LATEST POSTS

Wednesday, July 30, 2014

FAHAMU HATUA TANO ZA HIV MWILINI


Leo tutachambua jinsi Virusi vya Ukimwi (VVU) ambavyo pia hujulikana kama HIV  vinavyoingia mwilini na kujiimarisha. Ni somo gumu lakini tutajitahidi kuelezea ili kila mmoja aelewe. Kuna hatua tano ambazo hufanya Virusi vya Ukimwi kuweza kuingia ndani ya seli za binadamu na kuzaliana.
Virusi hao ambao pia kama nilivyosema hapo juu hujulikana kama HIV hutumia kiasili cha CD4 na wana kama njia ya kupita kwani baada ya mtu kupata maambukizi ya VVU kwa njia yoyote ile navyo kuingia ndani ya mzunguko wa damu wa mwanadamu kuna hatua tano hufuata.

Hatua ya kwanza
Virusi hawa wa HIV huanza maisha yao kwa kuunganisha ncha za protini zilizojitokeza kwenye utando wake zijulikanazo kitaalamu gp120 kwenye vipokeo  vinavyoitwa kitaalamu receptors, vya CD4.
Muunganiko huu wa CD4 na gp120 hubadilisha kabisa umbo la gp120 hali ambayo huruhusu HIV kujipachika katika vipokeo visaidizi  yaani co-receptors vilivyoko kwenye utando wa juu wa seli ya binadamu.
Vipokeo hivi visaidizi hujulikana kitaalamu  chemokine receptors CCR5.
Baada ya hapo, aina nyingine ya ncha za protini zilizo kwenye utando wa nje wa HIV ziitwazo gp41 nazo hubadilika umbo lake, na hivyo kuwezesha HIV kuachia aina nyingine ya protini inayoitwa fusion peptide kwenye seli nyeupe ya damu (white bood cells). Protini hii huwezesha utando wa juu wa HIV kuungana na utando  yaani cell membrane wa seli nyeupe inayoshambuliwa.
Hatua ya pili
 Hatua hii HIV kupenya na kuingia ndani ya seli nyeupe ya binadamu kitendo kinachojulikana kitaalamu  kama Viral Penetration/Fusion. Kitendo cha kuungana kwa utando wa juu wa HIV na ule wa seli nyeupe husababisha kutokea kwa tundu katika utando wa seli nyeupe.
Kitendo hiki huwezesha kibeba vinasaba cha HIV na kusukumwa moja kwa moja mpaka ndani ya seli nyeupe ya binadamu kupitia kwenye tundu hilo. 

Hatua ya tatu
Hao HIV hujivua gamba tendo ambalo hujulikana kama uncoating na husaidia kuruhusu vinasaba vyake  pamoja na vimeng’enyo muhimu kwa ajili ya kubadilisha vinasaba vya RNA kwenda DNA, hatua ambayo husababisha kuzaliana kwa virusi wengine wapya.

Hatua ya nne
 Vinasaba vya RNA hubadilika na kuwa DNA ya virusi kwa kutumia kimeng’enyo cha reverse transcriptase. Kitendo hiki hujulikana kitaalamu kama reverse transcription kwa sababu hutokea kinyume na vile kinavyotakiwa kutokea kwa viumbe hai wengine.
Kwa kawaida, kitendo cha transcription hufanyika kwa kubadilisha DNA kuwa RNA na si kinyume kama chake. Baada ya DNA hii ya virusi kutengenezwa ndani ya ute wa seli ya binadamu, hubadilishwa kuwa aina fulani ya RNA iitwayo messenger RNA, yenye uwezo ya kuamrisha seli kufanya kazi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mwili.
Baada ya hapo aina hii ya RNA yenye uzi mmoja hubadilishwa tena kuwa DNA ya virusi yenye nyuzi mbili. Matukio haya yote hufanyika ndani ya ute  unaoitwa kitaalamu cell cytoplasm wa seli nyeupe ya damu.
Hatua ya tano
Hatua hii kitaalamu huitwa integration. Baada ya HIV kufanikiwa kubadilisha RNA yake kuwa DNA, ni lazima sasa HIV aingize DNA hii mpya kwenye DNA ya seli ya damu ili aweze kudhibiti kikamilifu na kuamrisha matendo na kazi zote za seli nyeupe ya damu ili iweze kufanya inavyotaka HIV.

Itaendelea wiki ijayo.

0 comments: