Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa (wa tatu kutoka kushoto) akiwa
katika picha ya pamoja na Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon
Ndesamburo (wa pili kulia) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho,
Japhary Michael (kushoto) na viongozi wengine wa chama hicho
walipomtembelea Slaa nyumani kwake Dar es Salaam jana.
Siku tatu baada ya Baraza Kuu la Chadema kuridhia kumpumzisha
kwa muda Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa baada ya
kutofautiana na Kamati Kuu kwa kumkaribisha waziri mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, kiongozi huyo amesema yupo salama na wakati mwafaka
ukifika atazungumza ya moyoni.
Akizungumza kwa mara ya
kwanza na gazeti hili tangu Chadema imkaribishe Lowassa na hatimaye
kumpitisha kuwania urais kupitia muungano wa Ukawa, Dk Slaa alisema
amekuwa akisikia mengi yakisemwa juu yake lakini yote yamekuwa
yakimchekesha tu.
Hakuhudhuria vikao muhimu vya chama
hicho na vile vya Ukawa, vikiwamo; wakati Lowassa akitambulishwa rasmi,
akichukua fomu, kikao cha Baraza Kuu na juzi Mkutano Mkuu na hakuwa
akipatikana kwa simu yake ya mkononi.
Wakati kimya kikitawala juu ya hatima yake, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kuwa amejivua uanachama Chadema.
Lakini
jana alisema: “Naangalia mambo mengi yanayoendelea kwenye mitandao
halafu ninacheka tu, usifikiri sifuatilii, nafuatilia kinachoendelea na
ninabaki nikicheka.”
Kuhusu hatima yake kisiasa na
madai ya kujiuzulu uanachama ndani ya Chadema, alisema hawezi kuzungumza
lolote kwa sasa na atafanya hivyo wakati mwafaka ukifika. “Usijali
wakati wangu wa kuzungumza ukifika nitasema tu, sasa hivi nawaachia
mzungumze, lakini nitazungumza,” alisema.
Kadhalika,
alipoulizwa kuhusu taarifa zilizozagaa kuwa maisha yake yapo hatarini
kwa kuwa anatishwa, Dk Slaa alisema hata hilo pia atalizungumzia wakati
mwafaka ukifika.
“Ndiyo hayohayo ninayosema, wala msijali nitazungumza wakati ukifika,” alisema na kusisitiza: “Nipo salama.”
Dk Slaa alisema kwa sasa yupo mapumzikoni nje ya jiji la Dar es Salaam ingawa hakutaka kueleza ni eneo gani.
Juzi,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifafanua tofauti iliyojitokeza
kati ya Kamati Kuu ya Chadema na Dk Slaa wakati wa mchakato wa kumpokea
Lowassa.
Katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Chadema,
Mbowe alisema wamekubaliana katibu mkuu huyo apumzike kwa muda... “Nina
hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na
yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri
wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.”
Ndesamburo na siri nzito
Mbunge
wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo na makada wengine wa Chadema, jana
walikwenda kuonana na Dk Slaa nyumbani kwake na kufanya naye kikao cha
faragha.
Picha zilizomuonyesha Ndesamburo akiwa na Dk
Slaa na makada wengine akiwamo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Jaffar
Michael, zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii jana na kuibua
mijadala.
Baadhi ya waliochangia mijadala hiyo
walidokeza kuwa huenda Ndesamburo anayeheshimika ndani ya chama hicho
alikwenda kujaribu kusawazisha hali ya mambo.
Mkuu wa
Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwa picha hizo ni
halisi, baadhi zilipigwa juzi na nyingine jana mchana, lakini hakutaka
kuingia undani wa mkutano wa wanasiasa hao.
Ndesamburo
alithibitisha kukutana na Dk Slaa: “Ni kweli tulikwenda, kwani kuna
tatizo gani? Si mzee mwenzangu? Halafu bado ni mwanachama wetu, hajatoka
Chadema, hivyo tuna kila haki ya kwenda kumsalimia.”
Alipoulizwa
kama alikwenda kumsihi Dk Slaa arejee kuendesha mapambano ya kuing’oa
CCM, Ndesamburo alisisitiza kuwa walikwenda kumsalimia.
Michael alipoulizwa nia ya safari hiyo alijibu kwa kuuliza; “Dk Slaa ni katibu mkuu wetu kwani tunazuiwa kwenda kumsalimia?”
Dk
Slaa aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili baada ya Rais
Jakaya Kikwete na ndiye aliyekuwa akitajwa kuwania tena nafasi hiyo
kupitia Chadema na Ukawa kabla ya “kubadili gia angani” na kumteua
Lowassa.
0 comments:
Post a Comment