimbazi lililopo Tabata Matumbi jana kutafuta miili ya ndugu zao
waliozolewa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika
maeneo mbalimbali ya jiji
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya mvua
kubwa kunyesha tena kuanzia leo na kesho katika ukanda wa Pwani.
Katika taarifa yake kwa umma jana jioni, TMA
imesema maeneo ambayo yataathiriwa na mvua hizo za kuanzia leo ni Visiwa
vya Unguja na Pemba pamoja na mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam.
Huo ni mwendelezo wa mvua zilizosababisha maafa
makubwa ambazo zilianza kunyesha Aprili 10, mwaka huu katika ukanda huo
wa pwani. Maeneo yaliyokuwa yameathiriwa zaidi ni Dar es Salaam na
Morogoro ambako zaidi ya watu 25 walifariki dunia.
Mbali ya vifo hivyo, mvua hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara hasa madaraja.
Mawasiliano ya barabara kati ya Mkoa wa Dar es
Salaam na mingine nchini yalikatika kwa siku mbili baada ya barabara
zake zote zinazouunganisha na maeneo hayo ama kuharibiwa vibaya na
mafuriko au kujaa maji na kushindwa kupitika.
Taarifa hiyo ya TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kuwa kubwa kwani zitazidi milimita 50 katika saa 24.
“Wakazi wa maeneo hatari, watumiaji wa bahari
pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, wanashauriwa kuchukua tahadhari
stahiki,” ilisema taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment