UPDATE 2 – Karibu watu 108 kati ya wahanga 298
wa ndege ya Malaysia iliyotunguliwa Ukraine Alhamisi walikuwa ni
watafiti wa Ukimwi waliokuwa wakielekea Melbourne kuhudhuria Kongamano
la 20 la Kimataifa la Ukimwi (AIDS 2014).
AFP imevinukuu vyombo vya habari nchini
Australia vikisema kuwa, wakati wa mkutano wa maandalizi ya AIDS 2014
mjini Sidney, washiriki walielezwa kuwa wenzao 100 walikuwa wamepanda
hiyo ndege iliyotunguliwa Ukraine Mashariki.
Kati ya waliofariki yumo mtafiti maarufu wa Ukimwi
toka Uholanzi, Joep Lange, ambaye amewahi kuwa Rais wa Jumuiya ya
Kimataifa ya Ukimwi.
Vilevile, Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa
msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Glenn Thomas, pia amekufa
katika mkasa huo.
Malaysian Airlines imetoa orodha ya wahanga
inayoonyesha kuwa abiria 189 kati ya 298 walokuwa ndani ya ndege hiyo
walitokea Uholazi, huku pia kukiwa na Wamalaysia 44, Waaustralia 27,
Waindonesia 12, Waingereza tisa, Wajerumani wanne, Wabelgiji wanne,
Wafilipino watatu, Mkanada mmoja na abiria mmoja toka New Zealand.
Utaifa wa abiria wanne waliobaki bado haujafahamika.
UPDATE 1 - Hadi kufikia Ijumaa
alfajiri, shirika la ndege la Malaysia limethibitisha abiria 298
wamefariki baada ya ndege yao namba MH17 kutunguliwa Ukraine Mashariki
jana.
Kati ya wahanga wa zahama hilo, 150 walikuwa raia
wa Uholazi walokuwa wakielekea Kuala Lumpur. Imethibitishwa pia kuwa
Waaustralia 27 na Waingereza 9 wamefariki katika shambulizi hilo.
Shirika hilo la ndege limesema litatoa taarifa
zaidi litakapokamilisha shughuli ya kuwatafuta ndugu wa marehemu, huku
ikitangaza kusitisha safari zake zote Ulaya hadi hapo baadaye.
Wakati huo huo, Marekani pia imeyaonya mashirika yake yanayosafirisha abiria yasithubutu kuruka kwenye anga la Ukraine.
FIRST POST - Kiev, Ukraine. Ndege
ya Shirika la Malasyia jana ilitunguliwa mashariki mwa Ukraine na
wanajeshi wanaoiunga mkono Russia na kuua watu 295 waliokuwa ndani,
ofisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine alisema.
Ndege hiyo ‘Malaysia Airlines’ ilikuwa ikisafiri
kutoka Amsterdam kwenda Kuala Lumpur na ilikuwa juu umbali wa futi
33,000 kutoka usawa wa bahari wakati ikitunguliwa.
Ikizidisha hali ya wasiwasi katika mzozo baina ya Mashariki na
Magharibi ukihusisha Kiev na Moscow, ofisa huyo alilaumu “magaidi” kuwa
walitumia kombora la kutokea ardhini kutekeleza shambulizi hilo na
waziri mkuu wa Ukraine alizungumzia kutunguliwa kwa ndege hiyo kuwa ni
“janga”.
Mwandishi wa Reuters aliona mabaki ya ndege hiyo
yakiungua pamoja na miili ya watu ikiwa ardhini kwenye kijiji cha
Grabovo, karibu kilomita 40 kutoka mpaka wa Russia katika eneo ambalo
waasi wanaoiunga mkono Russia wamekuwa wakifanya shughuli zao na wamedai
kutungua ndege nyingine.
Ndege hiyo, Boeing 777 ilidondoka karibu na jiji
la Donetsk, sehemu ambayo ni ngome ya waasi hao, ofisa huyo wa Wizara ya
Mambo ya Ndani, Anton Gerashchenko alisema kwenye ukurasa wake wa
facebook, akiongeza kuwa ndege hiyo ilitunguliwa na kombora aina ya Buk
na watu aliowaita kuwa “magaidi” – neno ambalo serikali ya Ukraine
hutumia kumaanisha wanajeshi wanaotaka kuunganisha nchi ya Ukraine na
Russia.
Watu waliokuwamo kwenye ndege hiyo ni abiria 280 na wafanyakazi 15.
Shirika la Ndege la Malaysia lilisema kwenye
ukurasa wa Twitter kwamba ilipoteza mawasiliano na ndege hiyo namba
MH-17 kutokea Amsterdam. “Sehemu ya mwisho iliyojulikana ilikuwa kwenye
anga ya Ukraine,” ilisema taarifa ya shirika hilo.
Msemaji wa ikulu ya Marekani, Josh Earnest alisema
ofisi hiyo ina taarifa ya ajali hiyo lakini “hakuwa tayari kuthibitisha
“ taarifa zaidi.
Rais Barack Obama ameshataarifiwa na ameagiza timu yake ya usalama wa taifa kuwa karibu na mamlaka za Ukraine, alisema Earnest.
Obama alipuuza swali lililoulizwa kwa kupaza sauti
kuhusu taarifa hizo wakati akiwa njiani kutoka ofisini kwake kwenda
ofisi ya jeshi.
Kutunguliwa kwa ndege hiyo kumekuja miezi minne
baada ya ndege nyingine ya Malaysia, M370 ilipopoteza mawasiliano katika
muda wa chini ya saa moja baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kuala Lumpur na kupotea hadi sasa.
0 comments:
Post a Comment