Wakati jamii ikiwa
bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na kusababisha kifo
chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika Kijiji cha Matongola, Tarafa
ya Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya kubainika mtoto wa miaka sita akiwa
amefichwa uvunguni mwa kitanda na kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama yake
mzazi.
Mtoto Devota Malole. |
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Morogoro, Leonald Paulo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa
taarifa za mateso ya mtoto huyo zilifikishwa Kituo cha Polisi wilayani Kilosa
za saa za mchana jana, baada ya uongozi wa kijiji na kata kutoa taarifa na
tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Mama aliyefanya
ukatili huo anafahamika kwa jina la Sala Mazengo ambaye alimficha ndani mtoto
wake aliyefahamika kwa jina la Devota Malole na kumfanyia vitendo vya kikatili
ikiwa pamoja na kutompa chakula, wala kumfanyia usafi.
Baada ya kufichuliwa
kutoka alipofichwa, mtoto huyo alionekana kuwa dhaifu kiafya kutokana na kukosa
lishe pamoja na mazingira aliyokuwa akiishi kutoridhisha, jambo ambalo ni kosa
kisheria, pia ukiukwaji wa haki za watoto.
Inadaiwa kuwa tangu
mwka 2009 Sala amekuwa akimficha mtoto wake huyo ambaye sasa amelazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu.
Hata hivyo, mwanamke
huyo alipoulizwa alidai kuwa afya ya mtoto wake ilikuwa mbaya tangu alipozaliwa
kutokana na magonjwa ya mara kwa mara, pia hali ngumu ya maisha ilichangia
kudhoofisha afya ya mtoto huyo.
Alidai kuwa ana watoto
sita, pia alikiri kumlaza chini mtoto huyo kutokana na kuwa na kitanda kimoja,
ambacho hakiwatoshi watoto hao. Aliongeza kuwa hata chakula amekuwa akikipata
kwa shida kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda Paulo alisema
kuwa mwili wa mtoto huyo umedhoofu kutokana na kufichwa ndani kwa muda mrefu na
bado mwanamke huyo hajaeleza sababu za kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya
mtoto huyo. “Siwezi kutoa taarifa ya kidaktari, lakini kutokana na afya ya
mtoto yule na mazingira tuliyomkuta ni dhahiri alikuwa akipata mateso na
kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Hata hivyo, uchunguzi
zaidi tunaufanya na kwamba taratibu za kumfikisha mtuhumiwa huyo Kituo Kikuu
cha Polisi mkoani hapa zinaendelea,” alisema Kamanda Paulo.
Alisema kuwa mpaka sasa bado haijafahamika
kama mtoto Davota ni mlemavu au la na kwamba taarifa za afya ya mtoto huyo
zitatolewa baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi wa kina.
0 comments:
Post a Comment