LATEST POSTS

Saturday, July 26, 2014

Katiba Mpya njia panda, Ukawa waapa kuendelea kususia vikao

  Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta akisisitiza jambo juzi, baada ya mkutano wa Kamati ya Maridhiano uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiazimia kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wajumbe wa Bunge hilo ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), viongozi wa kundi hilo wamesema hawatishwi na uamuzi huo na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo.
Kikao kilichokuwa kiwe cha mashauriano kilichoitishwa juzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kiliazimia kuzifanya marekebisho baadhi kanuni za uendeshaji kwa lengo la kusimamia nidhamu wajumbe wake, hatua inayotafsiriwa kwamba inawalenga Ukawa.
Jana Sitta akizungumza na Mwananchi Jumamosi alisema mabadiliko yanayokusudiwa kufanywa yatahusisha masuala ya nidhamu, yakiwamo fujo na utoro, mambo ambayo hivi sasa hayawezi kudhibitiwa moja kwa moja na mwenyekiti wa Bunge hilo.
Sitta alikuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake jana na kusomwa mbele ya waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, ikieleza maazimio ya kikao ya usuluhishi alichokuwa amekiitisha kwa ajili ya kutanzua mzozo unaotishia kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Hata hivyo, Ukawa unaoundwa na wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka Vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe kutoka Kundi la 201 walioteuliwa na Rais, walisusia kikao hicho na kusababisha uamuzi uliofikiwa kuwa wa upande mmoja.
Hata hivyo, wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, viongozi wa Ukawa ambao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na yule CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walisema hawatishwi na mabadiliko ya kanuni yanayokusudiwa kufanywa na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo hadi hoja zao zitakapozingatiwa.
Ukawa walitoka bungeni siku chache kabla ya kuahirishwa kwa awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu mwezi Aprili mwaka huu, kwa madai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia wingi wa wajumbe wake kutaka kufutwa kwa baadhi ya mapendekezo ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
Kauli ya Sitta
Sitta aliliambia gazeti hili kuwa moja ya kasoro katika uendeshaji wa Bunge ni pale makundi kama Ukawa na Tanzania Kwanza yanapotambuliwa kama makundi rasmi ya Bunge Maalumu, wakati makundi rasmi ni wabunge, wawakilishi na Kundi la Wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais.
“Bunge hili lina uhuru wa ajabu ambao ni mkubwa kuliko Bunge jingine lolote, Bunge ambalo hata uongozi wake hauwezi kumchukulia mtu hatua kwa utovu wa nidhamu eti mpaka umuone mtu anafanya makosa, umpeleke kwenye Kamati ya Kanuni na hivyo ndiyo inakuwa imekwisha maana kama ana watetezi wake wanamtetea,” alisema Sitta na kuongeza:
“Matokeo yake wananchi wanalalamika kwamba hakuna nidhamu bungeni na kwamba kiti kimeshindwa kuchukua hatua, sasa unachukuaje hatua wakati kanuni zetu ndivyo zilivyo?”
Aliendelea: “Yako mambo mengi yanapaswa kufanyika na tuna siku 63 tu za kukamilisha kazi tuliyopewa sasa hatuwezi kutumia fedha za umma na watu wengine wanafanya mzaha, leo huyu anachukua posho, mara anaondoka, haya mambo lazima yatafutiwe dawa.”
Kauli hiyo ya Sitta inaungwa mkono na taarifa iliyotolewa mapema jana ikisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge kutokuwa na vipengele vinavyozuia utoro, ukosefu wa nidhamu na matendo mengine yanayolenga kuvuruga mchakato wa Katiba, ni kasoro ambayo lazima itafutiwe ufumbuzi katika kikao kijacho.
Taarifa hiyo inasema kitendo cha Ukawa kuendelea kususia Bunge, kinapuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini na juhudi za usuluhishi za kutaka kuwezesha vikao vya Bunge hilo viendelee.
“Mambo hayo yote yanazua mashaka kuhusu lengo la wasusiaji kwamba pengine ajenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba. Kwa mtindo huu wa kususa ni vigumu kuweza kupata mwafaka” inasomea sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Sitta.
Mbowe na Lipumba
Akizungumzia uamuzi huo, Mbowe alisema haamini kwamba kauli kama hizo zimetolewa na Sitta ambaye ni msomi na mwanasiasa mzoefu anayefahamu misingi ya hoja na maridhiano.
“Kanuni hazitungi Katiba, Katiba inatungwa na utashi wa wale tuliopewa dhamana ya kufanya kazi hiyo, sasa ni kwa bahati mbaya kwamba Sitta anafikiri vitisho vya kutunga kanuni za kutubana vitasaidia, haviwezi kusaidia chochote,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Ukawa hatutishwi na mabadiliko ya kanuni, waende wakabadilishe ili dunia nzima iwashuhudie wakipitisha Katiba ya upande mmoja, wasikwepe hoja wanapaswa kutafakari mantiki ya hoja zetu na siyo kutoa vitisho vya kutulazimisha kwenda bungeni, Katiba ni hiari na wala haitungwi kwa vitisho.”
Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisema Bunge Maalumu la Katiba haliwezi kubadili kanuni ili kumbana au kumfuta mjumbe wa Bunge hilo bila kwanza kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwanza, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kufanyiwa marekebisho na Bunge la Jamhuri ya Muungano na siyo Bunge Maalumu la Katiba. Pili, hata Rais aliyeteua wajumbe 201 wa Bunge la Katiba hawezi kuwafukuza kwa sababu haijaelezwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sasa Bunge la Katiba litaweza vipi kuwafukuza,” alihoji.
Profesa Lipumba alisema wajumbe 201 waliteuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kufafanua kuwa hata wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi nao hawawezi kufukuzwa kwa kubadilishwa kwa kanuni za Bunge la Katiba.
“Mbunge wa Jamhuri ya Muungano au Baraza la Wawakilishi ili apoteze sifa za kuwa mjumbe wa Bunge la Katiba ni lazima kwanza apoteze sifa za kuwa mbunge,” alisema.
Alisema kuwa msimamo wa Ukawa ni kutoshiriki kikao cha Bunge hilo hadi hapo wajumbe wote 629 wa Bunge hilo watakapokubaliana kuheshimu Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi yenye msingi wa muundo wa serikali tatu na siyo serikali mbili.
Taarifa ya Kamati
Mapema katika taarifa iliyosainiwa na Sitta kisha kutolewa kwa waandishi wa habari na Hamad, inaeleza kuwa vikao vya Bunge Maalumu hilo vitaendelea mpaka mwisho hata kama Ukawa wataendelea kususia vikao vyake.
“Kuanzia Agosti 5 Bunge liendelee kwa kuzingatia upya baadhi ya kanuni zake ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kuwa kazi ya kujadili na kupitisha Katiba inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, yaani 60 za nyongeza na tatu pungufu ya zile siku 70 za awali,” inasomeka taarifa hiyo.
Hamad alisema kikao cha juzi kimeamua Bunge hilo kuendelea kutokana na kuwa na masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanawaunganisha Watanzania, yakiwamo usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi, kuikarabati Tume ya Uchaguzi (Nec), kurekebisha kikatiba masuala ya muungano na ukomo wa vipindi vya uongozi.
Taarifa hiyo ilieleza kukerwa na mikutano ya Ukawa inayofanyika katika mikoa mbalimbali nchini. “Hatua ya baadhi ya wajumbe wa Ukawa kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo mwafaka na siyo wakati wake. Bunge la Katiba liwajibike katika siku za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa Katiba kadiri ulivyojitokeza” alisema Hamad.

0 comments: