LATEST POSTS

Saturday, July 19, 2014

Aliyemuua mtoto na kula ubongo afariki

Wananchi wakishuhudia mtuhumiwa wa mauaji Laurency Mramba akipandishwa kwenye gari kupelekwa Hospitali ya Kilema kwa ajili ya matibabu baada ya kujikata nyeti zake na kuzila.

Yanawezekana yakawa ni moja ya mauaji ya kutisha nchini, baada ya kijana mmoja kumuua mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi ya Marangu Hills Academy kisha kula ubongo wake.
Mbali na kula ubongo wa mtoto huyo, Francis Urassa (9), mtuhumiwa huyo Lawrence Mramba alijikata sehemu za siri kwa kutumia wembe na kuzila mithili ya mshikaki akikata kipande kimoja baada ya kingine.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo naye alifariki dunia saa chache baadaye baada ya kufikishwa Hospitali ya Kilema iliyopo Moshi Vijijini wakati madaktari na wauguzi wakimpatia matibabu.
Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea jana saa 1:00 asubuhi Kijiji cha Samanga, Wilaya ya Moshi Vijijini, walidai kijana huyo alikuwa na nguvu za ajabu lakini baadae polisi walifanikiwa kumdhibiti.
Wananchi walipiga simu polisi kuomba msaada baada ya kijana huyo aliyekuwa na panga kuwazidi nguvu na kubakia watazamaji wakimwangalia namna anavyokula nyama za mwili wake.
Lilikuwa ni tukio lililovuta hisia za wakazi wengi waliokusanyika kijijini hapo huku wengine wakirekodi tukio la kijana huyo kula uume wake kwa kutumia simu za mikononi.
Polisi kutoka Mji wa Himo walifika eneo la tukio na kumkamata kijana huyo wakati huo akiwa katika hali mbaya kutokana na kupigwa kwa mawe na wananchi na kujikata sehemu mbalimbali.
Mwili wa kijana huyo ulionekana ukiwa umetapakaa damu kuanzia mdomoni hadi sehemu za siri kutokana na damu nyingi kuchuruzika wakati akijikata uume vipande vipande na kuula.
RPC Kilimanjaro anena
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz aliliambia gazeti hili jana kuwa chanzo cha tukio hilo ni upungufu wa akili uliomkumba kijana huyo na kuanza kuvunja vioo vya nyumba.
“Leo (jana) asubuhi alimkata huyo mtoto wa tajiri yake kwa panga na kisha na yeye akaanza kujikata sehemu zake za siri na kula baadaye akajikata pia sehemu mbalimbali za mwili,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, mtuhumiwa huyo alifariki katika Hospitali ya Kilema iliyopo Wilaya ya Moshi Vijijini wakati madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo wakimpatia matibabu.

Mtendaji wa kijiji asimulia
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Samanga, Vick Lyimo alisema siku moja kabla ya mauji hayo, kijana huyo aliyekuwa akijifunza kazi ya Useremala alionekana kuchanganyikiwa kiakili.
Kutokana na kuchanganyikiwa huko, tajiri yake aitwaye Fortunatus Urassa ambaye ni baba wa marehemu, alimchukua na kumpeleka nyumbani kwake kwa ajili ya kupumzika.
Hata hivyo, mtendaji huyo alidai jana saa 1:00 asubuhi, wakati mtoto wa tajiri yake akitoka nyumbani kwenda shule alimvamia na kumpasua kichwa kwa panga na kisha kula ubongo wake.
“Sasa baada ya kula huo ubongo ndio akaanza kujitaka uume wake kipande kwa kipande na kukila mpaka polisi walipofika kwa vile alikuwa akitishia watu kwa panga,” alisema mtendaji huyo.
Mchungaji wake ashikwa na butwaa
Mchungaji Ebeneza Ngomuo wa Kanisa la Pentecoste Marangu alikokuwa akisali mtuhumiwa alisema haamini kilichotokea kwa vile muumini wake huyo alikuwa ni mtu mpole na mtaratibu.
“Ni tukio la kusikitisha na siamini kama huyu kijana yuko sawasawa kwa vile kabla ya tukio alikuwa anaonekana mara zote ni mpole, mtaratibu na asiyetumia kilevi,” alisema mchungaji huyo.
“Sisi kama kanisa tumepata mshangao lakini naamini huu ni mpango wa shetani kwa hali ya kawaida kijana huyo hawezi kufanya unyama huu,” aliongeza mchungaji huyo na kusema;
“Siyo jambo rahisi mtu kula nyama ya binadamu mwenzie na yeye mwenyewe kula nyama zake zikiwamo sehemu za siri... lilikuwa ni tukio baya sana kuliona.”
Mtoto aliyeuawa alikuwa na uwezo kwenye masomo
Mwalimu wa Shule ya Marangu Hills Academy alikokuwa akisoma mtoto Francis, Thomas Malulu alisema tukio hilo ni la uchungu na limewaumiza sana wao kama familia ya shule hiyo.
“Tukio hili ni la uchungu sana kwetu na familia ya Francis. Alikuwa ni mtoto mwenye kipaji darasani na kwa kweli tukio hili limezima ndoto yake,”alisema mwalimu huyo.
Mwalimu huyo alisema tukio hilo limeacha kumbukumbu ambayo itawachukua muda mrefu kuwatoka na kusisitiza kuwa wao kama wanadamu hawana la kufanya zaidi ya kumwachia Mungu.

0 comments: